Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana amepongeza hatua inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kuangalia upya mfumo wa kodi bandarini.
Amesema mifumo iliyopo sasa imekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi hivyo mabadiliyo yanayotarajiwa ya kuiboresha na kubadili mifumo hiyo, itaongeza ufanisi na kurahisisha biashara.
Mbwana amesema hayo leo Julai 5,2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kwa mlipa mlipa kodi inayotolewa na TRA kwa wananchi katika maonesho ya biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa kutokana na elimu waliyoipata, ni dhahiri kuwa mifumo hiyo itawasaidia katika kukuza biashara zao na kutimiza lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kukuza uchumi wa nchi.
“Niwaombe wafanyabiashara wenzangu kwenda kwenye maonesho ya Sabasaba kwani watajifunza masuala mengi ya biashara na kwa kuwa kujifunza hakuna mwisho, watapata elimu na kutatuliwa changamoto mbalimbali za kikodi zinazowakabili,” amesisitiza Mbwana.
“Maonesho ya Sabasaba ni ya wafanyabiashara na taasisi nyingine hivyo zipo fursa mbalimbali za biashara ambazo wanapaswa kuzichangamkia kupitia maonesho hayo”. Amesema
Ameongeza kuwa amejifunza vitu vingi sana…..,niseme tu kuna tofauti kubwa kati ya kumfata mtu ofisini kwake na kwenye maonesho haya, utapata elimu nzuri ambayo itakusaidia katika utekelezaji wa majukumu ya kibiashara,” alisema Mbwana.
Afisa Mkuu wa Forodha TRA Shuweikha Salum Khalfan kushoto akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafabyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana (aliyevaa kofia) alipotembelea banda la 77 wakati wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo Julai 5,2024 katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam