MTU WA MPIRA: Hivi mapro wa kigeni wamewakosea nini?

NIMEONA sehemu mjadala kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni nchini. Kuna watu bado wanaamini kuwa idadi ya wachezaji 12 wa kigeni katika ligi yetu ni kubwa. Inashangaza sana.

Hoja ya hawa wasioamini wanataka idadi ya wachezaji wa kigeni ipunguzwe. Wanadai wingi wa wageni unaziba nafasi za wachezaji wazawa. Inachekesha kidogo.

Kuna vitu vinafikirisha kuhusu mjadala huu wa wachezaji wa kigeni. Umeanzishwa na nani? Kwa sababu gani? Kuna msukumo gani nyuma yake? Ni maswali magumu.

Kweli hii ni nchi huru na kila mtu anaweza kutoa maoni yake, lakini siyo kwenye kila kitu. Sijaona sababu ya hili suala kuwa mjadala kwa sasa. Kwanini? Nitakwambia.

Kwanza hoja ya kuwa wageni wanaziba nafasi za wachezaji wazawa naona ni dhaifu. Ni mawazo mgando katika dunia ya ushindani.

Tutazame kwa undani. Ni wachezaji gani wazawa wamezibiwa nafasi zao na wachezaji wa kigeni? Pale Yanga kuna mabeki wanne wazawa. Wote wanacheza. Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto wanacheza mbele ya Gift Fred. Wanacheza vizuri.

Fred ni raia wa Uganda. Alisajiliwa kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi, lakini amejikuta benchi mbele ya kina Job na wenzake. Kwanini? Kwa sababu wazawa wamekubali kushindana. Wanacheza vizuri na kocha anawapa nafasi.

Kule pembeni kuna Nickson Kibabage. Anacheza mbele ya Joyce Lomalisa. Kwanini? Kwa sababu Kibabage ni mshindani. Lomalisa alikuwa staa kabla yake pale Yanga, ila Kibabage amekuja na kuonyesha kitu cha tofauti. Kocha Miguel Gamondi anampa nafasi.

Kwenye ushambuliaji kuna kina Kennedy Musonda na Joseph Guede, lakini bado Clement Mzize huwa anacheza. Amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha kocha Gamondi. Kwanini? Kwa sababu Mzize anapambana.

Pale Simba walikuwepo kina Luis Miquissone, Essomba Onana na wengineo lakini bado kina Ladack Chasambi na Edwin Balua wanacheza. Kibu Denis anacheza kila siku. Kwanini? Kwa sababu wanashindana. Ndio dunia ya ushindani ilivyo. Hata kule Azam kulikuwa na Cheikh Sidibe nyota wa timu ya taifa ya Senegal, lakini alikuwa akikalishwa benchi na Pascal Msindo na hata Edward Manyama. Kuna Yahya Zayd na Adolph  Mtesigwa wamekuwa wakiwakalisha benchini baadhi ya mapro wa kigeni wa kikosi hicho. Feisal Salum ‘Fei Toto’ amecheza mechi karibu zote eneo la ushambuliaji akiwaacha wageni nje na kufikia hatua ya kuchuana na Stephane Aziz KI katika mbio za Mfungaji Bora wa msimu. Ni miaka mingi imepita Azam kuwa na nyota mzawa mkali wa kuibeba timu tangu alipoondoka John Bocco kwenda Simba msimu wa 2017-2018.

Nimetoa mifano michache lakini wapo wachezaji wengi wazawa wanacheza mbele ya wageni. Mzamiru Yassin anacheza kila siku pale Simba na kina Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na Babacar Sarr wapo. Kwanini anacheza?

Hivyo unaweza kuona kama hoja ya kuziba nafasi za wazawa haina mashiko. Wachezaji wazuri lazima wajue kushindana na wachezaji bora.

Hoja ya pili ilikuwa ni kuruhusu wazawa wengi wacheze ili kuwa na timu ya taifa imara. Hii ndio inashangaza zaidi. Ni kweli tutakuwa na timu imara zaidi ya taifa kwa kupunguza wageni ili wazawa wengi wacheze? Hapana. Ni hoja dhaifu pia.

Kwanza, naamini timu ya taifa itakuwa imara zaidi kama tutapata wachezaji wengi wenye ushindani. Ndiyo sababu wakati wachezaji wa kigeni wakiwa watatu, kisha watano na baadaye saba bado timu ya taifa ilikuwa haifanyi vizuri. Tulibahatika tu kufuzu Chan mara moja 2009. Mara nyingine zote tuliangukia pua.

Ila kanuni iliporuhusu wachezaji 10 wa kigeni, tulifuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2019 kwa mara ya kwanza baada ya miaka 40. Wakati wachezaji wa kigeni wakiwa 12 tumerudi tena Afcon, 2023 na tukafanya vizuri zaidi ya miaka yote tuliyoshiriki. Tukapata sare mbili kwa mara ya kwanza.

Kwanini? Kwa sababu wachezaji wetu wamejua kushindana. Wamekomaa. Ushindani unaanzia ndani hadi nje. Halafu timu zenye wachezaji wa kigeni wanaofikia 12 hazizidi tano katika Ligi Kuu ya klabu 16, wale wachezaji wengine wazawa waliopo katika timu nyingine mbona hawazibebi timu zao na kuitwa Taifa Stars?

Pili, timu ya taifa itakuwa imara zaidi kama wachezaji wetu watakwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwa wingi zaidi. Kama tunataka wachezaji wetu wakacheze nje, kwanini tuanze kubana wageni hapa kwetu? Haiingii akilini.

Leo hii tunajivunia hawa kina Mbwana Samatta, Himid Mao, Saimon Msuva na wengineo kucheza soka la kulipwa nje. Ndivyo ambavyo Mali wanajivunia Djigui Diarra kuwepo hapa. Ndivyo ambavyo Burkina Faso inajivunia Stephane Aziz Ki kuwa hapa.

Tatu, uwepo wa wachezaji hawa 12 wa kigeni umezifanya klabu  zetu kufanya vizuri katika mashindano ya CAF. Imekuwa kawaida kwa timu za Tanzania kufika robo fainali kwenye mashindano ya CAF. Iligua jambo gumu sana kipindi cha nyuma lakini sasa imekua kawaida.

Hii imesaidia hadi Tanzania kupata nafasi nne za uwakilishi wa klabu kule CAF. Ni nchi 12 tu  Afrika zina nafasi nne. Inafurahisha sana. Halafu anakuja mtu huko sijui katokea wapi anasema wachezaji wa kigeni wapunguzwe. Hoja dhaifu sana.

Related Posts