DIRISHA kubwa la uhamisho linaendelea kushika kasi kwa klabu mbalimbali zikiwamo za Ligi Kuu Bara hasa Simba, Yanga na Azam FC ambazo zimekuwa gumzo zaidi kutokana na sajili za kibabe ambazo zimekuwa zikifanya tangu dirisha hili limefunguliwa.
Kati ya mijadala mikubwa kwa mashabiki kila kona kuanzia kwenye mitandao ya kijamii hadi vijiwe vya kahawa, ni ishu ya kuporana wachezaji kama ilivyokuwa kwa Yanga iliyomnasa Clatous Chama akitokea Simba, uvumi wa Simba kumtaka Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka Azam FC, wakati Azam ikijitafutia chaka la kunasa saini za mastaa wake huko Colombia.
Wakati Azam ikishusha mashine kutoka Colombia, kiraka wa timu hiyo Sospeter Bajana amefunguka ugumu wanaokutana nao kuwasiliana na mastaa hao ambao amekiri kuwa wamekuwa na kitu cha ziada akimtaja beki wao Yeison Fuentes kuwa licha ya kuelewana naye kwa vitendo wamekuwa wakipata nyakati ngumu kwenye kuzungumza.
“Ni wachezaji wengi wametua Azam FC wakitokea nchi hiyo, kitu muhimu ni ishara ya michezo, kwetu sisi tuwapo uwanjani tumekuwa tukielewana vizuri, ukimuangalia beki Fuentes ameingia tayari kwenye mfumo na tunawasiliana vizuri, ishu ni kwenye mazungumzo binafsi, hapo ndio mtihani,” anasema Bajana, ambaye alipata nafasi ya kuchuana na mchezaji ghali wa Manchester United, Sofyan Amrabat wakati Taifa Stars ilipoivaa timu ya taifa ya Morocco.
Mwanaspoti lilipata ufafanuzi zaidi juu ya picha alizopiga na jezi aliyokabidhiwa na mchezaji huyo ambapo alikiri kuwa ametengeneza fremu na kuweka ndani kwake, huku pia akizungumzia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sababu zilizomzuia kutua Simba.
Bajana alikuwa anatajwa kutua Simba katika dirisha kubwa la kuelekea msimu wa 2023-24 lakini baadaye ofa ikayeyuka na kujirudia tena katika dirisha dogo la msimu huo na bado mambo hayakwenda sawa kwa kiungo huyo kwenda Msimbazi.
“Ni kweli Simba walileta ofa mezani wakinihitaji mimi kujiunga nao msimu ulioisha, lakini mambo yalikwenda tofauti kutokana na mazungumzo ya muda mrefu baina yangu na Azam FC, timu ambayo imenilea na kunikuza kisoka,” anasema na kuongeza;
“Simba nilifanya nao mazungumzo lakini bahati ilikuwa upande wa Azam FC ambao waliboresha maslahi na kutimiza vitu vingine vingi ambavyo nilitamani wafanye hivyo nikachagua kubaki kwenye timu hii.”
Bajana anasema mazungumzo kwa pande mbili yalienda vizuri, lakini aliamua kuchagua Azam FC kulingana na ushawishi wao lakini pia alikuwa na uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza kwani tayari alikuwa amejitengenezea ufalme wake huko licha ya kusajiliwa kwa mastaa wengi wa kigeni katika eneo analocheza.
“Azam FC nimekutana na viungo wengi wageni na wazawa, lakini bado nafasi yangu kikosini ipo kwani ubora na nidhamu yangu ndio vinanibeba na nawahakikishia mashabiki wangu kuwa wategemee kuniona uwanjani tena baada ya miezi miwili kuanzia sasa kwani tayari nimerudi na nimeanza mazoezi,” anasema Bajana ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha.
Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ni mmoja wa wachezaji waliocheza kwa mafanikio ndani ya kikosi cha Azam FC wakiipa timu hiyo ubingwa lakini sasa anakipiga Yanga baada ya kuachana na waajiri wake hao lakini bado anatajwa na baadhi ya wachezaji kuwa ni miongopni mwa wachezaji wa kukumbukwa.
“Nimecheza na viungo wengi Azam FC lakini bado nitaendelea kumtaja Sure Boy kuwa ndiye kiungo wangu bora niliyecheza naye na kuufurahia mchezo wa mpira kwasababu alikuwa ananirahisishia mambo mengi uwanjani,” anasema na kuongeza;
“Nilipokuwa nakua naye uwanjani nikipokonya mpira kwa mpinzani na kufanikiwa kumpasia yeye nilikuwa naamini nimepeleka mpira sehemu salama kwasababu ni mchezaji ambaye anajua kukaa na mpira mguuni na kuutunza huku akisambaza pasi za upendo,” anasema.
