Buswita bado yupo Namungo | Mwanaspoti

KIUNGO mshambuliaji, Pius Buswita amekata mzizi wa fitina kwa kuamini kusaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kukipiga Namungo akimaliza uvumi kwamba alikuwa anaachana na timu hiyo ili atue kwingine.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, alikuwa akiwaniwa na Dodoma, JKT Tanzania na Mashujaa, lakini akaamua kusalia kwa Wauaji wa Kusini baada ya kuvutiwa na ofa  sambamba na mambo mengine kadhaa tofauti na klabu zilizokuwa zikimfukuzia.

Buswita aliyemaliza msimu ulioisha kama kinara wa mabao  wa timu hiyo, akifunga saba na asisti mbili, alisema katika misimu mitatu timu hiyo ilimaliza nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu, jambo lililomfanya akatae ofa nyingine na kuendelea kusalia kikosini hapo.

“Kabla ya msimu ulioisha kumaliza nafasi ya sita, misimu miwili nyumba tulimaliza nafasi ya tano, hivyo unaweza ukaona ni timu ambayo ipo imara kwenye Ligi Kuu. Nimesaini miaka miwili ya kuendelea kuitumikia, najua usajili mpya unafanyika, hivyo najipanga kwa changamoto mpya za ushindani, kuhakikisha napata nafasi ya kucheza,” alisema Buswita aliyewahi kuwika na Mbao FC.

“Japo sijasaini timu zilizonifukizia, lakini nisewe wazi zote ni nzuri, nje na pesa, mchezaji anapojiunga na timu, anaangalia vitu vingi, ikiwemo nafasi ya kucheza kikosini,” alisema Buswita akifafanua juu timu zilizomtaka.

Related Posts