SINGIDA Black Stars, iko mbioni kukamilisha uhamisho wa kiungo, Josaphat Arthur Bada kutokea kikosi cha ASEC Mimosas.
Nyota huyo wa Ivory Coast, tayari amefanya mawasiliano na viongozi wa Singida ili asaini na dili hilo likitiki, atakuwa ni nyota wa pili kutokea ASEC kusajiliwa na timu hiyo baada ya beki wa kati, Anthony Tra Bi Tra.
MABOSI wa Pamba wamewasiliana na wakala anayemsimamia kiungo wa Inter Club de Brazzaville Mcongomani, Inno Jospin Loemba.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Congo Brazzaville, inaelezwa ameridhia kujiunga na Pamba kwa mashindano mbalimbali msimu ujao na kilichobaki ni Pamba kumalizana na waajiri wanaommiliki.
TIMU ya Mashujaa ya Kigoma inakaribia kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa kiungo wa Namungo, Khamis Khalifa ‘Nyenye’.
Nyota huyo inaelezwa hayupo tayari kusalia Namungo kwa msimu ujao jambo lililowafanya mabosi wa Mashujaa kuzungumza naye ili akaichezee timu hiyo, huku ikielezwa ishu ya maslahi haiwezi kuwa kikwazo katika kuinasa huduma yake.
SINGIDA Black Stars iko mbioni kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa winga wa kikosi cha Geita Gold, Edmund John.
Nyota huyo ambaye ni mchezaji huru kwa sasa baada ya Geita kushuka daraja, inaelezwa anakaribia kusaini kuichezea timu hiyo msimu ujao na kuifanya Singida kushinda vita na klabu mbalimbali zilizomuhitaji zikiwemo za Pamba na Coastal Union.
BEKI wa kati wa Singida BS, Mukrim Mussa Abdallah, ameomba kutolewa kwa mkopo kwenda timu nyingine itakayompa nafasi ya kucheza.
Nyota huyo aliyewahi kukipiga Fountain Gate na JKU ya Zanzibar, inaelezwa ameomba kuondoka ili kulinda kipaji chake huku klabu mbalimbali zikimhitaji ikiwemo Coastal Union.
PAMBA Jiji ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa beki wa kulia wa Mbuni ya jijini Arusha, Yunus Lema.
Nyota huyo anayefananishwa Shomari Kapombe, inaelezwa ameivutia Pamba kwa umri mdogo na uwezo mkubwa alionao, ni chachu ya kukiletea mafanikio kikosi hicho kilichodhamiria kuleta ushindani.
TANZANIA Prisons inataka kumrejesha aliyekuwa beki wa kati wa klabu hiyo, Vedastus Mwihambi kutoka Singida Black Stars.
Nyota huyo aliyewahi kuichezea Mtibwa Sugar, inaelezwa hayupo katika mipango ya kocha mkuu wa kikosi hicho Mbelgiji, Patrick Aussems, hivyo kuna uwezekano mkubwa akaondoka kikosini.