Wadau mkoani Mara walia na uwekezaji hafifu

Musoma. Wadau wa maendeleo mkoani Mara wamesema kasi ya uwekezaji mkoani humo bado iko chini,  licha ya mkoa huo kuwa na fursa nyingi za kiuchumi na uwekezaji, hivyo wameitaka Serikali kufanya jitihada zaidi zitakazosababisha kuongezeka zaidi na kuboresha uchumi wa mkoa.

Wadau hao wamebainisha hayo Julai 5, 2024 kwenye mdahalo kuhusu uwekezaji ulioandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC, ambapo wamesema fursa zilizopo zikitumika vema kutakuwa na mapinduzi chanya ya uchumi wa mkoa na watu wake kwa ujumla.

“Mara tumebarikiwa kuwa na kila kitu lakini bado hizo fursa hazijatumika kuunufaisha mkoa na watu wake, lazima jitihada ziongezeke ili kuhakikisha mkoa unapaa kiuchumi na hili linawezekana tukiamua,” amesema Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwekezaji na Huduma za Masoko na Uwekezaji (Haippa Plc), Boniface Ndengo.

Ndengo amesema zipo njia mbalimbali ambazo zinaweza kutumika ili kuongeza kasi ya uwekezaji mkoani humo, ambapo njia moja wapo ni uanzishaji na utumiaji wa kampuni za umma, jambo ambalo amesema litakuwa na matokeo chanya tena ndani ya muda mrefu.

Amefafanua kuwa kupitia kampuni za umma, changamoto zinazowakabili watu wenye nia ya kuwekeza ikiwa ni pamoja na mitaji na masoko, inaweza kupata suluhisho huku akieleza kuwa kampuni za umma zinaratibiwa na Serikali, lakini zinatoa fursa kwa wananchi kuziendesha kwa manufaa yao.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kuzalisha Mafuta ya Alizeti cha Nyihita kilichopo wilayani Rorya, Nyihita Nyihita amesema hali ya uchumi ya wakazi wa mkoa huo haiendani na utajiri uliopo katika mkoa huo, hivyo ametoa wito hasa kwa vijana kujitokeza na kuanza kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.

“Mara tuna viwanda vya mafuta ya alizeti lakini bado hakuna alizeti ya kutosheleza, inatulazimu kuagiza hadi nje ya mkoa wakati tuna ardhi inayofaa kwa kilimo cha alizeti karibu kila wilaya. Niwaoambe vijana wenzangu tutumie fursa hiyo ya mahitaji ya alizeti tuanze kulima kwani soko lipo la uhakika,” amesema.

Katibu wa MRPC, Pendo Mwakyembe amesema umefika muda sasa Serikali isaidie kutafsiri kwa vitendo, mwongozo wa uwekezaji ulioandaliwa na Serikali ya mkoa ili kuvutia watu wenye nia ya kuwekeza waanze uwekezaji mara moja.

“Inasikitisha kuona fukwe zote za Ziwa Victoria kwenye mkoa wa Mara zikiwa wazi, hakuna shughuli yoyote ya kiuchumi inavyofanyika wakati ukienda mikoa ya jirani unaona namna watu walivyochangamkia fursa hizo. Hii sio sawa, tumechoka kuwa masikini wakati fursa zipo za kutosha.Tunaomba Serikali iangalie namna ya kufanya mkoa uwe imara zaidi kiuchumi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema ni kweli hali ya uwekezaji mkoani humo bado haijaenda sawa na fursa zilizopo,  huku akisema Serikali inafanya jitihada ili fursa hizo zitumike vema.

Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ziwa Victoria, madini ya dhahabu, mifugo na ardhi yenye rutuba huku akiongeza kuwa mkoa huo ndipo alipozaliwa na kuzikwa hayati Mwalimu Julius Nyerere, hivyo fursa hizo zinatakiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi.

“Tuna dhahabu kila wilaya yaani ‘Mara region is a gold carpet area’ (mkoa wa Mara ni ardhi ya dhahabu) na hizi fursa zikitumika vema zitachechemua uchumi wa mkoa, watu wake na taifa kwa ujumla,” amesema.

Related Posts