Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amefika katika Soko la Simu2000, Ubungo kuzungumza na wafanyabiashara waliopo kwenye mgomo.
Mgomo na maandamano ya wafanyabiashara ulioanza asubuhi ya leo Jumatatu, Julai 8, 2024, wakishinikiza Manispaa ya Ubungo ifute uamuzi wake wa kuipatia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) eneo hilo, ili ijenge karakana zake.
Kabla ya Chalamila kufika eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko alifika, lakini hakupewa nafasi ya kuzungumza na wafanyabiashara hao na kumtaka aondoke kwa kile walichoeleza hawana imani naye kwa kuwa walishamwita kwa takriban mara tatu wamweleze changamoto yao, lakini aliwapuuza.
Bomboko alisogea kutoka eneo alilokuwepo na kwenda mbali kidogo na eneo hilo, kisha kuzungumza na waandishi wa habari.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari, Bomboko amesema mazungumzo kati ya Manispaa na Dart kuhusu eneo hilo hayajakamilika.
Kwa sababu hiyo, amesema hakuna kiongozi aliyekubali kuikabidhi Dart eneo hilo, bali ni maneno tu.
Bomboko anasema hayo, wakati katika kikao cha Julai 4, 2024 cha Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo, Meya wa Ubungo alisema kikao hicho na manispaa kwa ujumla imeridhia Dart ikabidhiwe eneo hilo.
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maboresho ya Soko, Mussa Ndile amesema kinachowashangaza ni uamuzi huo kufanyika bila wafanyabiashara kushirikishwa.
Amesisitiza hadi wanafika katika eneo hilo, walishahamishwa mara kadhaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo barabarani tangu mwaka 2014.
“Tuliwekeza fedha zetu kutengeneza vibanda na kuanzisha biashara, leo hii tunaona dalili ya kufuzwa hapa,” amesema.
Hata hivyo, amesema kuna maeneo mengi ambayo Dart ingeweza kupewa ndani ya manispaa hiyo.
“Hatutaki kuchezewa kwenye eneo hili, tunaomba mkuu wa mkoa utoe maelekezo kwenye baadhi ya maeneo Mamlaka ya Udhubiti wa Usafiri Ardhini (Latra),” amesema.
Katika hotuba yake kwa wafanyabiashara, Chalamila amekiri uwepo wa mpango wa eneo hilo kukabidhiwa kwa Dart.
Pamoja na hilo, amesema wafanyabiashara walipaswa kushirikishwa kabla ya uamuzi wowote.
Kwa anavyofahamu, amesema alishaielekeza Manispaa ya Ubungo ikimalizane na Dart, kisha suala hilo lifikishwe ofisini kwake kwa ajili ya kutafakariwa.
“Hili linalosemwa kwa asilimia 100 lipo, lisemwalo lipo ndugu zangu, lakini bado halijafika ofisini kwangu, lakini mlipaswa kushirikishwa,” amesema.
Chalamila amesema tayari wafanyabiashara hao wameshahamishwa sana na sasa imetosha kuendelea kunyanyaswa.
Katika kulimaliza hilo, amesema ndani ya wiki hii atazungumza na pande zote zinazolalamikiwa, kisha Jumamosi (Julai 13), atakutana na wafanyabiashara kwa ajili ya kuzungumza nao.
“Leo ni Jumatatu naomba mundelee na kazi zenu hadi Jumamosi nitakuja, nataka kumsikiliza mtu wa Dart na wengine wote, kisha kwa kuwa sio siri nikija nitakuwa nao, ili wanieleze mbele yenu,” amesema.
Baada ya maelezo ya Chalamila, wafanyabiashara hao wamesema siku hiyo hawatafungua maduka kwa ajili ya kuisikiliza Serikali na iwapo itaamua jambo lililo nje ya maslahi yao hawatavumilia, watalazimika kutumia mbinu yoyote, ili waonane na Rais Samia Suluhu Hassan.
Hadi Mwananchi inaondoka eneo hilo saa 5 asubuhi, maduka na biashara mbalimbali zikianza kufunguliwa.