Bajana anasema kwa kizazi chake ameshuhudia viungo wengi bora lakini kwake Sure Boy atabaki kuwa mchezaji wake kiongozi kwani ndiye aliyemfanya pia kuwa kiungo mzuri kutokana na maelekezo yake walipokuwa wanacheza timu moja huku akikiri kuwa ni mchezaji kiongozi uwanjani.
AZAM ILIMZUIA KUTUA JESHINI
Wakati anatamba katika soka, lakini Bajana yeye anathibitisha kuwa ndoto yake ilikuwa ni kuwa mwanajeshi.
“Sijui kama umri wangu unaruhusu mimi kuwa mwanajeshi kwa sasa lakini ndoto yangu ni siku moja ningechezea timu za jeshi ili kwenda kutafuta nafasi ya kwenda jeshini lakini mambo yamekwenda tofauti,” anasema na kuongeza;
“Nimekaa Azam FC kwa muda mrefu hii ni kwasababu ya maslahi ila matamanio yangu yalikuwa nikitoka hapa basi niende timu za jeshi ili niweze kutimiza ndoto yangu.”
Kwa sasa ukitaja viungo bora kwenye ligi msimu ulioisha huwezi kuacha kumtaja Fei Toto kama anavyothibitisha Bajana ambaye amemtaja mchezaji huyo kuwa ni mwepesi wa kujifunza.
“Fei ameanza kucheza kama kiungo mkabaji, lakini kadri anavyosogea anaendelea kuwa bora kutokana na kuwa mwepesi wa kujifunza na ni mchezaji ambaye kila siku anakuwa tofauti,” anasema na kuongeza;
“Kufanya kazi na mchezaji wa aina yake inaongeza wigo mpana wa kuongeza ubora wako binafsi kwani yeye kila siku anajifunza, namuona mbali, na ni kiungo ambaye nchi yetu imebarikiwa kuwa naye kutokana na umri wake na kuwa na maono ya kufika mbali.”
Bajana anasema Fei kwa kujifunza kila siku, anajitofautisha na wachezaji wengine ambao majina yakikua kidogo wanahisi wamemaliza kila kitu huku akimuombea kutokupata majeraha kwani anaamini ana mchango mkubwa kwa taifa na Azam FC.
Bajana amedumu Azam kwa miaka 11 akianza kuitumikia timu hiyo tangu 2013 hadi sasa, anafunguka siri ya kuendelea kuhudumu kwenye kikosi cha timu hiyo ambacho kimetwaa taji moja tu la Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa ni nidhamu na kuheshimu kazi.
“Nimekaa Azam kwa muda mrefu nafikiri ni uwezo kujituma na nidhamu nafikiri ndio kitu pekee kimenifanya nikae muda mrefu zaidi ndani ya hii timu,” anasema na kuongeza;
“Bado nipo sana kwasababu nina mkataba mrefu, soka ni kama maisha tu, leo upo kesho umekufa haupo, atakuja mtu mwingine ataziba nafasi hivyo kwa upande wangu nafasi niliyoipata naendelea kumuomba Mungu anipe afya njema ili niendelee kuipambania timu hii.”
Wakati mastaa wengi wa ndani ndoto zao zikiwa ni kucheza katika timu za Simba na Yanga kwa upande wa Bajana ni tofauti kwani amethibitisha kuwa kuhudumu kwake kwa muda mrefu ndani ya timu hiyo anatamani kustaafia hapo.
“Ni moja ya ndoto zangu, kama mwenyezi Mungu ataweka heri zake nimalize mpira nikiwa Azam FC. Kila mtu ana matamanio yake, mpira ni biashara kama biashara nyingine mimi ni mchezaji wa Azam FC bado nitaendelea kuheshimu mkataba nilionao,” anasema na kuongeza;
“Kuhusu kubaki hapa ni uamuzi wangu, lakini endapo mkataba wangu ukimalizika na zikaja ofa tukakubaliana na wao wakakubali kile ninachokitaka tunaweza kumalizana, hakuna kinachoshindikana, ila kwa sasa mimi ni mchezaji wa Azam FC bado nina mkataba wa muda mrefu.”
Kila mchezaji ambaye anacheza soka la ushindani huwa ana mchezo wake bora wa kumbukumbu kutokana na aina ya mchezo wenyewe bila kujali matokeo kama ambavyo inathibitishwa na Bajana ambaye amekiri kuwa mechi yake bora ni dhidi ya Morocco akiwa na timu ya taifa.
