Wamachinga wanavyoitesa Serikali | Mwananchi

Dar/mikoani. Uamuzi wa Serikali kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga barabarani na kuwapatia maeneo rasmi ya kufanyia shughuli zao, umeonekana kugonga mwamba.

Hiyo ni baada ya makundi ya wafanyabiashara hao, kushuhudiwa yakirejea kwa kasi barabarani, huku ugumu wa biashara katika maeneo waliyopangiwa ukitajwa kuwa moja ya sababu.

Kwa mujibu wa wamachinga wenyewe, kupangwa maeneo yaliyotajwa kuwa rasmi kwao kumefanyika bila kuzingatia miundombinu sahihi, hali iliyochochea uchache wa wateja na hivyo kudumaza biashara zao.

Kwa sababu hiyo, wafanyabiashara hao katika mikoa mbalimbali nchini, wameyahama maeneo waliyopangiwa na kurejea barabarani, wanakodai kuna idadi kubwa ya wateja.

Vuguvugu la kupangwa kwa wafanyabiashara hao lilianza Septemba 13, 2021 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwataka wakuu wa mikoa yote nchini kuratibu jambo hilo bila kutumia nguvu.

Sambamba na wakuu wa mikoa, aliwataka wamachinga pia kuhakikisha wanawasikiliza viongozi hao na wanafuata sheria na kanuni pale watakapopangiwa maeneo ya kufanyia shughuli zao.

Msingi wa maelekezo hayo ni kuhakikisha mikoa yote nchini inakuwa na mazingira safi na rafiki kwa wafanyabiashara wote.

Utekelezwaji wa maelekezo hayo ulianza mara moja, kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini kutenga maeneo ya biashara kwa ajili ya wamachinga.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, masoko ya Machinga Complex, Kisutu, Ilala, Kijichi, Kisemvule, Kamchea na Toangoma, yalipangwa kwa ajili ya machinga.

Masoko mengine yaliyopangwa ni Mtambani, Mwenge Cocacola, Kigogo Sambusa, Mawasiliano, Big Brother na Mbezi Shule.

Mkoani Mbeya, wamachinga walipangiwa kwenda kufanya shughuli zao katika soko la Old Airport.

Kama ilivyofanyika katika mikoa hiyo, maeneo mengine ya Tanzania wafanyabiashara hao walipangiwa maeneo rasmi ya kufanya shughuli zao, lakini wameyaacha na kurejea barabarani.

Juzi, baada ya kuwaapisha mawaziri aliowateua, Rais Samia alitoa maelekezo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo kwenda kuangalia jinsi ambavyo Karikakoo itafanya kazi saa 24 na kumtaka kila baada ya miezi mitatu awe anawasilisha taarifa ya shughuli za biashara zinavyokwenda nchini.

Pia alimtaka Dk Jafo kwenda kuangalia eneo la biashara, ili wafanyabiashara na wamachinga wakafanye shughuli zao vizuri.

Mwananchi limeangazia mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Dodoma na Mwanza hali ilivyo na kushuhudia kurejea kwao, huku mamlaka za mikoa hiyo ikieleza mikakati mbalimbali.

Mazingira magumu ya biashara katika maeneo ambayo Serikali imewapeleka ndizo sababu za kurejea kwa wamachinga barabarani, kama inavyoelezwa na Selina Joram anayefanya biashara eneo la Mbezi Mwisho, jijini Dar es Salaam.

Mazoea nayo ni sababu nyingine iliyotajwa na Haule anayefanya biashara katika soko la Kariakoo tangu mwaka 2008, akisema hana mbinu za kupata wateja nje ya soko hilo.

“Haya maisha wengine tumeshayozoea na kwa kuwa ndio ajira yetu tunavumilia, mie nipo hapa kitambo najua kuna msimu wanapoa na maisha yanaendelea,” amesema.

Amehusisha kuondoshwa kwao na masuala ya kisiasa, akisema kwa nyakati kama hizi unapoelekea uchaguzi (wa Serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025), hakuna anayewasumbua.

“Mfano sasa hivi kuelekea uchaguzi, hakuna mtu anatushika hapa, wanajua tutakuja kuwaadhibu kwenye kura, ila ukiisha tu watu tujipange, kwani kila ikifika kipindi hiki ndivyo inavyokuwaga hivi,” amesema Haule. 

