Dar es Salaam. Siku mbili tangu Shadrack Chaula (24) kuanza kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani au kulipa faini ya Sh5 milioni, tayari wadau mbalimbali kupitia mitandao ya kijami ya X na Instagram wamemchangia kijana huyo Sh5.6 milioni kwa saa sita.
Chaula ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ntokela, Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya anatumikia adhabu ya miaka miwili gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kusambaza video zenye taarifa za uongo Juni 22, 2024 kwenye mtandao wa kijamii wa Tik Tok, kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandaoni.
Msanii huyo wa uchoraji, video yake ilisimbaa mtandaoni Juni 22 akiwa anachoma moto picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, suala ambalo lilikemewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na kuagiza akamatwe.
Jana Julai 4, 2024 alihukumiwa jela miaka miwili au faini ya Sh5 milioni hukumu iliyotolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, Shamla Shehagiro.
Wakati wakili wa kijana huyo Peter Kibatala, Michael Mwangasa na Michael Lugina wakiendelea na utaratibu wa kukata rufaa, Mwanaharakati Godlistern Malisa ambaye anahamisha michango ya faini kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kumsaidia kijana huyo kutoka gerezani, amesema tayari wamekusanya Sh5.6 milioni.
“Tayari tumeshapata Sh5.6 milioni kwa saa sita, faini tunalipa leo na kwa kuwa leo ni ijumaa ‘remove order’ itaombwa jumatatu,” alisema Malisa muda ambao alipigiwa na hata hivyo, baadaye mchango huo ulifikia Sh6.5 milioni.
Awali, Malisa aliandika katika kurasa zake za Instagram na X kuwa, kwa saa mbili pekee tayari walikuwa wamekusanya zaidi ya Sh2 milioni kati ya Sh5 milioni zinazohitajika kwa faini ya Chaula.
“Lengo ni Chaula atoke leo. Tunaamini kufika saa 7 (mchana), litakuwa limetimia ili faini ilipwe na Chaula atoke leo. Tunamtaka Chaula akiwa huru leo. Pigia mstari neno LEO,” ameandika Malisa kupitia mtandao wake wa Instagram.
Ameongeza, “Lakini kumbuka leo ni Ijumaa na ofisi nyingi za umma zinafungwa mapema. Hivyo, juhudi zetu ndio zitakazoamua Chaula atoke leo au aendelee kula mvua hadi Jumatatu. Tuendelee kusukuma ili kufikia lengo kwa haraka na Chaula atoke leo kabla ofisi za hazijafungwa. Do something to set.”
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Malisa amesema michango hiyo wanaratibu na James Mbowe na wameshawasiliana na baba mzazi wa Chaula, Yusuph Chaula ambaye alikiri kuwa hakutarajia mwanaye angekumbwa na adhabu kubwa kiasi kile.