HATIMAYE baada ya kumsaka kwa miaka mingi, Yanga wamempata mtu wao. Clatous Chama. Mwamba wa Lusaka. Afadhali amekwenda Yanga. Tulichoshwa na uvumi wa kila siku kuhusu Chama kwenda Yanga. Hata mashabiki wa Simba walichoshwa na uvumi huu.
Kuna tafsiri nyingi kwa Chama kwenda Yanga. Kwanza kabisa kunaifungulia milango Simba kutengeneza timu ambayo haina mfalme mmoja mkubwa klabuni. Walimuacha Chama akawa mkubwa kupita kiasi. Nadhani wapo ambao hadi sasa hawaamini kuwa Chama amekwenda Yanga.
Mfano ni namna ambavyo wameshindwa kutoa ‘THANK YOU’ kwa Chama mpaka sasa. Nasikia walikuwa wanapambana kadri walivyoweza kurudisha pesa ambayo Yanga wamempa Chama ili waendelee kubakia naye.
Awali Simba walijiridhisha kwamba hawamtaki Chama. Baadaye mioyo yao ikasita na wakamwambia tajiri yao Mohamed Dewji, kwamba Chama alikuwa karata muhimu kwa umaarufu wake klabuni hapo baada baadhi ya mashabiki kuwa na wasiwasi naye kuhusu ufadhili na udhamini wake Simba.
Yote yamebakia kuwa historia na sasa Chama amekwenda Yanga. Napita mitaani na kukutana na maswali yanayochekesha kutoka kwa wachambuzi na mashabiki wetu. Chama atakwenda kuchukua nafasi ya nani Yanga?
Mashabiki na wachezaji wetu bado wanaishi katika dunia ya kikosi cha kwanza. Pep Guardiola alituondoa katika dunia hii. Mpira wa sasa una kasi kubwa na una idadi kubwa ya mechi. Unahitaji wachezaji wengi wazuri katika nafasi zote uwanjani. Waingereza wanaita options.
Pale Manchester City upande mmoja wangeweza kuwepo Phil Foden na Jack Grealish. Upande mwingine wangekuwepo Riyad Mahrez na Bernado Silva. Hapo ni nani yupo katika kikosi cha kwanza? Hauwezi kujua. Anachojua Pep ni kwamba mechi hii angeweza kuanza na Silva hadidakika ya 60 halafu akaingia Mahrez. Mechi ijayo angeanza Mahrez na Silva akaingia baadaye.
Kuna mechi ambazo Kevin De Bruyne pia anakaa benchi na Ilkay Gundogan anaanza. Utajiri wa vipaji vingi katika kila nafasi umefanywa kwa makusudi na Pep kupitia pesa za matajiri. Hii inasaidia wachezaji kupumzika.
Natazama pia za mitandaoni ambazo zinawaonyesha kwa pamoja Stephane Aziz Ki, Chama, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli. Mashabiki wanatamani hawa wote waanza kwa pamoja na mbele yao asimame Prince Dube. Miguel Gamondi anaweza kujikuta akifanya kosa kwa kuwaanzisha wote kwa pamoja.
Wakati mwingine ukiwaanzisha mastaa wote kwa pamoja timu inakosa uwiano. Wachezaji hawa wenye vipaji wanapaswa kulindwa na wachezaji wenye kariba ya ukabaji na matumizi mazuri ya nguvu. Real Madrid waliwahi kutengeneza timu ya ndotoni kama hii wakaishia kuwa kichekesho kutokana na ukosefu wa uwiano kati ya ukabaji na ushambuliaji.
Florentino Perez kwa pamoja aliwachukua David Beckham, Zinedine Zidane, Luis Figo, Raul Gonzalez na Ronaldo de Lima akataka wote wacheze kwa pamoja. waliitwa Galacticos. Waliishia kuambulia vichapo vya mara kwa mara kwa sababu timu ilikosa wakabaji. Mbaya zaidi akamuuza Claude Makelele kwenda Chelsea baada ya kugoma kumuongezea mshahara.
Perez alikuwa na sababu zake za kibiashara zaidi kufnya hivyo ili mauzo ya jezi yaongezeke lakini pia mashabiki waendelee kununua tiketi kwa wingi ili kuiona timu hii ya ndotoni ikisakata soka. Hata hivyo mpango mzima ulishindikana kutokana na wachezaji wengi mastaa kutokuwa wakabaji sana uwanjani. Walijikuta wanatembea zaidi wakati hawana mpira kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kiliwagharimu walinzi. Zidane, De Lima, Figo, Beckham wote sio wakabaji wazuri wakati timu haina mpira.
Gamondi kama kocha mwenye akili timamu sio lazima awaanzishe wote kwa pamoja hasa katika mechi kubwa ambazo Yanga nao watalazimika kukaba. Kinachopaswa kufanyika ni wengine kuanzia nje kwa ajili ya kuingiza wachezaji watakaoweza kufanya kazi chafu.
Lakini Yanga wanapata faida pia kama wakikabiliwa na mazingira magumu kama waliyopitia katika mechi mbili dhidi ya Mamelodi Sundowns. Pacome na Khalid Aucho waliumia. Ina maana kama wangekuwa na Chama bado angeshirikiana vema na Aziz Ki katika kuleta ubunifu eneo la mwisho.
Yanga kama ilivyo kwa Simba na Azam, wanakabiliwa na mechi za CAF, Ligi Kuu, FA na njiani wanalazimika kushiriki michuano ya kisiasa ya Mapinduzi Cup. Hii ni achilia mbali ukweli kwamba Simba na Yanga wanaweza kushiriki michuano ya Super League ambayo ilianzishwa na Patrice Motsepe kwa siasa zake.
Ina maana kunaweza kuwa na idadi ya mechi zaidi ya 55 ndani ya msimu mmoja. Hauhitaji sana First eleven katika hili. Tayari Yanga wameonekana kumudu jambo hili na ndio maana hata walipoondoka Fiston Mayele, Fei Toto, Djuma Shaaban na Yannick Bangala bado waliendelea kutamba.
Chama anaenda kuwapa Yanga nafasi ya machaguo mengi uwanjani. Sidhani kama anaenda kupora nafasi ya mtu. Hata Dube anakwenda kuwapa Yanga machaguo mengi uwanjani lakini sidhani kama ndio anakwenda kuwa mshambuliaji kinara zaidi.
Mpira wa kisasa umebadilika. Mifumo pia imebadili mpira wa kisasa. Kuna wakati unalazimika kujaza wachezaji wa aina fulani kutokana na tabia ya mechi yenyewe itakavyokwenda. Lakini jaribu kufikiria ni namna gani mchezaji mmoja anaweza kucheza mechi 55 bila ya kuchoka. Unawezaje kumaliza msimu bila ya kuwa hoi?
Jicho linakwenda kwa Gamondi kwa namna ambavyo atawatumia mastaa wake. kama atawatumia kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki anaweza kujikuta kilioni kama ilivyokuwa inawatokea Real Madrid wakati ule. Binafsi siamini kama atakwenda na akili za mashabiki.