WATAALAM wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) wakiongozwa Mtendaji Mkuu wake Dkt. Stella Bitanyi wameendelea kutoa elimu kuhusiana na huduma mbalimbali zinazotolewa na TVLA katika Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa ya Dar Es Salaam (Sabasaba) tangu yalipoanza Juni 28, 2024 na kutarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2024.
Akizungumza katika maonesho hayo Julai 05, 2024 Dkt. Bitanyi amesema kuwa katika Maonesho hayo TVLA imekuja kutangaza na kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na TVLA, ikiwemo umuhimu wa uchanjaji wa Mifugo, utambuzi wa magonjwa ya wanyama, uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo, utafiti wa magonjwa ya wanyama na ushauri kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo.
Aidha Dkt. Bitanyi aliongeza kuwa TVLA inatoa elimu ya udhibiti wa wadudu aina ya mbung’o pamoja na kuwadhibiti wadudu hao ambao hueneza ugonjwa wa Nagana.
Aliongeza kuwa TVLA inatoa elimu ya kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe kama ndigana kali na ndigana baridi kwa kuhakiki ubora wa viuatilifu kwa ajili ya kuogesha wanyama ili kudhibiti kupe.
“Tunaendelea kuwakaribisha wananchi wote waliopo ndani ya viwanja vya maonyesho ya Sabasaba na maeneo mengine, kutembelea banda letu la TVLA lililopo kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kupata elimu kuhusiana na udhibiti wa magojwa ya wanyama, chanjo za mifugo zinazozalishwa na TVLA, ufugaji pamoja na uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo.” Alisema Dkt. Bitanyi.
Baadhi ya wadau wa Mifugo waliotembelea banda la TVLA wamefurahishwa na huduma zinazotolewa hasa elimu ya uchunguzi wa magonjwa ya Mifugo kabla ya kuwatibu pamoja na elimu ya uchanjaji wa Mifugo kwani walikuwa wanachanja Mifugo yao bili kuipima kitu ambacho kilikuwa kinasabasha vifo kwa Mifugo yao.
Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa ya Dar Es Salaam (Sabasaba) yanayokutanisha wafugaji, wakulima, wafanyabishara na wajasiriamali kutoka kila pande za Dunia. TVLA imeshiriki kwa kuonesha teknolojia mbalimbali za kitaalamu na za kiubunifu.