Morogoro. Watu watatu wanashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama, kwa tuhuma za wizi na uharibifu wa miundombinu katika reli ya kisasa (SGR), kipande cha Morogoro – Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amethibitisha kukamatwa kwa watu hao na kuwaonya wananchi wenye mawazo ya kuhujumu miundombinu kuacha mara moja.
Akizungumza na Mwananchi Digital Julai 6, 2024, mara baada ya kukagua reli hiyo kutoka Morogoro hadi Kilosa, Malima a amesikitishwa na tukio hilo kwani Serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya mradi huo wa kimkakati na wenye tija kwa Taifa.
“Wamekamatwa watu watatu ambao wanadaiwa kujihusisha na wizi wa nyaya za shaba, ambazo zimetumika kwenye ujenzi wa miundombinu ya njia ya treni kwa kipande cha Morogoro – Kilosa na vyombo vyetu vinaendelea na uchunguzi ili utaratibu ukikamilika wafikishwe mahakamani,” amesema Malima.
Amesema uwepo wa reli hiyo una maslahi kwa wananchi wote bila kubagua dini kabila wala itikadi kwa Watanzania wote, lakini inasikitisha kuona wachache wanapanga kwenda kukata nyaya na kuchukua shaba, kitendo anachokiita ni fikra choyo.
‘’Mkoa wa Morogoro sio sehemu ya kufanyia masihara, watafute sehemu nyingine ya kufanya hujuma hizo. Kama Serikali haitakubali kuona wachache wanaharibu miundombinu ya mradi huo kwa kuwa mkoa huo ni mnufaika mkubwa,’’amesema.