Nyumbani kwa Naibu Waziri Ujenzi walilia barabara

Songwe. Wananchi wa Kijiji cha Bwenda kilichopo katika Kata ya Lubanda mkoani Songwe, wamemlilia mbunge wa jimbo la Ileje (CCM) na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya kuhusu ubovu wa barabara katika jimbo hilo ambayo haipitiki wakati wa masika.

Wananchi hao, pia, wamemlalamikia mkandarasi aliyetekeleza mradi wa barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura), kwa kuchimba na kuitelekeza barabara hiyo kiasi cha kutopitika wakati wa msimu wa mvua.

Barabara hiyo inayolalamikiwa ina urefu wa kilomita tatu na inatoka Mtula – Bwenda na inatarajiwa kugharimu Sh201 milioni.

Wananchi wametoa malalamiko hayo mbele ya Kasekenya ambaye licha ya kuwa mbunge wa jimbo hilo, pia ana dhamana na wizara inayohusika na masuala ya ujenzi. Kasekenya alikuwa akisikiliza na kutatua kero za wananchi wake ambao waliitaja barabara hiyo kuwa kero.

Hata hivyo, Kasekenya amesema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo na kuwa tayari wameshapata mkandarasi mwingine ambaye kuanzia Agosti 2024, atakuwa ameanza kutengeneza barabara hiyo.

Diwani wa kata ya Lubanda, Kambola Kapushi amesema  barabara hiyo  imegeuka adha kutokana na mkandarasi kuutelekeza mradi huo tangu mwaka jana.

Kapushi amesema mazao ya wananchi yanaozea shambani kutokana na kushindwa kusafirisha, jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi.

Hata hivyo, Kapushi amesema soko la mazao kama vile ndizi ambalo linategemewa na wananchi wa Mbeya kupitia Wilaya ya Rungwe, mkungu unauzwa Sh3,000 ambapo kwa kata jirani ya Luswisi, mkungu mmoja unauzwa Sh7,000 hadi 8,000.

“Endapo barabara hiyo itakamilika, itakuwa imerahisisha shughuli za usafiri kwani barabara hiyo ni kiunganishi  na kata ya Ngulilo wilayani humo,” amesema Kapushi.

Dereva bodaboda katika kijiji cha Bwenda, Omary Kapushi amesema kama vijana waliojiajiri kufanya kufanya shughuli hiyo, wanapata shida kusafirisha abiria kipindi cha masika, kwani huwezi kumbeba mama mjamzito kwenda kituo cha afya Lubanda, hivyo wanajifungulia njiani.

Akijibu malalamiko ya wananchi hao, Kasekenya amesema wanatambua umuhimu wa barabara hiyo na sasa tayari wameshapata mkandarasi mwingine ambaye ataanza Agosti 2024.

“Natambua barabara hii ni muhimu kusafirisha ndizi, mbao na kahawa, hivyo miundombinu kutokuwa rafiki inapunguza uchumi, mniamini, kuanzia Agosti, mwaka huu, mkandarasi atakuwa eneo la kazi kumalizia kazi kwani tayari kifusi kipo,” amesema Kasekenya.

Kasekenya amesema ahadi yake ya kwanza tangu aingie madarakani ni kufungua barabara ikiwepo ya Mtula – Bwenda ambayo haikuwepo awali na changamoto iliyopo ni kutokuwa rafiki kwa watumiaji.

Amesema hatua inayofuata ni kuhakikisha barabara hiyo inapitika muda wote ili kuinua uchumi wa wananchi,  kwani mkandarasi aliyekuwepo aliondolewa na akatafutwa mkandarasi mwingine ambaye yupo kwenye maandalizi ya kuja kufanya kazi.

Related Posts