Uhamiaji yapewa nafasi ya Chipukizi CAF

KLABU ya Uhamiaji imepata nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao 2024-2025.

Hiyo ni baada ya mabingwa wa Kombe la FA Zanzibar, Chipukizi FC kujiondoa katika uwakilishi huo ikidaiwa sababu kubwa ni ukata ilionao.

Taarifa iliyotolewa na Klabu ya Uhamiaji, imebainisha kwamba nafasi hiyo wameipata baada ya ZFF kufuata utaratibu wa kikanuni.

“Tunapenda kuwatangazia wadau wa mpira kuwa tumepata nafasi kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Hii ni baada ya ZFF kufuata utaratibu wa kikanuni kutokana na bingwa wa FA kujiondoa kwenye nafasi ya kuiwakilisha nchi.

“Uhamiaji FC tulimaliza nafasi ya tatu kwenye Kombe FA kwa mujibu wa Kanuni. Mshindi wa pili (JKU) yeye amepata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwa bingwa wa Ligi Kuu.

“Taratibu zote za makubaliano zimetimizwa na sasa Uhamiaji FC ndio tutaiwakilisha Zanzibar kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika.”

Ikumbukwe kwamba, Chipukizi ilitwaa ubingwa wa FA baada ya ZFF kuipa ushindi wa mezani kutokana na mchezo wao wa fainali dhidi ya JKU Kuvunjika dakika ya 103 matokeo yakiwa sare ya 1-1. Vurugu zilizodaiwa kuanzishwa na JKU ndizo zilivunja mchezo huo.

Related Posts