Hiki ndicho anachokipeleka Baleke Yanga

HII sasa sifa. Hizi huenda zikawa taarifa za kushtukiza kwa mashabiki wa soka nchini, kwamba baada ya Yanga kumbeba Clatous Chama kutoka Simba na Prince Dube aliyekuwa Azam, sasa imemshusha kikosini, Jean Baleke aliyewahi kuwika na Wekundu wa Msimbazi miezi sita tu iliyopita,  lakini hiki ndicho anachokwenda nacho Jangwani.

Ndio, hivi unavyosoma Mwanaspoti ni kwamba Baleke amesaini mkataba wa mwaka mmoja na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa rasmi kuitumikia timu hiyo akiungana na Chama na Jonas Mkude aliowahi kucheza pamoja wakiwa Msimbazi.

Alijiunga Simba katika usajili wa dirisha dogo la msimu 2022/23 na akamaliza na mabao manane na katika msimu ulioisha alioachwa katika dirisha dogo alifunga mabao manane, hii ikiwa na maana kwa mwaka mmoja alioitumikia timu hiyo ya Msimbazi ameifungia mabao 16 katika Ligi Kuu Bara.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 aliyewahi kukipiga FC Aigles RDC, Nejmerh SC na Mazembe, kabla ya taarifa za kusaini Yanga, Simba iliripotiwa kurudi kuhitaji tena huduma yake, ambapo ilielezwa aliwahi kufuatwa na Juma Mgunda, lakini hawakufanikisha dili hilo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mabosi wa Yanga wameona Baleke ni mtu sahihi kumchukua kuliko Jonathan Sowah waliyekuwa wakimwinda tangu akiwa Medeama kabla ya kusajiliwa Al-Nasr Benghazi pia ya Libya.

Mwanaspoti lililowadokeza mapema kwamba mshambuliaji huyo Mkongomani aliyekuwa akicheza Libya alikuwa kwenye mazungumzo na Yanga na ilikuwa imebaki suala la kusaini tu, jambo ambalo limefanyika juzi na sasa Baleke ni Mwananchi.

Chanzo makini kutoka ndani ya Yanga kimesema Baleke amesaini mwaka mmoja na endapo akifanya vizuri, ataongezewa mwingine. 

“Kasaini tayari, ishu inakuja ni kumalizana na TP Mazembe kwani bado ana mkataba nao, hata timu ya Al-Ittihad alikuwa anacheza kwa mkopo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Viongozi wanalishughulikia hilo, tayari wameanza mazungumzo na uongozi huo pia kufuatilia barua yake ya timu ambako alikuwa anacheza Al-Ittihad na mambo yakiwa freshi wanamtambulisha muda wowote.” 

Related Posts