Katavi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limeeleza mafanikio ya operesheni, doria, misako na hatua za kesi zilizofikishwa mahakamani ambapo watu 74 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa makosa mbalimbali ikiwemo watu 12 kutuhuma kuhusika na mauaji ya wanafamilia.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Julai 5, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amesema operesheni ya kupambana na wahalifu inayoendelea katika mkoa huo kwa Juni pekee, watu 74 wanashikiliwa huku 12 wakituhumiwa na makosa ya mauaji.
Ngonyani amesema mauaji yaliyotokea katika kipindi cha mwezi mmoja ni wanafamilia kuuana wenyewe kwa wenyewe kutokana na visa vya kulipiza visasi na vifo vingine vinatokana na wivu wa kimapenzi. Amesema hiyo imetokana na kuwepo kwa mwingiliano wa watu wengi wanaotoka maeneo mengine kuhamia Katavi.
“Operesheni yetu tuliyoanza tangu Juni kwa kufanya misako na doria, tumefanikiwa kukamata watu 74 kwa makosa mbalimbali wakiwemo watu 12 ambao wanatuhumiwa kwa mauaji. Tumefuatilia mauaji haya tumegundua yanatokana na kulipiza visasi vya familia kwa familia.
“Hii imesababisha familia nyingi kupoteza maisha ya watu wao na vifo vichache ambavyo vinasababishwa na wivu wa mapenzi,” amesema Kamanda Ngonyani.
Amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria za nchi na hawatasita kuchukua hatua kali kwa mtu yeyote ambaye anakutwa na makosa ya mauaji na makosa mengineyo.
Katika operesheni hiyo, watu 30 wamekamatwa kwa makosa ya unyang’anyi, uporaji nyakati za usiku huku mtu mmoja akikutwa na silaha aina ya gobore ikiwa na risasi mbili huku wengine 24 wakikamatwa kwa kutengeneza pombe moshi kiasi cha lita 251 na watuhumiwa saba wakiwa na kete 287 za dawa za kulevya aina ya bangi.
Mkazi wa Manisapaa ya Mpanda, Joel Samweli amesema: “Kweli matukio ya watu kuuana yamekithiri hasa vijijini katika Wilaya za Tanganyika na Nsimbo. Kwa hapa Mpanda, ni mara chache sana kusikia mtu ameuawa wa kulipiza kisasa au wivu wa mapenzi ninachoomba Serikali itoe elimu kwa Wananchi ili kuzuia watu wasiuawe,” Samweli.
Kwa upande wake, Rebecca Ismail amesema: “Mauaji mengi yanatokana na imani za kishirikina ili kutafuta utajiri na jambo hili limekuwa tatizo sana katika familia zetu kwani pia kuna wanawake wanaua wanaume zao ili wabaki na mali,” amesema Rebecca.
Kwa upande wake, mwananchi mwingine, Lilian Vincent ameeleza kuwa mauaji ya visasi yanatokana na watu kuzulumiana mali au mashamba jambo hilo linasababisha familia na familia kulipizana visasi kwa kuuana.
“Mauaji ya familia na familia yanatokana na watu kudhulumiana mali, ninaishauri jamii kuwa na moyo wa kusameheana na kuimarisha malezi mazuri kwa watoto ili tusiwalee kwenye mazingira yatakayosababisha kujenga kinyongo cha kulipiza visasi,” amesema Lilian.