Guede huyoo Singida BS, mchongo mzima uko hivi!

MSHAMBULIAJI aliyemaliza na mabao sita katika Ligi Kuu Bara na matatu ya Kombe la FA na moja la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita akiwa na kikosi cha Yanga, Joseph Guede huenda akaendelea kusalia nchini licha ya kudaiwa kupewa ‘thank you’ Jangwani, baada ya kudaiwa anajiandaa kutua Singida Black Stars.

Guede alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la Januari akitokea Tuzlaspor FC ya Uturuki akiitumikia kwa miezi sita na anatajwa ni kati ya nyota wa kigeni walioachwa kikosini, ili kupisha mastaa wapya akiwamo Jean Baleke anayeenda kuchukua nafasi yake eneo las ushambuliaji.

Awali mshambuliaji huyo, ilielezwa alikuwa na nafasi kubwa ya kubaki Yanga kutokana na viongozi kutofautiana juu ya kutemwa kwake na hasa baada ya kuelezwa kocha mkuu, Miguel Gamondi hakutaka aondoke kwani anamuelewa sana, lakini kwa sasa ni rasmi anaondoka akimpisha Baleke aliyepewa mwaka.

“Jina hili limetajwa sana hivi karibuni ndani ya kambi yetu, sijajua ni usajili mpya au la lakini nimelisikia akizungumziwa mchezaji huyo kwani ameachwa na Yanga,” kilisema chanzo cha kuaminika kutoka Singida BS inayotajwa ndiko atakapoibukia, kilichoongeza:

“Usajili kwenye kikosi chetu bado unafanyika na kuna idadi kubwa ya wachezaji wanafanya mazoezi kwa upande wa mastaa kutoka Yanga ni Metacha Mnata pekee ambaye ndio tumeanza naye mazoezi, na Guede anatajwa kuwa mbioni kuja, kwa ishu ya Joyce Lomalisa huku haipo kabisa.”

Mshambuliaji huyo alikuwa anatajwa kumpisha mshambuliaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya mambo yamekuwa tofauti kwani tayari Yanga wamemalizana na Baleke na kama atatua Singida atakuwa ni mchezaji wa tatu baada ya Metacha na Zawadi Mauya waliosaini mkataba mapema.

Related Posts