Wingi wa wamachinga barabarani kwa mujibu wa Masi Yussuf, anayefanya biashara Kariakoo unatokana na ongezeko la vijana wanaofanya shughuli hizo baada ya kuhitimu ngazi mbalimbali za elimu bila kupata ajira.

“Wapo waliomaliza darasa la saba mwaka jana, kidato cha nne na wale wa kidato cha sita ambao wameshindwa kuendelea na shule kutokana na sababu mbalimbali, hawa tupo nao huku mtaani,” amesema.

Ugumu wa biashara katika maeneo waliyopelekwa umeibuliwa pia na Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Yusufu Namoto aliyesema miundombinu ya maeneo hayo ni changamoto.

Amesema changamoto nyingine ni kubomolewa kwa baadhi ya masoko makubwa na yanapokamilika wafanyabishara hao wanaachwa kando na kuchukuliwa wengine, hali inayosababisha wakimbilie mtaani.

Ametaja Soko la Mbagala, Stendi ya Magufuli na Koko la Kariakoo, akisema maeneo rasmi hupewa watu wenye uwezo mkubwa kifedha, huku wenye uwezo wa chini wakiachwa bila kuwa na maeneo. 

Pamoja na hatua hiyo, wamachinga wameendelea kurudi kwenye maeneo waliyohamishwa, huku uchafu wa mazingira ukikithiri.

Maeneo ambayo yamekithiri wafanyabiashara hao ni Karikaoo, Mbagala Rangi Tatu, Gongolamboto, Mwenge, Mbezi, Kivukoni na Kigamboni.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila Julai 4, 2024 alipoulizwa suala hilo alimtaka mwandishi kumtumia ujumbe na hata alipotumiwa, hakujibu.

Alipoulizwa Julai 5, 2024, alisema, “suala hilo la wamachinga ndugu mwandishi naomba tuwasiliane baadaye, tafadhali.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya, amekiri kurejea kwa wafanyabiashara hao na kueleza ni kutokana na ufinyu wa maeneo yanayoendana na mazingira yao ya kufanyia kazi.

“Tunaliona hili la wafanyabiashara na tayari tumeliwekea mpango ambapo Soko la Tandale na lile la Tandika tumeyatengea Sh6 bilioni kila moja kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao. Kazi hiyo itaanza wakati wowote kuanzia sasa,” amesema Mabelya.

James Samwel, anayefanya shughuli za umachinga mkoani Mbeya, amesema mitaji midogo waliyonayo haikidhi kuwaweka katika maeneo rasmi, hivyo wanalazimika kuzurura barabarani.

“Tunaamua kurejea mjini kutokana na sehemu tunazopangiwa kutokuwa safi kwa biashara, kule Old Airport hakuna mzunguko wowote wa biashara, tulienda njaa almanusura ituue.

“Kama Serikali ina dhamira ya kweli, kutupeleka huko waboreshe mazingira, kwani vyoo hakuna, maji ni shida, barabara ni vumbi kali, hakuna mzunguko wa biashara” amesema Samwel.

Mfanyabiashara mwingine, Hafidh Juma amesema sehemu ya machinga ndio imekuwa kimbilio la wahitimu wa elimu ya vyuo vikuu, vya kati, vidogo na kiwango chochote cha elimu kutokana na ukosefu wa ajira.

“Nimehitimu chuo tangu mwaka 2015, fakati ya Ofisa Rasilimali Watu (HR), nimeomba ajira muda mrefu sipati, nimejikusanya nikapata mtaji mdogo naendesha maisha,” amesema Juma.

Kwa upande mwingine, mfanyabiashara Bariki John amesema uwapo wa machinga katika eneo hilo umesababisha kero, kwani wanaziba maduka yao na wateja wengi huishia eneo la machinga na kuwafanya wao kukosa mapato.

Amesema bado wanaona kuwapo dalili za ‘watu wa juu’ kuwatumia wamachinga kujinufaisha na kuwafanya wenye maduka wanaolipa pango na kodi serikalini kuingia hasara.

