BIMA YA AFYA KWA WOTE IPEWE KIPAUMBELE DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050- WAZIRI UMMY

Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam

SUALA La Bima ya Afya kwa wote limetakiwa kupewa kipaumbele zaidi katika maandalizi ya Dira ya Taifa 2050 ili kuboresha zaidi huduma za afya ili kila mtanzania awe na afya bora na kuweza kulitumikia Taifa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika kongamano la kitaifa la wadau wa sekta ya ya Afya kuhusiana na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema, Katika kuijenga Tanzania tuitakayo lazima wananchi waone umuhimu wa kuwekeza katika afya na kuingizwa kwa suala la Bima ya Afya kwa wote katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutasaidia kuboresha huduma za afya nchini.

Akieleza mafanikio ya sekta hiyo Waziri Ummy ameeleza kuwa ni pamoja na kufanikiwa kwa kiwango cha juu kwa wanawake kujifungulia katika Vituo vya Afya, kwa kuongezeka kutoka asilimia 41 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 81 kwa sasa na mpango ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2025.

Waziri Ummy amesema changamoto kubwa katika sekta ya afya ni ugharamiaji wa huduma za afya, huku akitaja changamoto kubwa kuwepo katika magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo, kisukari na afya ya akili.

“Tukiwa na Bima ya afya kwa wote tutafanikiwa kwa kuwa huduma za afya ni kila kitu, Nchi nyingi katika uchaguzi angalieni Marekani, Uingereza na kwingineko kampeni kubwa ni kuhusu bima ya afya na hifadhi ya jamii, kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika gharama za matibabu.” Amesema Ummy.

Aidha kuhusiana na changamoto ya ugharamiaji huduma za matibabu kwa wasiojiweza Waziri Ummy ameeleza kuwa, baada ya muswada kuwa sheria na kuona namna gani watanzania wasio na uwezo watachangia Rais Samia Suluhu Hassan alielewa suala hilo.

“Na tayari chanzo cha ugharamiaji kimepatikana sasa hivi kitagharamia wazee wasio jiweza, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wajawazito na tutaanzia kwa watoto wa umri sifuri mpaka miaka miwili,” ameeleza Waziri Ummy.

Akizungumza katika Kongamano hilo Waziri wa Nchi; Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema tafiti imeonesha kuwa asilimia 81 ya Watanzania wanahitaji mabadiliko katika huduma za kijamii ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya.

Maoni hayo yaliyokusanywa na Tume ya Mipango kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutoka kwa watanzania zaidi ya milioni moja, asilimia 81 ya waliohojiwa walipendekeza uboreshaji wa huduma za afya huku asilimia 19 wakitaka upatikanaji wa huduma za afya.

Ameeleza kuwa maoni ya wadau hao ni muhimu na yatapewa kipaumbele katika kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaleta tija kwa jamii.

Wadau wa sekta ya afya nchini, wametoa maoni yao na kushauri kupewa kipaumbele kwa Bima ya Afya kwa wote ili kuboresha huduma zinazotolewa pamoja na kuwekwa kwa mfumo rasmi katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kupambana na changamoto ya ajira kwa wahitimu wa kada ya Afya wakiwemo madaktari na wauguzi kwa kuwa kada hiyo ni muhimu na wanahitajika zaidi katika jamii hivyo kukosekana kwa wataalam hao huchagiza changamoto ya ubora wa huduma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma (BMH,) Prof. Abel Makubi akitoa maoni katika kongamano hilo amesema kuwa ni muhimu kuwa na mikakati ili fedha inayowekezwa katika kusomesha na mafunzo kwa wataalamu hao ilete tija kwa jamii.

Pia Katibu Mtendaji; Tume wa Mipango Lawrence Mafuru amesema mwongozo na usimamizi wa matayarisho ya Dira hiyo ulipitishwa na Baraza la Mawaziri na utakuwa sheria pindi utakapokamilika rasmi na kuongeza kuwa michango mingi katika simu na midahalo watanzania wanahitaji huduma bora za afya na kueleza kuwa maoni yatakusanywa hadi Agosti mwaka huu na baadaye kupangwa kwa ajili ya utekelezaji.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imejikita katika maeneo sita ikiwemo maboresho ya Utawala bora, Haki na Amani,Uchumi na Jamii,Utunzaji wa mazingira sayansi ya mabadiliko ya kidijitali na mabadiliko ya tabia Nchi.

Wadau walioshiriki kongamano hilo ni pamoja na Taasisi za Utafiti, wamiliki wa vituo binafsi vya Afya, Taasisi za Elimu, watoa huduma za Afya, Waganga wakuu wa mikoa na wataalam wa Afya.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza katika kongamano la kitaifa la Wadau wa Sekta ya Afya kuhusiana na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kueleza kuwa kipaumbele kwa Bima ya Afya kwa wote ni muhimu ili kuboresha huduma za afya. Leo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi; Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo akizungumza katika kongamano la kitaifa la Wadau wa Sekta ya Afya kuhusiana na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kueleza kuwa utafiti unaonesha asilimia 81 ya watanzania wanahitaji mabadiliko katika huduma za kijamii ikiwemo uboreshaji wa huduma za Afya. Leo jijini Dar es Salaam.

Matukio mbalimbali wakati wa kongamano hilo.
 

Related Posts