Serikali yatoa onyo kwa makandarasi

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewataka makandarasi wanaopewa dhamana ya kujenga miradi ya maendeleo Zanzibar kuheshimu mikataba ya makubaliano wanayoingia kati yao na Serikali, vinginevyo hawatasita kuwachukulia hatua.

Hemed ametoa kauli hiyo Julai 6, 2024 alipofanya ziara kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ukiwa ni mwendelezo wa ziara za kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.

Amesema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wakandarasi kuchelewesha kumaliza miradi kwa wakati wakiomba kuongezewa muda jambo ambalo linakwamisha lengo la Serikali ya kutatua kero za wananchi kwa wakati.

Ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu atishie kumtimua mkadarasi wa kampuni ya ujenzi ya Fuchs inayojenga Sekondari ya Makunduchi kutokana na kuchelewa kukamilisha ujenzi wa shule hiyo licha ya kuongezewa muda mara mbili. 

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea kuheshimu mikataba inayoingia na kampuni na kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa kampuni zinazojenga miradi ya maendeleo nchini ili kuharakisha ukamilishaji wa miradi hiyo kwa utaratibu uliopangwa na viwango vyenye ubora,” amesema Hemed.

Amesema kumalizika kwa wakati kwa ujenzi wa jengo hilo kutatoa fursa kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufanya kazi katika mazingira mazuri na salama kulingana na umuhimu wa ofisi hiyo.

Mkataba wa ujenzi wa ofisi hiyo ulianza Januari mwaka huu na unatakiwa kukamilika Oktoba, 2024.

Hata hivyo, Hemed ameonyesha wasiwasi wa kukamilika kwa wakati ujenzi huo.

Mbali na hayo, kiongozi huyo amesema kuanzia sasa Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) wanapaswa kuwachukulia hatua stahiki kampuni ambayo haitakabidhi miradi kwa wakati ili iwe fundisho kwa nyingine zinazoendelea na ujenzi wa miradi.

Amewataka wakala wa majengo kuacha muhali kwa kampuni yoyote itakayokwenda kinyume cha mkataba wa ujenzi wa miradi ya Serikali ambayo imefungwa baina ya Serikali na kampuni husika.

Mkandarasi kutoka kampuni ya China Railway Jianhuwang Engineering (CRJE), Chey Yur amesema licha ya kukabiliwa na changamoto mwanzoni mwa ujenzi, watahakikisha wanakamilisha na kukabidhi jengo hilo ndani ya muda waliokubaliana.

Yur amesema wameshaongeza nguvu kazi katika ujenzi huo na wanatarajia kuanza kufanya kazi usiku na mchana ili kuongeza kasi ya ujenzi na kukamilisha kwa wakati.

Msimamizi wa majengo kutoka ZBA, Mohamed Nahoda Mohamed amesema wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na mkandarasi wa ujenzi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 20, wakitarajia kukamilisha mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.

Ujenzi wa jengo la ZEC la ghorofa nne ukikamilika utagharimu Sh11 bilioni.

Related Posts