TIMU 19 za soka zitachuana kuwania ubingwa wa Kombe la TBA katika fainali zitakazofika kilele, Julai 19 katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.
Mikikimikiki ilianza Julai Mosi kwenye viwanja hivyo vya Gymkhana, huku lengo kubwa likiwa kuboresha afya kwa timu shiriki ambazo zinamilikiwa na taasisi za mabenki hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki nchini (TBA), ambao ni waandaaji wa mashindano hayo, Tuse Joune amesema hii ni mara pili kwa mashindano hayo kufanyika huku lengo lake kubwa likiwa kuwasaidia wafanyakazi wanaoketi muda mrefu kujiondoa kwenye hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukizwa.
“Tunafahamu wafanyakazi wa benki muda mwingi wanakuwa wamekaa, sasa hii ni hatari kwa afya ikizingatiwa kwamba mtindo huo wa maisha unachangia kwa kiasi kikubwa kuangukia kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Kwa kutambua hilo tumeona tuwe na mashindano ambayo yatawawezesha wafanyakazi kupata muda wa kufanya mazoezi na kuchangamsha miili yao ili kujiweka vizuri kiafya,” amesema Tuse.
Wadhamini wa mashindano hayo benki ya CRDB, kupitia kwa mkuu wa kitengo cha kadi, Farid Seif amesema licha ya kuboresha afya itasaidia katika kukuza uhusiano maana michezo ni ushirikiano.
“Tunafahamu michezo ni burudani, vijana wanapata fursa ya kuonesha vipaji vyao nje ya kazi wanazozifanya kila siku, kama uongozi tumefurahishwa na namna wafanyakazi walivyojitoa kwa dhati kushiriki.
“Tumeonyesha kwa mfano hatukuishia ushiriki wetu kwenye kudhamini michezo, tuna timu makini kabisa ambayo itaonyesha makali yake kwenye mashindano haya,” amesema Seif.
Ofisa hHabari na Mahusiano wa Benki ya NMB, ambao ni wadhamini wengine wa mashindano hayo, Goodluck Ngai amesema: “Ni furaha yetu kuona watu ambao wamezoeleka siku zote wakifanya kazi kwenye kompyuta wanapata fursa ya kukutana na kuoneshana umahiri wao kwenye mchezo wa mpira wa miguu.”