“Sisi waliopanga maduka hasa maeneo ya ndani ya soko tunakosa wateja kwa kuwa wengi wanaishia huko nje walipo wamachinga. Nadhani ‘walio juu’ wamewapa mitaji kutudumaza,” amesema John.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alipotafutwa kuzungumzia jambo hilo amesema yuko safarini nchini China.

Akizungumza kwa niaba ya Homera, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema kwa kutambua thamani ya wamachinga, Serikali mkoani humo ipo hatua za mwisho kukamilisha miundombinu iliyoonekana kutokuwa rafiki.

“Kwa maana haitatumika nguvu yoyote bali tutashirikisha mamlaka zote tupitie maeneo yote ikiwamo barabara, maji, vyoo na sehemu zote ili tujiridhishe kwa pamoja waweze kurudi sehemu yao,” amesema Malisa.

Naye Ofisa Biashara Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Furaha Mkonongo amesema licha ya wamachinga kuwapo wengi eneo la Kabwe, wapo kwenye operesheni maalumu ya kuwaondoa.

Jijini Mwanza nako wafanyabiashara wamerudi maeneo waliyoondolewa, licha uongozi wa jijini hilo kuanzisha Kikosi kazi maalumu kukabiliana na wafanyabiashara hao.

Kikosi kazi hicho kinachoundwa na askari wa Jeshi la Akiba, yaani mgambo wenye gari aina ya Toyota Hilux, kwa nyakati tofauti kimeonekana kikipita katikati ya jiji hilo na kukwapua bidhaa za wamachinga wanaofanya biashara maeneo yaliyokatazwa.

Jiji hilo linakadiriwa kuwa na wamachinga zaidi ya 9,000.

‘Wanaathiri walipo kodi’

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema uwepo wa wamachinga katikati ya jiji hilo si tu unaikosesha Serikali mapato (bila kutaja kiasi) na kuathiri biashara za walipa kodi, pia unachangia uchafuzi wa mazingira, huku akidokeza kuwa asilimia 25 ya taka zinazokusanywa katikati ya jiji hilo huzalishwa na wamachinga hao.

“Jiji la Mwanza linazalisha taka zaidi ya tani 350 na asilimia 25 ya taka hizo, sawa na tani karibia 90, wakati wanaozalisha kiwango hicho cha taka hawalipi ushuru wa taka wala ushuru wa huduma,” amesema Kibamba.

Kibamba amewataka machinga jijini humo kutokaidi maelezo aliyotoa ya kuwapeleka kufanya biashara zao kwenye masoko yaliyoelekezwa, likiwemo Soko la Mchafukuoga, Buhongwa, Dampo wilayani Nyamagana na Soko la Bango la Zein, Kilimahewa na National (Nyasaka) wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza kwenye kikao na Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza Julai 6, 2024, Mkuu wa Mkoa, Said Mtanda amesisitiza kuwa msimamo wa Serikali ni kuona wamachinga wakifanya biashara katika maeneo yaliyoelekezwa na kuendelea kutekeleza agizo ya Rais Samia Suluhu Hassan la kuwapanga wafanyabiashara hao.

“Tuweke juhudi zetu wakati tunawapanga wamachinga, tunafanya zoezi la wananchi kulipa kodi, lakini tufanye pia iende sambamba na uboreshawaji wa masoko yetu, ili tunapogombana na hawa watu wawe na maeneo ya kwenda,” amesema Mtanda.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Muungano wa Wamachinga Mkoa wa Mwanza (MWM), Said Tembo, machinga ni mfanyabiashara anayemfuata mteja, hivyo uamuzi wa kuwaondoa katikati ya jiji hilo unaondoa tafsiri ya neno ‘Machinga’.

Tembo amesema hata katika masoko walikopelekwa hakuna miundombinu ya kuridhisha na inayowafanya wafanyabiashara hao watulie kwa kile alichodai masoko hayo hayana wateja wa kutosha kwa ajili ya bidhaa zao.

“Wamachinga tunapenda maeneo yenye mikusanyiko ya kutosha, ili tuuze bidhaa zetu na tupate fedha ya kuhudumia familia zetu na kulipia kodi ya pango huko tunakoishi, sasa ukitupeleka eneo ambalo hakuna wateja lazima turudi tunapoona kuna wateja,” amesema Tembo.

