JAJI MKUU AIPONGEZA TUME YA USULUHISHI NA UAMUZI (CMA)

• Ahidi Kuitetea Kupata Bajeti Wezeshi Kutekeleza Majukumu Yake.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Hamis Juma ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kuendelea kuboresha na kusogeza huduma zake karibu na wananchi.

Pongezi hizo amezitoa alipotembelea banda jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake katika maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es salaam leo Julai 05,2024.

Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ameitaka CMA kutoa mafunzo kwa waajiri na waajiriwa ili kuweza kupunguza idadi ya migogoro ya kikazi inayotokana na ukosefu wa elimu, ili kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji.

Vilevile ameitaka Tume kuwa na mifumo inayosomana na mahakama ili kuweza kusaidia katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama kwa kushirikiana naTume.

Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Usekelege Mpulla, amesema Tume inatarajia kuanza mataumizi ya mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao unaofahamika kama ‘Online Case Management System’ ambao utamuwezesha kila mwananchi kusajili mgogoro wake popote alipo.

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mwanasheria Mkuu wa Serikali juu ya mkakati wa kuwafikia wananchi katika ngazi ya Wilaya nchini.

Ameongeza kuwa tayari CMA imejipanga kuhakikisha huduma za Tume zinapatikana katika ngazi ya Wilaya na tayari CMA inatarajia kuanzisha Tume inayotembea itakayowezesha wananchi kupata huduma na haki kwa wakati

Related Posts