Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki, kimemtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Shahada ya Heshima (Honoris Causa) katika Uchumi, ikiwa ni kutambua juhudi zake za kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi na kuiishi falsafa yake ya 4R.
Rais Samia ametunukiwa Shahada hiyo na Profesa Necdet Unuvar wa chuo hicho, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake, pia wameiheshimisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Samia amekishukuru Chuo Kikuu cha Ankara kwa kumpa heshima hiyo kubwa duniani, akisema ameipokea kwa furaha, akiamini uamuzi wao huo ni ishara njema kwa Taifa la Tanzania.
“Natoa shukrani zangu kwa Seneti ya Chuo Kikuu cha Ankara kwa uamuzi wa kunipa Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Uchumi. Nawashukuru kwa heshima hii kutoka kwa chuo kikuu hiki maarufu, kilichopo kwenye nchi ambayo elimu yake inachukuliwa kuwa ni ya daraja la juu duniani,” amesema Dk. Samia.
Rais Dk. Samia pia anatarajiwa kuelekea jijini Istanbul, mji mkuu wa kibiashara wa nchi ya Uturuki kushiriki Kongamano la kibiashara la Tanzania na nchi hiyo linalotarajiwa kuhudhuriwa na Makamu wa Rais wa Uturuki.