Wamiliki wa mashamba ya madini wapinga kugeuka watumwa wa mali zao

Bunda. Wamiliki wa mashamba, maduara pamoja na wachimbaji wadogo katika mgodi wa dhahabu wa Kinyambwiga uliopo wilayani Bunda mkoani Mara, wameiomba Serikali kubadilisha Sheria ya Madini kwa madai kuwa sheria hiyo inawapendelea wenye leseni ya uchimbaji na kuwakandamiza wao.

Wameyasema hayo leo Julai 5, 2024 walipokuwa wakitoa kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi aliyefanya ziara mgodini hapo kufuatia uwepo wa mvutano kati yao na wamiliki wa leseni ya uchumbaji ya JB and Panters.

Kwa mujibu wa Sheria ya Madini, sura ya 123, kifungu cha 95 na 96, mwenye shamba anamiliki sehemu ya juu ya ardhi, huku mwenye leseni akimiliki madini yaliyopo chini ya ardhi katika eneo husika lakini kabla ya kuanza kuchimba madini, mwenye leseni anatakiwa kuingia mkataba na mwenye ardhi kwa ajili ya kufanya kazi pamoja au kufanya tathmini kisha kumlipa mwenye shamba fidia ili apishe katika eneo hilo na matumizi ya ardhi hiyo yanabadilika na kuwa eneo la uchimbaji madini.

Wamesema kutokana na uwepo wa sheria hiyo, mwekezaji mwenye leseni amekuwa akisikilizwa na kupewa kipaumbele zaidi kuliko wao, jambo ambalo sio sawa ikizingatiwa kuwa wao ndio wanafanya utafiti wa awali na kugundua uwepo wa madini katika maeneo hayo.

“Inafika hatua mwenye shamba haruhusiwi kuingia katika eneo lake kuangalia uchimbaji unaendeleaje, hii sio sawa kabisa, tunataka sheria imtambue mwenye shamba na kumpa haki sawa kama ilivyotoa kwa mwenye leseni,” amesema Simon Yohana.

Yohana amependekeza kuwa endapo Serikali inataka kutoa leseni ya uchimbajii wa madini katika eneo fulani, ni vema kipaumbele kikatolewa kwa mmliki wa eneo na endapo atashindwa kukata leseni ndipo wapewe nafasi watu wengine, jambo ambalo litakuwa na manufaa kwao.

Wamedai migogoro mingi inayotokea kati ya wachimbaji na wamiliki wa leseni inatokana na hali hiyo na kwamba endapo wenye mashamba ndio watakaokuwa wamiliki wa leseni za uchimbaji, ni dhahiri kuwa hakutakuwa na migogoro kama ilivyo sasa.

Wamedai kutokana na wenye mashamba wengi kutokuwa na uwezo wa kifedha kwa ajili ya  kulipia leseni na mahitaji mengine, ni vyema ikatungwa sheria itakayowapa nafuu ili wakate leseni hizo hata kwa kutumia dhamana ya maeneo yao baada ya serikali kujiridhisha na uwepo wa madini katika maeneo hayo.

“Sheria imempa nguvu mmiliki wa leseni kwani hata kama mwenye shamba atakataa kuingia mkataba naye, basi anaruhusiwa kufanya tathmini na kukulipa fidia kisha unaondolewa katika eneo hilo, wamekuwa wakitumia kipengele hiki sana kwanza wanakuletea mkataba ambao hauna faida kwako ukikataa wanakimbilia kwa mkurugenzi kufanya tathmini, hii sio sawa kabisa, wenye mashamba wanatakiwa kupewa kipaumbele,” amesema Rigita Maucho.

Mmoja wa wamiliki wa leseni katika mgodi huo, Titus Kabua amesema siyo kweli kwamba hawataki kushirikiana na wamiliki wa mashamba pamoja na wachimbaji wadogo lakini wachimbaji pamoja na wamiliki ndiyo wameamua kufanya shughuli zao bila kufuata taratibu.

“Kwa wale wenye mashamba waliokubali, mbona tunafanya nao kazi vizuri tu, hata sisi huwa hatupendi migogoro na pale tunapopata leseni ya kuchimba, tukifika eneo husika hatutaki kuwatoa wachimbaji waliopo, ila tunafanya nao kazi kwa pamoja,” amesema Kabua.

Ameiomba Serikali kuingilia kati suala la uchimbaji katika mgodi huo ambapo amedai pamoja na kumiliki leseni lakini wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na baadhi ya wamiliki wa maduara na wenye mashamba wamewazuia kufanya shughuli zao huku wakitishia kuwaua wafanyakazi wake endapo watafika kwenye maeneo ya leseni yake.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewataka wachimbaji katika mgodi huo kufanya shughuli zao kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo na kuepuka ushauri wanaopewa na watu aliowaita wanasheria wa mitaani.

Amesema ili kuhakikisha uchimbaji katika mgodi huo unakuwa na tija hasa kwa wachimbaji wadogo na wamiliki wa mashamba, ofisi yake itatoa msaada wa kisheria kwa ajili ya wao kuingia mikataba na wamiliki wa leseni huku akisema mikataba itakayoandaliwa itazingatia maslahi ya pande zote bila upendeleo wowote.

“Natoa muda wa wiki moja kuanzia sasa, anzisheni  vikundi vyenu mchague na uongozi na muweke miongozo yenu, baada ya hapo nitaleta wanasheria wawaongoze kuingia mikataba na wawekezaji hawa, Serikali inataka mfanye shughuli zenu kwa kuzingatia sheria na taratibu na kwa faida, hapa hakuna sababu ya kuwa wababe,” amesema.

Amesema Serikali inaitambua na kuthamini kazi ya uchimbaji wa madini hasa kwa wachimbaji wadogo, hivyo imedhamiria kuboresha uchimbaji huo ili uwe wa manufaa kwa wachimbaji na taifa kwa ujumla na kwamba ili kuboresha shughuli hizo, ipo mikakati iliyowekwa ikiwa ni pamoja na fursa ya mikopo kwa wachimbaji wadogo.

Related Posts