Kuhusu masoko yaliyojengwa, Tembo amesema uamuzi huo haukuwa shirikishi, badala yake ulifanywa na wataalamu wa jiji hilo waliopendekeza wamachinga kuhamishiwa katika sehemu ambazo hawakuzipendekeza.

Jijini Arusha nako hali ni hiyo hiyo, ambapo sasa wamachinga wameiomba Serikali iwatengenezee mfumo rafiki, ili watumie maeneo rasmi yaliyotengwa na Serikali.

Licha ya uongozi wa Jiji la Arusha kujenga masoko mawili kwa ajili ya machinga, wameacha kuyatumia masoko hayo ambayo yamejengewa miundombinu na Serikali.

Maeneo yaliyojengwa ni pamoja na Machame, Ulezi na Olmatejoo, ambayo kwa sasa wafanyabiashara wachache ndiyo wapo, wengine wamerudi kandokando mwa barabara, ikiwemo ya Soko Kuu la Arusha na Kilombero.

Wamachinga waliozungumza na Mwananchi, wamelalamikia mazingira mabovu ya kufanya biashara na kwamba hayana mzunguko wa biashara.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Wilaya ya Arusha, Paulo Sanga, ameiomba Serikali itengeneze mfumo rafiki, ikiwemo pale wanapotekeleza miradi inayogusa kundi hilo, wawape nafasi ya kutoa mawazo yao kama walengwa.

“Tunaomba Serikali itutengenezee mfumo rafiki, mfano inapoleta mradi unaogusa kundi la machinga watupe nafasi ya kutoa mawazo sisi kama walengwa, waweke mazingira yanakofikika, kupitia mawazo yetu wakifanya tafiti wataamua jambo ambalo ni rafiki kwetu sote,” amesema.

Arafa Idd, machinga nje ya Soko Kuu la Arusha, amesema eneo la Machame walilopangiwa halikuwa na wateja, hivyo kushindwa kuendelea kufanya biashara na kuamua kurejea barabarani kama ilivyokuwa awali kabla hawajatengewa maeneo.

“Tulikaa kule kwa muda, ila tatizo hakuna mzunguko wa wateja, tukajikuta tumetaka tamaa kwani tuna mikopo, hivyo kila wiki tunadaiwa marejesho, tunashindwa kukaa mahali ambapo hakuna wateja, ndiyo maana nimerudi huku barabarani na ninauza kweli,” amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii jiji la Arusha, Isaya Doita, amekiri wamachinga kuwa mfupa mgumu na kudai miongoni mwa sababu ni pamoja na watendaji waliopendekeza masoko hayo kujengwa katika maeneo ambayo hayana mzunguko wa watu.

“Tukubaliane waliofanya uamuzi, ikiwemo sisi madiwani hatukufanya utafiti wa kutosha, ila mbaya zaidi wamachinga hawakushirikishwa ni wapi wao wanadhani wangefanya biashara, ili wajipatie kipato chao cha kila siku,” amesema.

Juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuzungumzia hatua wanazochukua kudhibiti wamachinga zimekwama kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa, alipofuatwa ofisini kwake hakuwepo.

Hata hivyo, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmilian Iranghe, amesema mkakati wa jiji hilo ni kutokuwa na wamachinga katikati ya mji na kwa sasa wanajenga masoko makubwa ya kisasa kwa ajili ya wamachinga katika maeneo ya Kilombero na Kwa Morombo ambayo yana watu wengi.

Jijini Dodoma, baadhi ya wafanyabiashara wadogo wamekanusha kukwepa kodi, wakisema pamoja na shughuli hizo, wanalipa ushuru na tozo za Halmashauri ya Jiji kwa mujibu wa sheria.

Wakizungumza na Mwananchi wafanyabiashara hao wamesema awali walikuwa hawatoi tozo wala ushuru kwa sababu hawakuwa na maeneo rasmi ya kufanyia biashara zao, lakini baada ya Serikali kuwaweka kwenye maeneo rasmi wanatoa ushuru uliopangwa na Jiji.

Mwenyekiti wa Soko la Machinga Complex jijini Dodoma, Athumani Ally amekanusha kwamba wanakwepa kulipa kodi, kwani kulingana na aina ya biashara wanazofanya ndani ya soko hilo wanajulikana kuwa ni wafanyabiashara wadogo ambao wanalipa ushuru wa Jiji.

