Mtanzania ahukumiwa kunyongwa China, wengine 26 wakamatwa

Dar es Salaam. Mtanzania mmoja amehukumiwa kunyongwa hadi kufa nchini China kutokana na madai ya kujihusisha na dawa za kulevya, huku wengine 26 wakikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo haramu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambaa mitandaoni, Mtanzania huyo ambaye jina lake halijapatikana mara moja, amehukumiwa kunyongwa katika mji wa Guangzhou nchini humo.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba mamlaka za China zimewajulisha kuwa Mtanzania huyo ataitumikia adhabu hiyo kwa kupigwa sindano ya sumu kisha mwili wake kuchomwa moto na ikiwa kama familia yake itauhitaji mwili wake, itoe taarifa siku tano kabla.

“Familia tumeijulisha na imesema haina uwezo. Hivyo, akishauawa atachomwa moto katika pipa la gesi,” inasomeka taarifa hiyo iliyosambazwa mitandaoni huku ikiwekwa onyo kwa Watanzania kuwa makini, kwani mizigo mingine ni vigumu kusaidiana.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu taarifa hiyo, leo Julai 6, 2024, Balozi wa Tanzania nchini China, Khamis Musa Omar hakutaka kuzungumzia jambo hilo, hata hivyo amesema kwa miaka mingi Watanzania kama ilivyo jamii nyingine duniani, wapo wanaokamatwa na dawa za kulevya.

“Hili si jambo jipya baadhi ya Watanzania kukamatwa na dawa za kulevya nchini China na nchi zingine,” amesema.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa ubalozi aliyepo China ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema kwa kijana aliyehukumiwa kunyongwa, alitakiwa kunyongwa Julai 5, 2024 lakini kutokana na masuala ya kiufundi, haikutekelezwa.

“Ni kweli adhabu ya kunyongwa ingetekelezwa jana Julai 5, 2024 baada ya kubainika kuwa alikuwa anabeba dawa za kulevya. Ninachowaomba Watanzania wafanye yanayowaleta China waachane na tamaa, wengi waliokamatwa tukiwatembelea gerezani wanajutia walichokifanya,” amesema ofisa huyo.

Ofisa huyo alikemea tabia ya tamaa ya vijana akiwaeleza kuwa waache kukimbilia mafanikio kwa njia za mkato.

Ameeleza kuwa China ni sehemu ya biashara kuchukua malighafi, kujifunza masuala ya teknolojia na si eneo la kupeleka dawa za kulevya au kufanya biashara ya ngono.

Mbali na kutoa msisitizo huo, amewataka Watanzania wanaokwenda nchini China kutokubali kuwasaidia watu mizigo yao.

“Kuhusu vijana 26, wapo wanaoshikiliwa kwa muda mrefu na wengine walikamatwa hivi karibuni, hii inajenga taswira mbaya baina ya Tanzania na China ambayo uhusiano wetu umekuwa mzuri,” amesema.

Ofisa huyo amesisitiza uhusiano wa Tanzania na China umesaidia watu wanaokwenda kusoma nchini humo na wengine kufanya biashara, hivyo alisema si vema kuuharibu kutokana na tamaa.

Mwananchi limezungumza na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo kuhusu tukio hilo, hata hivyo amesema atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza atakapopata taarifa rasmi kutoka China.

“Nimeona kwenye mitandao kuhusu taarifa hii lakini siwezi kuizungumzia hadi niwe na taarifa rasmi za kina ambazo tayari tumeshaomba nyaraka kutoka kwa wenzetu China ili kupata undani wake.

Lyimo amesema hadi kufikia Jumatatu Julai 9, 2024, nyaraka hizo zitakuwa zimewafikia, ndipo atazungumzia kwa kina aliyekamatwa ni nani, alikamatwa wapi akiwa na dawa zipi.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuwaelekeza Watanzania kujiweka mbali na biashara hiyo kwa kuwa kila nchi inaweka sheria kali kuwalinda watu wake dhidi ya dawa hizo haramu.

Amesema DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, imefanikiwa kuuvunja mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa kumkamata mtu aliyekuwa akiwatuma vijana kwenda nje nchi.

“Januari tulimkamata kinara wa biashara ya dawa za kulevya akafunguliwa shauri la uhujumu uchumi, linaendelea Mahakama ya mafisadi, tangu wakati huo idadi ya Watanzania wanaokamatwa nje imepungua.”

“Niendelee kuwasisitiza vijana, wasikubali kutumika, huwezi kubaki salama ukijihusisha na biashara hii haramu,” amesema Lyimo.

Related Posts