Benki Kuu kununua tani sita za dhahabu

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kwa mwaka huu wa fedha (2024/2025) inatarajia kununua tani sita za dhahabu,  ili kutunisha akiba ya madini hayo yanayoweza kutumika kama fedha kufanya ununuzi mbalimbali.

Hayo yameelezwa Alhamisi wiki hii na Naibu Gavana wa BoT anayeshughulikia uchumi na sera za kifedha, Dk Yamungu Kayandabila katika mkutano na waandishi wa habari kutangaza kiwango kipya cha riba ya Benki Kuu (CBR) kwa kipindi cha robo ya mwaka utakaoishia Septemba 2024.

Dk Kayandabila amesema tangu BoT ianze utaratibu wa kununua dhahabu mpaka sasa imenunua kilo 418, lakini imedhamiria kutunisha akiba ya madini hayo kama ambavyo Serikali imedhamiria.

“Kama mnafuatilia benki kuu nyingi duniani hivi sasa zinanunua dhahabu na sisi tumejaaliwa kuwa na madini hayo nchini si sawa tukakosa hata tani moja. Malengo ya awali ilikuwa kununua tani 12 lakini tukasema twende taratibu na mwaka huu tutanunua kilo 6,000,” amesema Dk Kayandabila.

Kuhusu thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni, Dk Kayandabila amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita,  thamani ya shilingi imepungua kwa asilimia 10 hadi 11 lakini haikuathiri mfumuko wa bei kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine zenye uchumi sawa.

“Mara nyingi thamani ya sarafu huathiri mfumuko wa bei lakini sisi pamoja na mtikisiko kwenye sarafu yetu,  mfumuko wa bei uliendelea kuwa mzuri ikilinganishwa na nchi nyingine, wakupongezwa hapa ni wananchi kwa kuwa na uzalishaji mkubwa wa chakula,” amesema.

Dk Kayandabila amesema kutokana na changamoto ya upatikanaji wa Dola kuna mwenendo mkubwa,  wafanyabiashara wameanza kutumia Euro kama mbadala wa sarafu ya kufanya ununuzi wa kimataifa.

Awali, akisoma taarifa ya Kamati ya Fedha kwa niaba ya Gavana wa BoT, Dk Kayandabila amesema tathimini ya jumla ya mwenendo wa uchumi wa nchi ni mzuri na makadirio ya ukuaji kwa mwaka 2024, unatarajiwa kuwa asilimia tano na 5.4 katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024.

“Mwenendo wa uchumi wa Zanzibar nao umeendelea kuwa imara, ulikua kwa asilimia 7.4 mwaka 2023. Mwenendo huu mzuri wa ukuaji wa uchumi nchini unatarajiwa kuendelea vyema katika kipindi cha nusu ya pili ya mwaka 2024 na mwaka 2025,” amesema.

Kutokana na mwenendo mzuri, Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania imeamua CBR itaendelea kuwa asilimia sita kwa robo mwaka utakaoishia Septemba 2024.

“Maamuzi ya kamati pia yanazingatia mtazamo chanya wa uchumi wa dunia, matarajio ni kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei katika nchi nyingi, kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia,” imeeleza taarifa ya kamati hiyo.

Kamati inatarajia uchumi wa ndani kuendelea kukua kwa kasi, sanjari na upatikanaji wa chakula cha kutosha, na kupungua kwa kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi kutokana na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni kunakochangiwa na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na chakula.

Related Posts