WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewaita wadhamini mbalimbali kudhamini mashindano ya kwenye mchezo wa gofu ambao umeanza kukua kwa kasi hapa nchini.
Nnauye ameyasema hayo kwenye mashindano ya Vodacom Golf Tour yanayoendelea kwenye viwanja vya Lugalo Golf Club jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo alisema kwa sasa mchezo wa gofu umeanza kujipatia umaarufu hapa nchini akiwataka wadhamini kujitokeza kwa wingi kutokana na kufanyika ajira kwa wengi.
“Nimekuja kuzindua mashindano haya, nimesikia kuna muitikio mkubwa wa watu wapo zaidi ya washiriki 100 na kwa mara ya kwanza imetupa washiriki wengi sana,” alisema Nnauye na kuongeza.
“Niwashukuru wadhamini wa mashindano haya, gofu imeanza kujipatia umaarufu hapa nchini lakini duniani ni mchezo maarufu kwa sababu unachezwa na rika zote kuanzia watoto na watu wazima.
“Japokuwa mashindano haya yalianza jana, nimekuja kuyazindua leo halafu kesho tunamalizia na kutoa zawadi, wito wangu kwa wadhamini ni kujitokeza kudhamini zaidi kwenye gofu hasa vijana ili waendelee kufaidika na mchezo huu ama vipaji vyao.”