Maajabu ya mrithi wa Chama Simba

ALFAJIRI ya jana Ijumaa, Simba iliupokea ugeni mzito kutoka Afrika Kusini, wakati kocha mkuu mpya anayetarajiwa kutambulishwa, Fedluraghman ‘Fadlu’ Davids na wasaidizi wake walipotua, lakini kiungo mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Jean Charles Ahoua akikabiliwa na mtihani mzito wa Clatous Chama.

MVP huyo wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, ametua Simba akitokea klabu ya Stella akipewa mkataba wa miaka miwili na kutambulishwa kama ndiye mrithi wa Chama aliyetua Yanga baada ya kumaliza mkataba aliokuwa nao na Wekundu wa Msimbazi.

Usajili huo umekuwa gumzo kwa mashabiki wa Simba wakiamini nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 ndiye anayeenda kumaliza utata wote wa shimo aliloliacha Chama aliyeitumikia timu hiyo kwa miaka sita tangu ilipomsajili akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia na kuandika rekodi mbalimbali za kusisimua Msimbazi.

Ahoua ni MVP wa tatu mfululizo kutoka Ivory Coast kutua nchini baada ya Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua wanaokipiga Yanga, lakini akiwa ni mmoja ya nyota wapya wa kigeni waliosajiliwa na kutambulishwa na Wekundu hao hao sasa akiwamo, Joshua Mutale na Stephen Mukwala na mastaa wote tangu jana wameanza kufanyiwa vipimo vya afya kujiandaa na Jumatatu kuanza safari ya kwenda kambini katika mji wa Ismailia, Misri.

Ahoua aliyewahi kuzitumikia timu za LYS Sassandra na Sewe Sports kabla ya kukipiga Stella zote za kwao Ivory Coast anasifika kwa uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kutoa pasi zenye macho kama ilivyokuwa kwa Chama, lakini pia ni mahiri wa kufunga mabao akimudu kucheza wingi zote za kulia na kushoto.

Msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, Ahoua alimaliza kama Mchezaji Bora (MVP) wa msimu na pia klabu aliyokuwa akiichezea, huku akiifungia mabao 12 na kuasisti tisa akimfunika rekodi alizomaliza nazo Chama ndani ya Simba, kwani Mwamba wa Lusaka alifunga mabao saba na kuasisti saba tu msimu mzima.

Kama ilivyo kwa Chama, nyota huyo mpya wa Simba anatajwa kuwa mmoja na wachezaji wenye vipaji na akili kubwa ya kusukuma boli, lakini ana kasi inayoweza kumtofautisha na Mzambia aliyeenda Yanga ambaye soka lake ni la taratibu japo ana akili na kipaji akiichezesha timu atakavyo na kuwa na maamuzi ya haraka.

Ahoua anasifika pia kwa kumiliki mipira na kuwa sio rahisi kumnyang’anya anapokuwa nao na ana uwezo wa kutumia miguu yote miwili, japo wa kulia ndio una balaa zaidi kama alivyokuwa kwa Chama, lakini anafunga pia mabao ya vichwa, faida nyingine inayowafanya Wanasimba kuanza kuliimbia jina lake lake mapema.

Kama alivyokuwa kwa Chama aliyeitumikia Simba katika mechi 179 za mashindano yote akifunga mabao 42 na kuasisti 60 aliyekuwa na uwezo wa kupiga mashuti ya mbali na kupiga friikiki kiufundi, hilo lipo pia kwa Ahoua anayesifika kwa kufunga mabao ya umbali mrefu, kuchezesha timu na kutengeneza nafasi kwa wenzie.

Umri alionao na nguvu kubwa alizonazo zinampa kibarua nyota huyo mpya kazi ya kuibeba Simba mabegani mwake kama alivyofanya alipotua kikosini, kiasi alipokosekana tu, timu haikuwa na maajabu na pia aliwakata stimu mashabiki na wapenzi wa timu hiyo ilipokuwa uwanjani bila ya Mzambia huyo.

Licha ya kwamba Ahoua bado hajaonekana jinsi anavyocheza kwani ndio kwanza kasajiliwa, lakini ana kazi za kupambana kufukia mashimo yaliyoachwa na Chama ambaye katika misimu sita aliyokuwa na timu hiyo aliandika rekodi tamu ikiwamo kufunga mabao muhimu katika mechi za kuamua katika Ligi Kuu, Kombe la FA na michuano ya CAF.

Rekodi tamu za msimu wa 2022/2023 alipohusika katika mabao 18 akifunga manne na kuasisti 14 na ile ya  msimu wa 2020/2021 alipokuwa wa moto ya kuhusika na mabao 23 akifunga manane na kutoa asisti 15 ni kati ya mambo ambayo mashabiki watakuwa na hamu ya kuona Ahoua anafikia na pengine kuzipita.

