Dar es Salaam. Viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wametakiwa kuipeleka kampeni ya ‘Zima zote, washa kijani’ hadi ngazi ya vitongoji ili kusaidia chama hicho kupata ushindi katika chaguzi zijazo.
Wito huo umetolewa leo Julai 6, 2024 na Katibu wa NEC Idara ya Oganaizesheni na mlezi wa Jumuiya za chama hicho, Issa Ussi Gavu, aliyekuwa akimwakilisha Katibu Mkuu wa CCM Dk Emmanuel Nchimbi, kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo, iliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Kampeni hiyo imelenga kuhamasisha vijana kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kushiriki kugombea nafasi mbalimbali na kujitokeza katika kupiga kura.
Akizungumza na vijana hao waliotoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo, Gavu amesema haitakuwa na maana kampeni hiyo kubwa kuzinduliwa Dar es Salaam halafu isisambae maeneo mengine ambayo ameifananisha kuwa itakuwa ni sawa na kampeni mfu.
“Nataka vijana mlichofanya leo hapa ndio kikafanyike mikoani, wilayani, kata, vijiji hadi kwenye vitongoji jambo litakalosaidia kuleta tija na kupata ushindi tuliokusudia,” amesema Katibu huyo.
Katika kuelekea uchaguzi amesema kutakuwa na mashambulizi ya hoja mbalimbali na kuwasishi vijana wa chama hicho kuhakikisha wanajibu hoja kwa hoja ili kuepusha kuvunja amani ya nchi
Gavu pia ametumia nafasi hiyo kuwaomba wazazi na walezi kuwahamasisha vijana wao kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura na kikifika kipindi cha uchaguzi wawahimize kwenda kugombea.
“Niwahikikishe vijana watakaojitokeza kugombea chama hakitamuacha kijana ambaye alionekana kujitolea kwa jamii pindi jina lake litakapopelekwa kwenye kupitisha majina ya wagombea,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM, Ally Mohamed Kawaida, amesema umati wa watu uliojitokeza ni kiashiria tosha kuwa wanaenda kushinda chaguzi hizo.
“Huu umati ni dalili tosha tunaenda kushinda chaguzi kwa kishindo na nina uhakika mitaa yote viongozi wake watatokana na CCM,” amesema Kawaida.
Awali Katibu mkuu wa UVCCM, Jokate Mwegelo, amesema kampeni hiyo ni katika kujiandaa na uchaguzi wa viongozi wa mitaa,madiwani na wabunge.
Pia amesema wamewakutanisha vijana hao kuwakumbusha umuhimu wa ushiriki wao katika uchaguzi, kupeana matumaini ya kuwafanya wawe imara na kuhalikisha uchaguzi unaenda vizuri.
Katika uzinduzi huo makundi mbalimbali ya vijana walishiriki wakiwemo wanamichezo, wasanii, bodaboda pamoja na vijana wengine wa kawaida waliofikisha umri wa kupiga kura na ambao mwakani wanatarajia kufikisha umri wa kupiga kura.