Mwanza. Katika hali isiyo ya kawaida, mwananfunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Isenga wilayani Ilemela (jina limehifadhiwa) anadaiwa kuiba Sh150,000 kisha kujiteka yeye na mdogo wake wakati wanakwenda shuleni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Julai 5, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema baada ya mtoto huyo mwenye miaka 12 kujiteka, alimtaka mama yake kutuma fedha ili aachiwe akidai katekwa na watu wasiojulikana.
Mutafungwa amesema mama huo alipeleka taarifa kituo cha polisi akidai watoto wake hao wametekwa na watu wasiofahamika na yeye anapigiwa simu na watu hao wakimtaka atoe fedha ili waachiwe.
Amesema baada ya jeshi hilo kupata taarifa hiyo, lilifungua jarada la uchunguzi na kuanza kufuatilia ambapo ilipofika Julai 4, 2024 saa 8:30 mchana waliwapata watoto hao katika Mtaa wa Shibayi wilayani Nyamagana.
“Walipatikana wakiwa wameomba hifadhi katika chumba kimoja wapo cha nyumba inayomilikiwa na Agness Magusu (50) ambaye anaitumia nyumba hiyo kwa biashara ya upangishaji,”amesema Mutafungwa.
Amesema uchunguzi wao umebaini kuwa Julai 3, 2024 mtoto huyo aliiba Sh150,000 ya mama yake kisha kwenda nazo shuleni akiwa amezificha kwenye moja ya madaftari yake.
“Kabla ya kufika shuleni alibadili sare za shule na kuvaa gauni kisha kuondoka na mdogo wake (8) wakaelekea maeneo ya Buhongwa, wakafika kwenye hiyo nyumba ya Agness na kumuomba awapatie chumba kwa ajili ya kupanga…mama huyo alikataa na akamtaka binti huyo awasiliane na wazazi wake,” amesema Mutafungwa.
Ameongeza kuwa: “Ndipo binti huyo akaanza kupiga simu kwa mama yake mzazi akimdanganya kwamba yeye pamoja na mdogo wake wametekwa na akawa anamuomba mama yake amtumie kiasi kingine cha fedha ili kuwapa wale waliomteka waweze kumuachia.”
Kamanda huyo amesema mama huyo hakutoa fedha badala yake alienda kuripoti tukio hilo polisi, kisha msako wa askari wa jeshi hilo ulifanikisha kuwapata huku mtoto huyo akiwa tayari kanunua godoro la futi tatu kwa sita, simu ya mkononi na vyombo kwa ajili ya matumizi ya ndani kwa kutumia fedha alizomuibia mama yake.
“Katika mahojiano mtoto huyo alikiri kwamba hakuna utekaji wowote uliokuwa umefanyika. Niendelee kuwakumbusha wazazi kuwa karibu na watoto wao sababu inaonekana watoto wengi huko mitaani wanajilea wenyewe, wazazi wamekaa mbali wakijipa ‘ubize’ huku wakiwaacha watoto wakitembea na kuwa na maamuzi makubwa ambayo si mazuri,”amesema Mutafungwa
Mama wa watoto hao, Sarah Charles amedai kushangazwa na tukio hilo kwa kuwa binti yake hakuwahi wala hajawahi kumuona na tabia ya kuiba, wala kupata malalamiko yoyote mabaya mtaani kuhusu mtoto wake.
“Zile pesa nilitoka nazo kanisani, nikafika nyumbani jioni nikamwambia akae na hizo hela maana siyo mara ya kwanza kumpa hela…kaa nazo nitakuomba kesho asubuhi unikumbushe akasema hakuna shida mama sasa kulipokucha nikawaamsha kujiandaa kwenda shule. Nikawaandaa, nikamaliza wakatoka…walivyotoka nikasahau kumuomba ile ela, akatoka akaenda shule”amesema mama huyo.
Amesema siku hiyo akiwa amelala nyumbani kwake saa 8:30 mchana alitumiwa ujumbe mfupi (sms) kwa namba ambayo haifahamu ikimtaka apige simu, alivyomuuliza yeye nani alimjibu apige simu na yeye kumwambia hana salio kisha namba ile kumpigia sauti anayodai ilikuwa nzito japo ilikuwa ya binti ikimwambia watoto wake wametekwa.
“Akaniuliza nipo wapi nikamwambia nipo nyumbani akaniambia watoto wako wametekwa…wamevaa nguo za shule mmoja amevaa nguo flani anataja kama kweli nikamwambia akate simu…nikafuatilia shuleni,”amesema
Ameongeza kuwa, baada ya kufuatilia shuleni aliambiwa na walimu kuwa mtoto wake mkubwa na yule mdogo wote hawakufika shuleni siku hiyo nakuamua kuitafuta namba hiyo tena.
“Badaye nilivyowasiliana naye akasema dada mimi nakulelea watoto wako, nikamwambia watoto wangu wametekwa dada niambie mpo wapi akasema subiri nikupe uongee naye…,”
Amesema alipopewa simu azungumze na binti yake na kumuuliza alipo yeye na mdogo wake alimjibu hapajui nakumtaka ampe simu mdogo wake ambaye alilia badala ya kuongea naye.
“Hawa watoto nimewalea malezi mazuri sana..sielewe hata mimi kilichomkuta huyu binti. hata sasa hivi sielewe..ana mika 12 sielewi yaani,”amesema