“Nakumbuka ulikuwa ni mchezo wa kuwania kufuzu ushiriki wa Fainali za Kombe la Dunia 2026 tulipangwa kundi E, mechi yangu bora ni dhidi ya Morocco. Ukiachana na matokeo, huu ni mchezo ambao mimi mwenyewe niliona nimeucheza vizuri na ulikuwa mchezo mkubwa kutokana na kukutana na mastaa wakubwa,” anasema na kuongeza;
“Ukiachana na kichapo cha mabao 2-0 kwenye uwanja wetu wa nyumbani nilicheza vizuri licha ya kukutana na mastaa wengi huku mimi nikikabana na staa wa Manchester United, Sofyan Amrabat. Hii mechi ilikuwa bora na nitaiweka kwenye historia.”
Licha ya kuwa bora na kuonyesha upinzani kwa viungo mbalimbali wa ndani wazawa, Bajana anawataja Kelvin Nashon anayecheza Singida Black Stars na Mtenje Albano wa Dodoma Jiji kuwa ni viungo ambao kuwakaba inahitajika nguvu ya ziada.
“Nimekutana na viungo wengi sana kwasababu nimecheza mechi nyingi kwa misimu niliyoanza kucheza Ligi Kuu Bara lakini nina viungo wangu wawili hao ndio wamekuwa wakinipa shida sana nikikutana nao,” amesema na kuongeza;
“Kuna Nashon na Mtenje, wamekuwa wakinipa shida sana tunapokutana bila kumsahau Jonas Mkude nafikiri sababu kubwa ni aina ya uchezaji wetu huwa tukikutana mambo yanakuwa magumu,” anasema.
Bajana anasema hakuna kazi ngumu kama kucheza na mchezaji wa aina ya nyota hao, hivyo kila anapokutana na viungo hao amekuwa akijiandaa tofauti.
Ligi Kuu Bara ilimalizika Juni, Yanga ikitetea taji, Azam FC nafasi ya pili huku Simba ikimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo. Bajana amefunguka kikosi chake cha msimu huku akijaza mastaa wa tano wa Yanga, watano Azam na mmoja KMC.
“Licha ya makipa wengi wa kigeni msimu huu kifanya vizuri lakini bado nitaenda na Djigui Diarra kwasababu ni kipa ambaye anakupa vitu vingi uwanjani, anajua kuanzisha mashambulizi pia ni mzuri kwenye kucheza na kudaka,” anasema Bajana na kutaja mastaa wake wa kikosi bora cha msimu.
Djigui Diarra, Kouassi Yao, Pascal Msindo, Yeison Fuentes, Dickson Job, Yahya Zayd, Bajana, Maxi Nzengeli, Fei Toto, Waziri Junior, Stephane Aziz Ki na Kipre Jr
Kwenye Ligi Kuu Bara kwa upande wa washambuliaji ni changamoto kupata mastaa ambao wamekuwa na muendelezo wa ubora kama ilivyokuwa kwa John Bocco miaka ya nyuma hii imekuwa changamoto kama anavyothibitisha Bajana kuwa uzalishwaji wa washambuliaji ni janga.
“Kutaja sababu za uzalishwaji wa washambuliaji sio rahisi lakini kwa historia ilivyo Tanzania kuzalisha washambuliaji ni nadra sana lakini kwa viungo siwezi kushangaa kwani wametokea viungo wengi bora na wamekuwa wakifanya vizuri bila kuchagua ni timu gani wanacheza,” anasema na kuongeza;
“Kwa Azam, Simba na Yanga kuna viungo wengi bora lakini huwezi kukosa wachezaji wa aina hiyo timu nyingine, kuna mastaa wengi na wanafanya vizuri maeneo yao lakini kwa upande wa washambuliaji ni janga la taifa,” anasema Bajana, shabiki mkubwa wa msanii wa Bongofleva, Alikiba.
Kila mchezaji anayecheza Ligi Kuu Bara matamanio yake ni kucheza timu ya taifa, Taifa Stars, lakini kwa wale ambao wamekuwa na uhakika wa namba kwenye kikosi hicho matamanio yao ni kucheza mashindano makubwa ya kuipambania timu hiyo kufuzu kuyashiriki kama anavyobainisha Bajana.
