Dar es Salaam. Wakati tafiti zikionesha wajasiriamali wadogo na wakati wakikabiliwa na changamoto lukuki zinazowafanya wasipige hatua, waaalamu wametoa suluhuhisho ya kukabiliana na changamoto hizo.
Ukosefu wa mitaji, ukosefu wa masoko ya uhakika ya bidhaa yao, kukosa maarifa na elimu ya fedha ni miongoni mwa changamoto zinazotajwa kudumuza sekta hiyo endapo hatua mathubuti hazitachukuliwa.
Hatua hizo zimeelezwa leo Ijumaa, Julai 5, 2024 wakati wa Kongamano la Wajasiriamali Wadogo, Wa chini na Wa kati (MSMEs) lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) lililobebwa na kaulimbiu ‘Kuboresha, kuendeleza ujuzi na kukuza biashara zinazochipukia, ndogo na za kati’.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Tobias Swai amesema ni vizuri kwa wajasiriamali kuwa rasmi kwa maana kufanya biashara yao kwa mifumo inayoeleweka.
“Mifumo ya fedha mifumo ya kujiajiri na mifumo yote inayotakiwa ili biashara iwe na uhakika iisipitie katika nyakati ngumu,” amesema.
Dk Swai amewashauri pia kuacha kufanya biashara kwa kuzoea akitolea mfano kuajiri tu mtu unayemjua kwa kusema njoo tu ukae tufanye biashara bila ya kufuata utaratibu.
Mbali na hilo, Dk Swai amesema kufanikiwa kwa wajasiriamali wadogo kunategemea pia maarifa hivyo ni muhimu kwao kutafuta zaidi maarifa ya ujasiriamali kupitia machapisho yanayoandikwa akitolea mfano yale ya watalaamu wa uchumi na ujasiriamali wa UDSM yanayopishwa kwenye Gazeti la Mwananchi kila Alhamisi.
Kwa upande wake, Meneja Miradi kutoka CRDB Benki Foundation, Baraka Kiyalo amesema ili kuwawezesha wajasiriamali waweze kukua nchini, lazima wapate uwezeshi ikiwemo elimu ya fedha.
Kutokana na hilo, Kiyalo amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya kijasiriamali pamoja na elimu ya usimamizi wa fedha.
Kupitia programu ya IMBEJU taasisi hiyo ya kifedha imeamua wajasiriamali wanufaike. kuwawesesha kwa kuwapa mafunzo na namna ya kusimamia fedha.
“Tunawazesha mtaji kuanzia Sh200,000 ili kila mmoja anufaike ikiwa sharti letu kubwa ni waaminifu. Lengo ni kila mmoja anayetaka kuwa mjasiriamali atimize malengo yake.” amesema Kiyalo.
Suala la mikopo na uwezeshaji kwa wajasiriamali lilizungumziwa pia na Ofisa Mtendaji Mkuu Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo ambaye ameeleza benki hiyo imetenga Sh300 bilioni kwa ajili ya mikopo hiyo.
Amesema katika kipindi cha miezi sita tayari imeshatoa mipango ya Sh151 bilioni kwa wajasiriamali 2,481 na pia mapitio ya mpango mkakati wa miaka mitano mwanzoni mwa mwaka huu ili kuigusa sekta ya MSMSe ambayo ni muhimu.
Mkuu wa masoko na tehama wa Tigo Business, Norman Kiondo amesema Tigo imewekeza zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu yao ikiwa ni hatua ya kwanza katika kuweka mazingira wezeshi ya utumiaji huduma za mtandao.
“Hatua ya pili ni kuwezesha watu waweze kutumia mtandao wako, kulikuwa na changamoto kubwa ya watu kuweza kumudu gharama za vifaa ili waweze kutumia mtandao.Tumeweza kuanzisha simu za mikopo ili watu waweze kutumia simu zao kupata taarifa mbalimbali,” amesema Kiondo.
Mtaalamu wa Uthibitisho wa Kiwango cha Kimataifa Mradi wa UNIDO-QUALITAN, Dk Ali Qazilbash amesema wamekuwa wakiboresha mazingira ya MSME kwa kufanya kazi na wadau mbalimbali ili kuwafikia.
“Tunahakikisha wanapata habari, kwa kufanya kile kinachohitajika kulingana na viwango na kufuata mahitaji ya soko na ndivyo tunavyofanya.Tunatambua mapungufu, tunatengeneza miongozo na TBS na Sido, na tuna mafunzo ya mtandaoni kuhusu mabadiliko na ubora,” amesema Dk Qazilbash.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Emmanuel Chao amesema biashara yoyote ni kama mtoto akiwa na maana kwamba biashara ndogo lazima ilelewe na sehemu kubwa ya jamii na si mtu mmoja.
Amesema katika biashara kuna ushindani na siku zote kuna nafasi ya aliyebora, akisema siku zote aliyebora ana nafasi.
Amesema biashara nyingi huwa hazikuwi kwakuwa hazina falsafa na ni vigumu kufika kwenye biashara kubwa kama nia yako ya kufika huko juu ni ndogo.
Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Victor Mushi amesema wajasiriamali wanapaswa kuamka ili kujiendeleza zaidi.
Sambamba na hilo amesema ndio maana MCL ikaamua kuja na Kongamano linalowahusu ili kuwawezesha kukua kama dhima ya kuliwezesha taifa.
“Kongamano hili linawezesha Taifa kama ilivyo dhima ya kampuni. Hapa tumejifunza mambo mengi ya kijasiriamali, lengo ikiwa ni kutanua wigo wa fursa za kibiashara ili kukuza mchango wa biashara hizi katika uchumi wetu.”
Amesema katika kongamano hilo wamekuja wadau, sekta binafsi, wajasiriamali wenyewe na Serikali ambapo wote wameahidiana kusaidiana ili kukuza sekta hiyo.
“Kongamano hili ni wezeshi na matokeo yake tutauyaona mitaani katika mafanikio ya wajasiriamali hawa,” amesema.
Mushi ameongeza:”Tunayo huduma ya Mwananchi Courier ambayo tunafanya huduma za kusafirisha mizigo yenu kwa usalama na unafuu hivyo changamkieni fursa hii.”