Unesco kuiunga mkono Tanzania mageuzi ya kidijitali

Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) limesema liko tayari kuiunga mkono Tanzania katika kuimarisha mabadiliko ya kidijitali.

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari na Mawasiliano wa Unesco, Tawfik Jelassi amesema hayo kupitia barua kwa Mkurugenzi wa Tume ya Tehama nchini, Dk Nkundwe Mwasaga.

Dk Nkundwe hivi karibuni alikuwa kikazi jijini Paris, Ufaransa ambako ni makao makuu ya shirika hilo.

Jelassi amesema Unesco imeguswa na kasi na utayari wa Tanzania katika mchakato wa kupambana kuyafikia mapinduzi halisi ya kidijitali.

“Ujuzi wa kidijitali ni nguzo muhimu kwa mafanikio na uendelevu wa mabadiliko. Tunayo furaha kuiunga mkono Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tume ya Tehama katika kuboresha ujuzi wa kidijitali,” amesema.

Amesema mfumo wa umahiri wa Unesco kwa umma kuhusu akili bandia (mnemba) -AI na mabadiliko ya kidijitali umeundwa kama zana hai ya maendeleo, kusaidia nchi wanachama katika mabadiliko yanayotokea.

“Kutokana na hali hiyo, tunapendekeza Tume ya Tehama ya Tanzania na Unesco kwa pamoja tuanzishe utafiti wa tathmini ya mahitaji kuhusu ujuzi wa kidijitali serikalini na umma kwa ujumla, ikifuatiwa na afua za kujenga uwezo ili kushughulikia upungufu wa umahiri uliotambuliwa,” amesema.

Mbali ya mambo ya kimsingi ya usimamizi wa data, faragha, usalama wa mtandao na AI, amesema mafunzo kwa maofisa wakuu yatazingatia umahiri zaidi wa kimkakati na muundo wa huduma ya umma unaozingatia binadamu.

Amesema anaamini Tume itachangia mabadiliko ya Tanzania kuwa kitovu cha kimataifa cha uvumbuzi.

Dk Mwasaga akizungumzia utayari wa Tanzania katika kuongeza kasi ya mageuzi ya kidijitali, amesema umewezeshwa na ushirikiano kati ya Tume ya Tehama na ofisi ya Unesco jijini Dar es Salaam chini ya uongozi wa Michel Toto, mwakilishi wa shirika hilo nchini.

Related Posts

en English sw Swahili