“Matamanio yangu yalikuwa ni kucheza fainali za 34 za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) yaliyofanyika nchini Ivory Coast, lakini sikuweza baada ya kusumbuliwa na shida ya nyonga ambayo ilianza kama utani na kocha kunipa muda mwingi wa mapumziko nikiamini nitakaa sawa lakini mambo yalienda tofauti,” anasema na kuongeza;
“Shida ya nyonga ilianza taratibu wala sikuwa na mgongano na mtu yeyote na kama kawaida yetu wachezaji shida kama hizi huwa hatuzipi kipaumbele nikawa naamini ni shida ambayo inaweza kudumu siku mbili tatu na kuondoka na kocha akawa ananipa muda mwingi wa kupumzika kwasababu alikuwa anatambua hii shida, lakini sikujua kama itakuja kuwa kubwa kama ilivyokuwa hadi kufanyiwa upasuaji.”
Bajana anasema siku ya mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania ambao alifunga bao moja na timu yake kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo ndio ulikuwa mwisho wake wa kucheza baada ya kubaini ana shida kubwa na akaamua kuomba mapumziko akiamini anajiweka kwenye nafasi nzuri ya kushiriki Afcon lakini mambo yakawa tofauti.
“Niliomba mapumziko ya wiki tatu na nakumbuka ligi ilikuwa inaendelea, lakini kocha Youssouph Dabo aliniruhusu kwasababu alikuwa anafahamu matamanio yangu ya kucheza Afcon, hivyo nilijua nikipata mapumziko nitakaa sawa, lakini haikuwa bahati kwani ilinilazimu kwenda kufanyiwa upasuaji,” anasema.
Tanzania ipo kwenye mchakato wa kuwania kufuzu ushiriki wa Kombe la Dunia 2026 na sasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya Morocco. Bajana anasema licha ya kwamba timu inayofuzu ni moja tu na Morocco ndiyo inayopewa nafasi kubwa, bado haiondolei Taifa Stars uwezekano wa kufuzu.
“Bado kuna nafasi ukiangalia pia kuna mechi nyingi na hakuna timu iliyofuzu, tuna faida ya kucheza mechi nyumbani, nafikiri tuendelee kushirikiana na kuamini kile ambacho Mungu amekipanga kiweze kuwa upande wetu,” anasema.
Wakati wadau wa soka wakiimba kuliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupunguza idadi ya mastaa wa kigeni ili kuunda timu bora na ya ushindani kwa wazawa kupata nafasi ya kucheza kwenye timu zao, Bajana amefunguka faida ya wachezaji wa kigeni kwenye Ligi Kuu Bara.
“Wana faida kubwa kwasababu wanatupa changamoto ya kujiweka fiti kupambana nao ili kujihakikishia nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, hakuna mchezaji wa kigeni ambaye amekuja kuchukua nafasi ya mtu, ubora wake ndio unamnyima nafasi mchezaji mzawa,” anasema na kuongeza;
“Mimi nafikiri kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kupamba kujiweka kwenye nafasi na sio kusingizia uwepo wa wageni, kama ana uwezo anatakiwa kumshawishi kocha mazoezini ili apangwe yeye na sio mgeni hakuna kocha ambaye anaweza kumuacha mchezaji bora nje ambaye anaweza kumpa matokeo na kumtumia asiye na uwezo.”
Bajana anasema mgeni akiwa bora anamfanya na yeye apambane ili awe bora aweze kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kqwanza huku akikiri kuwa uwepo wao unawapa morali ya kujipambania.
“TFF ndio wanaongoza mpira wanajua nini wanakifanya siwezi kuwashauri kwa lolote juu ya uwepo wa makipa wa kigeni Ligi Kuu Bara na ufinyu wa wazawa kupata nafasi ya kucheza, ninachoweza kuwashauri ni wachezaji wenzangu kuhakikisha wanapambania nafasi ya kucheza ili kujihakikishia ubora utakaowafanya waite Stars,” anasema.
“Ili Stars iwe na kikosi bora ni lazima wachezaji wajihakikishie nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kwenye timu zao hivyo kwa makipa wazawa waliopo ambao ni wengi kuliko wageni wanatakiwa kupambana zaidi ili kuja kuijenga stars ya ushindani.”
Akipambwa na sifa ya kasi uwanjani na mgumu kupoteza mpira, Bajana anathibitisha kuwa licha ya ugumu wake uwanjani kwake ishu ya kula sio kipaumbele na ni mvivu sana kula.
“Kwenye ishu ya kula sio sana mimi ni mvivu, nakula kwa sababu ni lazima ili uishi lakini sio kipaumbele. Ninachopenda ni mazoezi na kupata muda mwingi wa kupumzika.”