KLABU ya Simba imethibitisha kumsajili kiungo mkabaji Debora Fernandes kwa mkataba wa miaka mitatu.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa na Wekundu hao wa Msimbazi akitokea Klabu ya Mutondo Stars ya Zambia, anamudu kucheza kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji yaani namba nane.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imesemw: Kiungo Debora Fernandes, 24, mwenye uraia pacha wa Congo Brazzaville lakini anayechezea timu ya taifa ya Gaboni amejiunga nasi akitokea Mutondo Stars ya Zambia kwa mkataba wa miaka mitatu.
“Debora anamudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji ingawa mwenyewe anafurahi kucheza kiungo wa juu yaani namba nane.
“Ujio wa Debora unaongeza nguvu kwenye eneo letu la kiungo kwa kuwa anaweza kuzuia na kupiga pasi sahihi kuelekea mbele na kuanzisha mashambulizi.
“Tunaendelea kusuka timu imara kwa ajili ya muda mrefu ndiyo maana usajili wetu umezingatia umri wa wale tunaowasajili.”
Debora ni mchezaji wa saba mpya kutambulishwa ndani ya Simba kipindi hiki cha usajili baada ya Joshua Mutale, Steven Mukwala, Abdulrazack Hamza, Jean Charles Ahoua, Valentino Mashaka na Augustine Okejepha.