KLABU ya Simba imekamilisha usajili wa kiungo mkabaji, Augustine Okajepha, 20, akitokea Rivers United ya Nigeria.
Kiungo huyo raia wa Nigeria, anajiunga na Simba kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa kwenda kuongeza nguvu katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Taarifa iliyotolewa na Klabu ya Simba imebainisha kumsajili kiungo kwa mkataba wa miaka mitatu.
“Ni rasmi tumekamilisha usajili wa kiungo mkabaji raia wa Nigeria kutoka Rivers kwa mkataba wa miaka mitatu. Okajepha ni mchezaji kijana mwenye miaka 20 aliyetunukiwa kipaji kikubwa katika idara ya kiungo wa ulinzi.
“Katika miaka kadhaa sasa tumekuwa tukihitaji kupata mchezaji ambaye ataipa uimara safu yetu ya ulinzi na Okajepha anatarajia kuwa suluhisho.
“Okajepha ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu ya nchini Nigeria (MVP) kwa msimu 2023/2024,” ilisema taarifa hiyo.
Ujio wa Okajepha unalifanya eneo la kiungo cha ukabaji ndani ya Simba msimu ujao atakuwepo yeye, Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute na Yusuph Kagoma ambaye taarifa zilizopo ni kwamba muda wowote atatambulishwa kikosini hapo.
Huo unakuwa ni usajili wa sita kutambulishwa ndani ya Simba kuelekea msimu ujao baada ya Valentino Mashaka, Abdulrazack Mohamed Hamza, Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala na Joshua Mutale.
Pia Simba imetangaza kuwaongezea mikataba Kibu Denis, Israel Mwenda na Mzamiru Yassin huku ikiachana na Kennedy Juma, Shaban Chilunda, Luis Miquissone, Saido Ntibazonkiza, John Bocco na Henock Inonga aliyeuzwa kwenda FAR Rabat ya Morocco.
Clatous Chama naye ameondoka Simba baada ya mkataba wake kumalizika akiitumikia timu hiyo kwa takribani misimu sita na sasa ametua Yanga.