Misimu ambayo namba za Chama klatika Ligi Kuu zilikuwa chini ni za 2021/2022  aliporejea akitokeaRS Berkane ya Morocco kwani alifunga mabao matatu pekee na ule wa 2019/2020 akifunga mabao mawili na kutoa pasi za mwisho 10 na msimu wa kwanza Msimbazi 2018/2019 akifunga mabao saba na kutoa asisti tisa.

Ukiachana na Ligi Kuu, Chama pia alijiwekea mizizi katika michuano ya CAF, akifanya makubwa ndani ya Simba na kuipeleka robo fainali ya michuano ya CAF mara tano.

Eneo hilo limempa umaarufu zaidi Chama kwani amewanyanyasa wapinzani huku akipachika mabao 15 na asisti sita katika mechi 44 alizoichezea Simba hatua ya makundi ya CAF tangu ametua kikosini hapo.

Ahoua hana maajabu katika michuano ya CAF lakini Simba inaweza kuwa mlango wake wa kutimiza yote hayo kama atakuwa tayari kupambania namba na kufanya vyema, kwani Simba inaanza na Kombe la Shirikisho baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga na Azam FC.

Pia ana kazi ya kuthibitisha kweli yeye ni MVP, kwani Chama alishawahi kuletewa nyota Msimbazi waliotajwa kama warithi wake alipoenda Morocco akiwamo Rally Bwalya na Pape Sakho lakini kila mmoja alionyesha ubora ila hakuna aliyefika kiwango cha ufalme wa Chama na kuondoka wakimuacha akiendelea kuimbwa.

Kocha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema Chama ni mmoja tu na pengo lake haliwezi kuzibika, lakini lazima aisha yaendelee kwani sio wa kwanza kuondoka Simba.

“Simba inasajili mchezaji sio kwaajili ya kuwa kama aliyeondoka. Ilishawahi kuwa na wachezaji bora wakaondoka lakini wakaja wengine na kufanya vizuri. Walikuwepo kina Abdallah Kibadeni, Athuman Idd  Machuppa, Yusuf Macho, Emmanuel Okwi wakaondoka na timu ikasajili wengine.

Nadhani jambo la msingi ni wachezaji waliosajiliwa akiwemo huyo Ahoua kutimiza vyema majukumu yao uwanjani na baadae nao wanaweza kujitengenezea ufalme wao kama kina Chama walivyofanya,” alisema Mwaisabula, huku kiungo wa zamani wa Simba, Abdulswamad Kassim aliongeza kwa kusema kwa muda aliokaa na Chama kikosini hapo haoni kama kuna mchezaji anaweza kuziba pengo hilo lakini akapendekeza kuaminiwa kwa walioopo nao wataisaidia Simba.

“Sijamuona Ahoua akicheza, lakini nimemuona Chama na nimecheza naye. Hakuna mtu wa kumfananisha naye. Anajua sana pia Ana vitu vyakipekee ambavyo viungo wengi hawana. Lakini sio tatizo kwani kuna mechi nyingi tu Simba imecheza bila Chama na imeshinda hivyo naamini waliopo wakipewa muda na kuaminiwa wanaweza kufanya vizuri. Kikubwa ni timu kufika malengo na sio kumtegemea mchezaji mmoja tu,” alisema Abdul ambaye kwa sasa ni mchezaji huru.

Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema Chama ni mchezaji mzuri na amefanya makubwa ndani ya Simba, lakini ameondoka na timu hiyo inajipanga kucheza bila yeye.

“Chama ni mchezaji mzuri na mpira ndio kazi yake. Alifanya makubwa akiwa Simba, sasa ameondoka hivyo kwa sasa tunapanga mambo yetu kama Simba bila kumtegemea Chama. Hakuna mchezaji anayecheza milele kwenye timu hivyo kuondoka kwa Chama watakuja wengine na naamini watafanya vizuri,” alisema Mgunda.

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Amri Kiemba alisema mashabiki wa Simba hawapaswi kuishi na presha na matarajio makubwa kwa wachezaji wapya kwani ni msimu ambao timu hiyo imeamua kuanza upya hivyo wachezaji wanahitaji muda kuingia kwenye mifumo na kuelewana vyema.

“Matarajio hayapaswi kuwa makubwa sana kwenye msimu huu ambao timu imeanza kujitengeneza upya. Wasiwape presha sana wachezaji na kuwalinganisha na walioondoka kikubwa wajiandae kisaikolojia na wawape muda hata huyo Ahoua,” alisema Kiemba.

Beki na kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema haifai kulinganisha wachezaji kwani kila mmoja anasifa na ubora wake uwanjani kutokana na anavyotumiwa.

“Wachezaji wanacheza kwenye timu na kuondoka. Mfano Chama alikuwa mchezaji mzuri, lakini ameondoka Simba hivyo haina haja ya kumlinganisha na anayeingia (Ahoua). Kila mtu ana vitu vyake, ubora na udhaifu hivyo hakuna haja ya kuwalinganisha, tusubiri tuone kwani soka ni mchezo wa wazi,” alisema Julio.

Related Posts