Aliyedaiwa kumuua shangazi yake kwa imani za kishirikina ahukumiwa kunyongwa

Geita. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita imemhukumu kunyongwa hadi kufa, Peter Lameck (27) baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua shangazi yake, Isanziye Mwinula (67) akimtuhumu kuwaua wazazi wake pamoja na mtoto wake kwa imani za kishirikina.

Hukumu hiyo imetolewa leo Julai 5, 2024 na Jaji wa Mahakama hiyo, Griffin Mwakapeje baada ya kumtia hatiani kwa kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Jaji Mwakapeje ameeleza kuwa kwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na ukiri wa mshtakiwa umethibitisha pasi na shaka kuwa marehemu aliuawa na mshtakiwa huyo.

Ameeleza kuwa Mahakama hiyo haiwezi kukubaliana na na uamuzi wa kujichukulia sheria mkononi kwa kuua kwa imani za kishirikina na kwamba uamuzi wake wa ukiri umeonyesha nia ovu aliyokuwa nayo.

Ameeleza kuwa kwa mazingira yaliyotolewa, Mahakama imeshawishika na ushahidi uliotolewa pasipo kuacha shaka na kuwa mshtakiwa alikuwa na nia ovu ya kumuua shangazi yake.

Shauri hilo namba 78 ya mwaka 2022 lilikwenda Mahakamani kwa ajili ya hukumu ambapo Peter Lameck alishtakiwa kwa kosa la mauji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Imeelezwa kuwa  Machi 22, 2021 katika kijiji cha Bwina, wilayani Chato, mshtakiwa alimuua shangazi yake Isanziye Mwinula (67) na Julai 25, 2022 shahuri hilo lilifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza na mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo.

Amedai kutokana na uzito wa kosa kuwa kubwa, upande wa mashtaka uliomba shauri hilo lisikilizwe kwa ukamilifu wake na hivyo kuifanya Mahakama kutokana na mazingira ya mshtakiwa kukiri kosa, apewe nafasi ya kusikilizwa na upande wa mashtaka ulete mashahidi wa kuthibitisha.

Ameeleza katika kuthibitisha mashtaka upande wa Jamhuri walikuwa na mashahidi sita na vielelezo vitatu ambavyo ni ungamo kwa mlinzi wa amani,ukiri wa mshtakiwa pamoja na taarifa ya uchunguzi wa kifo cha marehemu .

Katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wa pande zote ikiwemo mshtakiwa mwenyewe ni kuwa suala hilo lilitokea ndani ya familia na lina sura ya familia ambapo mshtalkiwa na marehemu ni ndugu wa karibu na mshtakiwa alikua akimuita marehemu Shangazi.

Hata hivyo, Jaji alieleza toka kuzaliwa, mshtakiwa hakuwahi kufaidika na upendo wa wazazi na alielezwa na babu yake kwamba wazazi wake walifariki wakati akiwa mdogo na chanzo cha kifo kilisababishwa na shangazi yake ambaye aliwaloga kupitia uchawi.

Kutokana na misuguano kuendelea kuwa mikali baada ya mtoto wa mshtakiwa kufariki, katika kuomboleza, mshtakiwa alishawishika kuwa shangazi yake kwa namna moja au nyingine anahusika baada ya kifo cha mtoto wake.

“Uchungu wa kupoteza wazazi na mtoto wake ulimfanya kuamini kuwa shangazi yake anahusika na hivyo yeye kutaka kulipiza kisasi na siku ya tukio Machi 22, 2021, inaelezwa kwamba marehemu alienda nyumbani kwa mshtakiwa akiwa amelewa.

“Akiwa pale aliuliza marehemu kama anafahamu watu waliohusika na vifo vya wazazi wake na mtoto wake na marehemu alimwambia yeye anafuatia baada ya ndugu zake kutangulia mbele za haki,” amesema.

Hata hivyo, ilipofika saa tatu usiku, mshtakiwa aliondoka nyumbani kwake akiwa na kisu akiwa na nia ya kumuua shangazi yake ili asiweze kumletea madhara zaidi na baada ya kufika kwenye nyumba ya shangazi yake alikuta jembe alilolitumia kumshambulia shangazi yake mara kadhaa kwenye mwili wake.

Imeelezwa kuwa wakati anamshambulia shangazi yake, alipata maumivu na kukimbilia kwa jirani na kuanguka mlangoni na kutokana na vurugu zilizoendelea shahidi namba nne na namba tano walisikia mtu akipiga kelele akidai amemuua shangazi yake akiwaomba wawaite polisi.

Majirani hao waliamka na kukuta mwili wa marehemu ukiwa mlangoni na mshtakiwa akiwa amesimama na kwa ushahidi wa shahidi namba tano alieleza kumkuta mshtakiwa  akiwa na silaha ya jembe mwili wa marehemu ukiwa pembeni yake.

