Mapya yaibuka barabara iliyokuwa na nguzo katikati

Mwanza. Ni barabara yenye urefu wa kilomita 1.3 iliyoanza kujengwa kwa mawe Novemba, 2023 na kukamilika Aprili, 2024.

Barabara ya Mchungwani iliyopo Mtaa wa Kiloleli ‘B’ wilayani Ilemela, jijini Mwanza, hivi karibuni ilikuwa gumzo mitandaoni kutokana na nguzo za umeme kuwa katikati ya barabara hivyo magari kupita kwa tabu.

Hilo likipatiwa ufumbuzi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililoziondoa nguzo hizo, mapya yameibuliwa kuhusu ubora wa barabara hiyo, ikielezwa mawe yanayoruka yanahatarisha usalama.

Ikiwa ni miezi takribani miwili tangu ujenzi kukamilika ukigharimu zaidi ya Sh400 milioni, mawe yaliyotumika kwa ujenzi yameanza kung’oka.

Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilieleza nguzo hizo zilibaki katikati ya barabara pasipo kuondolewa licha ya Serikali ya mtaa kuitaka Tanesco kuziondoa bila mafanikio.

Hata hivyo, Julai 4, 2024 Tanesco ilitoa taarifa kwa umma ikieleza nguzo ziliondolewa Mei 13 na  kabla ya ujenzi wa barabara zilikuwa sehemu sahihi.

“Kabla ya kujengwa barabara ya mtaa, nguzo ile ilikuwa sehemu sahihi lakini wakati wa ujenzi barabara ilipita ilipokuwa na taarifa kwa ajili ya kuiondoa zilikuja kwa kuchelewa  lakini baadaye tuliiondoa,” ilisema taarifa ya Tanesco.

Wakizungumza na Mwananchi Julai 5,2024  baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamesema nguzo hizo zilikuwa zikisababisha ajali na msongamano wa vyombo vya moto, yakiwamo magari, bajaji na pikipiki.

“Kuna siku kijana mmoja aligongwa akaangukia kwenye mtaro,” amesema Lucia Kiswela, mkazi wa Kiloleli ‘B’

Mwenyekiti wa mtaa huo, Lucas Ndege amesema baada ya ujenzi kukamilika nguzo zikiwa katikati, ofisi yake iliwasiliana na Tanesco ili kuziondoa kwa kuwa madhara yalianza kuonekana baada ya magari kugusa nyaya cheche zilitokea.

Amesema ofisi yake haijui iwapo mkandarasi alikuwa akiwasiliana na shirika hilo.

“Nilishangazwa wakati barabara inajengwa mkandarasi alikuwa anazungusha mawe kwenye nguzo anasonga mbele, zikaachwa zikiwa katikati ya barabara.”

“Nilifuatilia kuwauliza kwa nini wanaacha nguzo katikati ya barabara, huku zikiwa zimezungushiwa mawe je, ikileta madhara zaidi? Hawakunipa jibu sahihi mpaka walipokuja kumaliza kujenga barabara ndipo tukaanza kupiga kelele mpaka Tanesco walipokuja kuziondoa,” amesema.

Kiwango ujenzi wa barabara

Ndege amesema changamoto iliyopo hivi sasa ni mawe yaliyojengewa barabara kuchomoka na kuruka akihofia huenda kiwango cha ubora wa ujenzi hakikuzingatiwa.

“Kwa kuwa bado hatujakabidhiwa barabara hii sina la kuongeza zaidi ya kushukuru Serikali Kuu maana ndiyo imetoa fedha za ujenzi, awali mtaa ulikuwa vibaya sana,” amesema.

Mkazi wa mtaa huo, Mussa Sakambule amesema baada ya nguzo kutolewa watembea kwa miguu na vyombo vya moto wanapita bila shida, lakini tatizo ni mawe kuchomoka.

“Ujenzi umefanywa na Tarura (Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini), mpaka sasa bado barabara hii hatujakabidhiwa lakini imechoka, ukiangalia mawe yanang’oka pia ubora wake upo chini ilihali haijatimiza hata mwaka mmoja,” amesema mkazi wa mtaa huo, Mohamed Kihinga.

Akizungumzia kuhusu nguzo kuwa katikati ya barabara, Meneja wa Tarura Wilaya ya Ilemela, Makonyo Sobe amesema mawasiliano na Tanesco yalifanyika ujenzi ukiendelea.

“Siyo kwamba aliacha… wakati barabara inajengwa tulikuwa tunafanya mawasiliano, sasa wakati taratibu za kifedha zikiendelea kuwalipa Tanesco ili kuja kuhamisha mkandarasi akawa anaendelea na majukumu ya kujenga barabara hiyo,” amesema Sobe.

Amesema,  “mawasiliano yalikuwapo lakini tukaona tusikwamishe ndiyo maana mkandarasi akaendelea na kipande cha mbele wakati taratibu zikiendelea na Tanesco pia nao waliweza kupokea vizuri na kushughulikia tatizo hilo, nadhani hicho kipande cha video kilichukuliwa kipindi hicho cha nyuma.”

Kuhusu ubora wa barabara hiyo, Sobe amesema bado ipo kwenye matazamio ikiangaliwa kwa miezi sita kabla ya kukabidhiwa, hivyo kama kuna tatizo au matengenezo yoyote yatafanywa na mkandarasi.

“Hakuna sehemu yoyote iliyochomoka mawe zaidi ya hilo eneo lililokuwa na nguzo,” amesema.

Related Posts