Unguja. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imefichua jinsi baadhi ya taasisi za umma zinavyokosa usimamizi mzuri wa udhibiti wa ndani kwa kutoanzisha vitengo hivyo kushindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, akishauri vipatiwe mafunzo.
Hayo yamo kwenye taarifa ya CAG katika kitabu cha ukaguzi wa taarifa za fedha za Tawala za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kilichowasilishwa katika Baraza la Wawakilishi Juni 27, 2024.
Pia dosari za kiutendaji zinakwaza kamati za ukaguzi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria jambo linalosababisha kamati hizo na kitengo cha ukaguzi wa ndani kutopitia ripoti za CAG, hesabu za mwisho wa mwaka na kushindwa kutoa maoni ya dosari na kasoro zilizobainishwa na CAG.
Katika ripoti hiyo yenye kurasa 171. CAG, Dk Othman Abbas Ali amesema vitengo vya ukaguzi vya ndani vinaonekana kutokuwa na uwezo, hivyo ameshauri kamati na vitengo hivyo kupatiwa mafunzo ya namna bora ya kutekeleza kazi zake.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, miongoni mwa taasisi zilizobainika kuwa na dosari hizo ni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Baraza la Manispaa Chake Chake Pemba, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi na Kikosi cha Valantia (KVZ).
Ukaguzi umebaini dosari katika usimamizi wa mikataba kwa baadhi ya taasisi za umma, ikiwamo kukiukwa vipengele muhimu vilivyoainishwa kwenye mikataba hiyo hali iliyosababisha kutofikiwa kwa malengo yaliyopangwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ripoti imebainisha kuwapo ukiukwaji wa vipengele hivyo, umesababisha baadhi ya miradi kutokamilika na kufikiwa malengo yaliyokusudiwa.
Dk Abbas amesema pia zipo baadhi ya taasisi zimetekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia rasimu za mkataba jambo linalosababisha kuitia hasara Serikali kwa kufanya malipo ya ziada kutokana na kutozingatia masharti ya jumla ya mikataba au kushindwa kutoza tozo ya fidia, kulikosababishwa na baadhi ya wazabuni kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati.
“Kutowasilishwa kwa hati ya dhamana pamoja na baadhi ya taasisi kushindwa kutekeleza ushauri wa kitaalamu ulitolewa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu uliowataka kufanya marekebisho ya rasimu za mikataba kabla ya utekelezaji,” amesema.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 mamlaka tisa kati ya 12 za Aerikali za mitaa zilikusanya Sh11.5 bilioni kutoka vyanzo vyake vya ndani ikilinganishwa na bajeti ya Sh15.5 bilioni sawa na upungufu wa mapato kwa Sh3.9 bilioni.
Amesema ukaguzi ulibaini mamlaka moja haikupangiwa bajeti ya makusanyo yatokanayo na vyanzo vya ndani, hivyo kuishauri Ofisi ya Rais Fedha na Mipango kuhakikisha wanalitazama jambo hilo kwa kina ili kuwa na bajeti ya makusanyo kwa taasisi hiyo, ili iweze kutoa huduma kwa jamii na kujiendesha yenyewe kwa mujibu wa dhana ya kulianzisha Jiji la Zanzibar.
Licha ya kuimarika kwa usimamizi wa fedha kwa baadhi ya taasisi, ukaguzi umebaini kuwapo zenye upungufu katika nidhamu ya fedha na kusababisha kutozingatiwa kwa matakwa ya sheria namba 12 ya usimamizi wa fedha za umma ya mwaka 2016.
Miongoni mwa dosari kubwa zilizobainika ni kufanyika malipo kwa fedha tasilimu, dosari katika uzuiaji wa kodi, mapato ya Serikali kutowasilishwa benki kwa wakati na kutozingatiwa maelekezo ya Serikali kuhusu kudai stakabadhi za kielektroniki wakati wa ufanyaji wa malipo.
Ununuzi usio na ushindani
Ripoti imefichua uwapo wa taasisi za umma zinazofanya manunuzi bila kuzingatia ushindani wa bei, kuzingatia rasimu za mikataba ikiwamo yenye rasimu zilizowasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Dosari nyingine ni kutokuambatanishwa nyaraka muhimu za manunuzi katika hati za malipo, kufanya manunuzi kinyume cha mpango wa manunuzi hivyo kusababisha baadhi ya taasisi kufanya hivyo nje ya mpango au manunuzi yenye gharama kubwa kuliko uhalisia wa bajeti iliyowekwa kwenye mpango.
Kwa mwaka wa fedha 2022/23 hati 22 za ukaguzi zilitolewa katika ripoti hiyo kati ya hati hizo, 19 ni hati zinazoridhisha sawa na asilimia 86.36, hakukuwa na hati mbaya wala hati ya kushindwa kutoa maoni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tathimini ya mapendekezo kwa mwaka uliopita inaonyesha kati ya mapendekezo 512 kwenye mamlaka ya Serikali za mitaa, 380 sawa na asilimia 74. 22 yametekelezwa, 44 sawa na asilimia 8.59 yapo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mapendekezo 47 sawa na asilimia 9.18 hayajatekelezwa, 23 sawa na asilimia 4.49 yamejirudia, huku 18 sawa na asilimia 3.52 yamepitwa na wakati.
Licha ya sheria kutaka chombo cha moto cha umma kuwa na bima lakini ukaguzi umebaini taasisi 15 za umma kutokatia vyombo vya moto bima yakiwamo magari, pikipiki na vespa.
Amesema kutofanya hivyo kunaweza kusababisha hasara kwa Serikali kwa kutumia fedha kwa ajili ya matengenezo pindi vinapoharibika, hivyo kushauriwa kuweka kipaumbele kutekeleza suala hilo.
Uwepo wa mifumo duni umetajwa kuchagia baadhi ya taasisi kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji mapato, ambapo 12 zimebainika kuwa na dosari hiyo kuchangia kushindwa kutimiza malengo yaliyopangwa.
Pia taasisi hizo zinatajwa kukosa ubunifu wa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato, huku zikishindwa kutilia mkazo ukusanyaji mapato ambazo ni pamoja na ofisi za wakuu wa mikoa ya Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja na Kusini Unguja.
Nyingine ni Baraza la Manispaa ya Mjini, Baraza la Mji Wete, Chake Chake, Baraza la Mji Mkoani, Baraza la Mji Wilaya ya Kati, Halmashauri ya Wilaya Micheweni na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi.
Mohamed Haji, mtaalamu wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) ameshauri ufike wakati ripoti ya CAG ipewe mkazo na kuchukuliwa hatua kwa wanaobainika kufanya makosa.
Zainab Mbarouk, mwanaharakati huru amesema bado Serikali ina kazi kubwa ya kujenga mifumo ndani ya taasisi ili kuleta ufanisi, vinginevyo wataendelea kuimba nyimbo zilezile kila mara.
Tofauti na hao, Shekha Suleiman Ali mtaalamu wa ugavi anaona kuna uimara kwani baadhi ya ripoti zimeonyesha kuwapo kwa ufanisi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
“Binafsi naona ipo haja CAG apewe meno ya kuchukua hatua badala ya kuishia kwenye ukaguzi tu, watendaji bado wanaona hakuna mkazo kwa sababu hata akikuta madudu kiasi gani hana hatua anayochukua badala yake anabaki kutoa mapendekezo ambayo yanaweza kufanyiwa kazi au yakaachwa,” amesema.