Ajali ya lori ilivyowanasa wahamiaji haramu Arusha

Arusha. Ikiwa ni mwendelezo wa ukamataji wa wahamiaji haramu wanaoingia nchi, Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Arusha limewakamata wahamiaji haramu 28 kutoka Ethiopia walioingia nchini kwa njia za panya.

Wahamiaji hao wamekamatwa usiku wa kuamkia Julai 5, 2024 baada ya lori la mzigo walilokuwa wamepakiwa kupata ajali baada ya kugongana na lori jingine, hivyo wakalazimika kushuka na kujificha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 6, 2024 na Naibu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Dickson Mwandikile, watuhumiwa hao walikamatwa maeneo ya Uwanja wa Ndege Kisongo uliopo nje ya mji wa Arusha.

Amesema kwa mujibu wa maelezo yao, walikuwa wamepakiwa kwenye lori la mizigo ambalo lilipata ajali baada ya kugongana na lori jingine, ndipo waliposhuka na kujificha maeneo hayo.

Ofisa huyo amesema raia hao waliingia nchini kutokea nchi jirani ya Kenya kwa lengo la kwenda Afrika Kusini.

“Baada ya kupekuliwa, baadhi ya raia hao walikutwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao ikiwemo kichwani yaliyosababishwa na ajali hiyo,” amesema.

Amesema jeshi hilo linaendelea kutafuta gari lililotumika kuwasafirisha raia hao pamoja na wasafirishaji na amebainisha kuwa wote wamekamatwa wakiwa hawana hati za kusafiria.

Naibu ofisa huyo amesema taratibu za kisheria zinaendelea ili kuwafikisha mahakamani wahamiaji hao.

“Tunatoa wito kwa wananchi kutojihusisha kwa namna yoyote na usafirishaji haramu wa binadamu na mtakapobaini wapo raia wa kigeni wanaosafirishwa kimagendo, toeni taarifa kwenye vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria,” ameongeza.

Tukio hilo siyo la kwanza kutokea nchini, siku za hivi karibuni, wahamiaji haramu wamekuwa wakikamatwa wakisafirishwa kutoka Kaskazini mwa Tanzania kwenda kusini ambapo inaelezwa wanasafirishwa kuelekea Afrika Kusini.

Hivi karibuni, Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na Mahakama ya Wilaya ya Moshi iliamuru kutaifishwa magari mawili yaliyokamatwa yakiwasafirisha wahamiaji haramu 12 raia wa Ethiopia, likiwamo linalodaiwa kumilikiwa na mbunge mmoja.

Magari yaliyotaifishwa kwa amri ya mahakama hiyo ni Toyota Land Cruiser lenye namba za usajiri T888 BTY ambalo jina la mmiliki linalosomeka kwenye nyaraka za umiliki, linafanana na la mbunge mmoja hapa  nchini.

Gari lingine lililotaifishwa ni lori aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili KCV 571Y la nchi jirani,  ambalo lilikamatwa katika mji wa Tarakea wilayani Rombo, Juni 19, 2024 likiwa na wahamiaji haramu watano.

Related Posts