Mfanyabiashara mwingine kutoka soko la Sabasaba, Privas Kulaya amesema hakuna wamachinga anayekwepa kulipa kodi, bali wanalipa ushuru kutokana na ukubwa wa biashara wanazofanya.

“Hivi sasa Serikali imeweka utaratibu mzuri wa wamachinga kufanya biashara, lengo ni kuwainua na wao wawe wafanyabiashara wakubwa, ili waingie kwenye mfumo wa kulipa kodi, hivyo si kweli wanakwepa kulipa kodi kwa sababu hata kipato chao hakitoshi kuingia kwenye walipa kodi wakubwa,” amesema Kulaya.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipoulizwa suala hilo, amesema hawezi kulizungumzia kwa wakati huo kwa kuwa alikuwa uwanja wa ndege akijiandaa na safari.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amesema jiji hilo limefanikiwa kuwaondoa wamachinga waliokuwa wanafanya biashara maeneo yasiyo rasmi kwa asilimia 95 kwa kuwapeleka Soko la Machinga Complex linalobeba wafanya biashara wadogo takribani 3,500 wa kila aina.

Amesema wamebaki wafanyabiashara wachache wanaorudi kwenye maeneo waliyoondolewa kwa kuvizia, lakini huwa wanakabiliana nao kwa kutumia mgambo wa Jiji na wanaendelea kutoa elimu zaidi, ili waondoke kwenye maeneo hayo.

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema kuwapo mfumo unaobebesha watu mzigo wa kodi, kunasababisha ukwepaji wa kodi.

“Kuwafanya kutumia karakana kuuza bidhaa au kupitisha bandari bubu, ni mambo yanayosababishwa na baadhi ya watu kutolipa kodi.

“Nikiona kuna mtu analeta biashara kama yangu akauza bila kodi, anaanza kunifundisha wizi ndiyo hapo wengine watauzia dukani na kuuza bei tofauti ya risiti na isiyokuwa ya risiti, unawafanya watu wakosee kwa sababu mfumo wako hauna haki,” amesema.

Amesema ikiwa watu wengi wanalipa kodi inapunguza mzigo wa kodi, huku akitolea mfano kuwa kama wanalipa asilimia 18 watu milioni moja wakiongezeka kuwa milioni 14 kwanini walisilipe asilimia 7.

Kuhusu ukosefu wa ajira, amesema katika tafsiri wamachinga ni ajira kwa sababu inamuingizia mtu kipato, lakini ikiwa anafanya kazi hiyo kutokana na kukosekana kwa kitu kingine cha kufanya ni tatizo.

“Tujiulize watu wangapi wakipewa kazi nyingine tofauti na wamachinga wataendelea na kazi hiyo? Wanaichagua kwa sababu hana njia nyingine ya kujiingizia kipato,” amesema.

Kwa upande wake, mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude amesema kwa kipindi kirefu sasa ajira katika sekta iliyo rasmi zimekosekana, jambo linalofanya wanaofikia umri wa kuanza kazi kutafuta kazi mbadala.

Amesema vijana wa miaka 21 na kuendelea ni wengi, lakini nafasi za ajira ni chache, hivyo wengi wanasubiri kwa muda mrefu kupata ajira rasmi.

“Ukosefu wa ajira rasmi vinahusiana moja kwa moja na ajira zisizo rasmi, ikiwemo umachinga. Wamachinga ni moja ya njia ya kuishi kwa walio wengi, ni sehemu waliojiegesha wakitegemea mambo yatakaa sawa na watapata kazi au shughuli nyingine za kuwapatia vipato,” amesema Mkude.

Kuhusu kodi, Mkude amesema machinga pia ni namna ya kukwepa ugumu wa kurasimishwa kwa maana ya kuanza kulipa kodi, ushuru na mambo kama hayo.

Imeandikwa na Nasra Abdallah na Aurea Semtowe (Dar), Saddam Sadick (Mbeya), Mgongo Kaitira (Mwanza), Janeth Mushi (Arusha) na Rachel Chibwete (Dodoma).

Related Posts