Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Katibu Mkuu wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Maborok Khamis, amehimiza wafanyabiashara kutumia fursa zinazotokana na uhusiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea ili kufaidika na soko la bidhaa mbalimbali, ikiwemo korosho, karafuu, chai, na kahawa.
Akizungumza Julai 6, katika Maonesho ya 48 ya Kibiashara ya Kimataifa (Sabasaba) jijini Dar es Salaam, Fatma alisema lengo kuu la Siku Maalum ya Jamhuri ya Korea ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Korea Kusini.
Fatma alisema Korea inaonyesha uhitaji mkubwa wa bidhaa za Tanzania na kwamba kampuni za Tanzania zina fursa ya kujifunza teknolojia ya kisasa kwenye uzalishaji wa bidhaa. Pia, alisisitiza umuhimu wa viongozi kuhamasisha wawekezaji kuwekeza Tanzania na kushughulikia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Dorothy Urio, alisema wadau kutoka Korea wanahitaji madini, korosho, na bidhaa nyingine kutoka Tanzania, na kwamba kuboresha mnyororo wa thamani wa korosho ni muhimu.
Mshauri wa Siasa na Uchumi kutoka Ubalozi wa Korea, Hyunseok Jeong, alisema hii ni mara ya kwanza kushirikiana na Tantrade, na kwamba uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili utaendelea kushirikiana na kubadilishana uzoefu.
“Inakumbukwa Juni mwaka huu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alitembelea Jamhuri ya Korea, hivyo uhusiano wa nchi hizi mbili ni mzuri,” alisema Jeong.