WACHEZA gofu ya kulipwa na ridhaa wanaanza kuondoka leo kwenda Arusha kwa ajili ya kusaka kitita cha Sh50 milioni ambazo ni zawadi kwa washindi wa raundi ya tatu ya Lina PG Tour itakayoanza Alhamisi hii kwenye viwanja vya Arusha Gymkhana jijini humo.
Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti wikiendi iliyopita, wacheza gofu kutoka klabu za Lugalo, Dar Gymkhana, TPC na Morogoro waliokuwa wanashiriki mashindano ya Lugalo Open, wamesema raundi ya tatu si ya kukosa kwa sababu ina vingi vya kuvutia licha ya zawadi nono ya pesa iliyoandaliwa kwa washindi wa madaraja mbalimbali.
“Niko timamu baada ya mazoezi ya kutosha nafikiri nitaendelea kung’ara hata huko Arusha,” alisema Ally Isanzu anayeongoza mbio za taji la Lina PG Tour kwa wachezaji wa ridhaa.
Vilevile, Nuru Mollel kutoka Arusha, ambaye juzi Jumamosi aliibuka mshindi wa Lugalo Open kwa wachezaji wa kulipwa alitegemewa kuondoka jana usiku kwenda Arusha tayari kwa raundi ya tatu.
“Siamini kama nitapata shida kubwa kwenye uwanja wa nyumbani na nimejizatiti kuhakikisha nafanya vizuri huko licha ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wachezaji wengine,” alisema Mollel.
Mmoja wa wacheza gofu waliotamka azma yao ya kuiteka raundi ya tatu ya Lina PG Tour, ni Iddi Mzaki kutoka Dar es Salaam ambaye amedai atayatumia mashindano ya Arusha vyema safari hii baada ya kuwa na matokeo yasiyoridhisha katika raundi ya pili ya mashindano haya mjini Morogoro.
“Nitatumia raundi hii kufuta makosa yangu ya raundi za awali,” alisema.
Kwa mujibu Mkurugenzi wa Lina PG Tour, Yasmin Challi, raundi hii ni ya tatu kati ya tano za mfululizo wa mashindano maalum ya kumuenzi Lina Nkya, ambaye wakati wa uhai wake, alifanya kazi kubwa ya kuilea gofu ya wanawake kimafanikio hadi kuwafanya wanawake wa Kitanzania kung’ara katika mashindano tofauti katika ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika na yale ya dunia yaliyofanyika Argentina kiasi cha muongo mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa Challi, mashindano haya ya raundi ya tatu yatafanyika kati Julai 11 hadi 14 mwaka huu kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Arusha.
Wacheza gofu ya kulipwa; Nuru Mollel aliyeshinda raundi ya kwanza katika viwanja vya TPC Moshi na Hassan Kadio aliyeutwaa ubingwa wa raundi ya pili mjini Morogoro, ni baadhi ya wacheza gofu nyota waliosajiliwa kucheza katika raundi hii ya tatu.
Vilevile, Ally Isanzu ambaye alishinda raundi zote mbili za mashindano hayo kwenye viwanja vya TPC, mwezi Machi na viwanja vya Gymkhana Morogoro mwezi Aprili mwaka huu, ndiye anayeongoza orodha ya wachezaji 19 wa ridhaa watakaowania taji na kitita cha zawadi katika viwanja vya Gymkhana Arusha, kwa mujibu wa Challi.
Akifafanua, Challi alisema wachezaji wa ridhaa wanaokubalika kushiriki mashindano ya mwaka huu ni wale wenye kiwango pungufu cha tano (5 handicap).