Imeelezwa kuwa mshtakiwa alikiri kumuua shangazi yake kwa sababu ya uchawi alioamini ulipelekea vifo vya wazazi na mtoto wake.

Uchunguzi wa kidaktari ulithibitisha kuwa marehemu alikuwa na majeraha makubwa kwenye ubongo yaliyotokana na maumivu kwenye kichwa, majeraha kifuani na mgongoni.

Amedai mshtakiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo kutokana na hasira na imani ya ushirikina kuwa shangazi yake aliua wazazi na mtoto wake pamoja na kuwa na hofu kuwa shangazi huyo angemuua na yeye hivyo katika kuokoa maisha yake alimuua shangazi yake.

Jaji Mwakapeje ameeleza baada ya Mahakama kuona ushahidi uliotolewa, swali la kujiuliza ni, je, mshtakiwa alikuwa na nia ovu ya kutekeleza mauji hayo ya shangazi yake?

Ameeleza katika ushahidi uliotolewa kuwa hakuna shahidi aliyeona kwa macho mshtakiwa kumpiga marehemu, hivyo ni muhimu Mahakama ikaangalia kwa kina kama kweli mshtakiwa alihusika na kifo cha shabgazi yake.

Katika shauri hilo ushahidi wa kimazingira unathibitika pale ambapo mshtakiwa mwenyewe alikiri  kumpiga marehemu kwa jembe na jambo la pili ni marehemu kukutwa kwenye mlango wa shahidi namba nne na mshtakiwa akipiga kelele akidai amemuua shangazi yake na kutaka polisi waitwe huku akiwa ameshika jembe mkononi.

Jaji Mwakapele ameeleza kuwa zaidi ya hayo mshtakiwa hakukimbia na alikamatiwa  eneo la tukio na katika uchunguzi wa tukio mshtakiwa hajabadilisha ukiri na ameendelea kukiri polisi,kwa mlinzi wa amani ,na hata baada ya kupandishwa mahakamani ameendelea kukiri kumuua shangazi yake.

Jaji ameeleza katika mazingira hayo mnyororo wa ushahidi haujakatika na mazingira ya ushahidi yanamnyooshea kidole mshtakiwa.

Mwakapeje ameeleza kuwa mwongozo wa Mahakama ya Rufani katika shauri kama hilo mshtakiwa mwenyewe amekiri kuondoka na kisu nyumbani kwake na hii inaonekana kwenye maelezo ya ungamo na maenelezo ya onyo na hata Mahakamani na pamoja na kuwa na kisu alipofika hakutumia kisu na badala yake alitumia jembe.

Amesema katika matukio ya hatari jembe litakuwa silaha endapo litatumika kwa nia ya kudhulu na kuongeza nguvu iliyotumika kwa mujibu wa ushahidi, mshtakiwa alimpiga marehemu kwa jembe na kumsababishia maumivu yaliyomfanya akimbilie kwa jirani lakini mshtakiwa hakutosheka aliamua kumfuatilia na kuendelea kumpiga .

Kutokana na kitendo cha mshtakiwa kutokimbia baada ya kutenda kosa hilo, tabia hiyo imeelezwa kuwa mshtakiwa aliridhishwa na kitendo alicho kifanya na matendo hayo yanaonyesha anaweza kulipiza kisasi kuua mtu mwingine na kwa mazingira hayo yanadhihirisha kuwa mshtakiwa alikuwa na nia ovu.

Jaji Mwakapeje ameeleza mshtakiwa alitembelewa na shangazi yake saa mbili usiku na saa tatu alikwenda kwa shangazi yake kutekeleza azma yake ya kuua na kwamba kwa muda wa saa moja mshtakiwa huyo alikuwa na uwezo wa kutafakari asitende kosa.

Ameeleza kuwa Mahakama hiyo ni ya kisheria, hivyo haiwezi kukubaliana na uamuzi wa kujichukulia sheria mkononi kwa kuua kwa imani za kishirikina na kwamba Mahakama imeshawishiwa na usahidi pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alikuwa na nia ovu ya kumuua shangazi yake.

Wakili wa Jamhuri, Musa Mlawa ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa huyo hana kumbukumbu nyingine za makosa lakini alikuwa na uwezo wa kutatua hisia alizokuwa nazo kwa njia nyingine pasipo kuua, hivyo kuimba Mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Wakili wa utetezi, George Alfred aliiomba Mahakama kumpa mshtakiwa adhabu nafuu kwa sababu ni kosa la kwanza na mshtakiwa hana rekodi ya uhalifu na kwamba bado ni kijana mdogo na ameshakaa ndani kwa miaka mitatu lakini pia hakuisumbua Mahakama.

Kufuatia ungamo hilo, Jaji Mwakapeje ameeleza kuwa kwa kosa lililofanywa na mshtakiwa adhabu pekee iliyopo ni kifo kwa kunyongwa, hivyo Mahakama imemhukumu kunyongwa hadi kufa.

Related Posts