Mwenyekiti wa NACTE aeleza changamoto za kazazi Kuwaficha watoto wenye mahitaji maalum

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Tanzania (NACTE), Bernadetha Ndunguru, amesema bado kuna changamoto kubwa kwa wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum kushindwa kuwaleta shuleni na vyuoni kupata elimu, ambayo ni haki yao ya msingi.

Akiwa kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba leo, Julai 5, 2024, alipotembelea banda la Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Ndunguru amesema kuwa wazazi wengi wamekuwa wakiwaficha watoto wenye mahitaji maalum badala ya kuwapeleka VETA kupata mafunzo ya ufundi.

“Ni kweli kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaficha watoto wenye mahitaji maalum ndani. Wanapaswa kuacha tabia hiyo na kuwaleta VETA ili wapate mafunzo ya ufundi na kujiajiri,” amesema Ndunguru.

Ndunguru ameeleza kuwa watoto wenye mahitaji maalum wanapata stadi na ujuzi mbalimbali kupitia VETA, hivyo kuwawezesha kujitegemea. Aliongeza kuwa ametembelea mabanda mbalimbali na kushuhudia watu wenye ulemavu wakifanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kushona nguo na kutengeneza mabegi ya shule.

“Niliona watu wenye ulemavu wakifanya kazi nzuri, wakishona nguo na kutengeneza mabegi ya shule. Watu wengi wameweka oda za nguo na mabegi hayo. Mafunzo yanayotolewa na VETA yanawasaidia vijana kujiajiri,” alisema Ndunguru.

Amesisitiza kuwa VETA wanapotoa mafunzo, wanapaswa kuzingatia pia mahitaji ya watu wenye ulemavu kwani nao wana mahitaji muhimu. Ndunguru amepongeza juhudi za VETA katika kuwajumuisha watu wenye mahitaji maalum kwenye programu zao za mafunzo.

“VETA wanafanya kazi nzuri ya kuwajumuisha watu wenye mahitaji maalum. Wakipatiwa ujuzi wa kutosha, wataweza kujiajiri na kuendesha maisha yao ya kila siku,” aliongeza.

Mwenyekiti huyo ameonyesha matumaini kuwa kupitia mafunzo ya VETA, watu wenye mahitaji maalum wataweza kupata fursa za kujitegemea na kuboresha maisha yao.

Related Posts