#Huduma za shule na hospitali zafikika kiurahisi
Na. Erick Mwanakulya, Berega, Kilosa.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imekamilisha ujenzi wa daraja la Berega lililopo katika barabara ya Berega – Dumbalume lenye urefu wa mita 140 na upana mita 11 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Kukamilika kwa daraja hilo limeweza kuunganisha Wilaya ya Kilosa, Gairo, Kiteto na Kilindi na hivyo kuondoa kero ya miaka mingi iliyokuwa ikiwakabili wananchi katika shughuli za usafiri na usafirishaji ikiwemo kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilosa Mhandisi Winston Munyanga alisema ujenzi wa daraja la Berega umekamilika kwa asilimia 100 pamoja na maboresho ya barabara ya Berega – Dumbalume yenye urefu wa Km 7 ambayo yamegharimu shilingi Bilioni 7 na kuondoa kero ambayo wananchi wa Wilaya hiyo na zile za jirani walikuwa wanazipata.
”Kwasasa ujenzi wa daraja la Berega umekamilika na tumefanikiwa kuunganisha Wilaya ya Kiteto, Gairo, Kilosa na Kilindi pamoja na kurahisisha huduma za kijamii na kiuchumi kwa kuzifikia kwa urahisi hasa shule pamoja na hospitali zilizopo ng’ambo ya daraja hilo”, alisema Mhandisi Winston.
Pia, Mhandisi Winston ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ongozeko la bajeti kwa Wakala wilayani Kilosa ambayo imewezesha kutekeleza mradi huo mkubwa wa ujenzi wa daraja la Berega ambalo limekamilika na kuwawezesha wananchi kutumia daraja hilo katika kipindi chote cha mwaka, pamoja na kusafirisha mazao yao na kufikisha sokoni kwa wakati.
Naye, Diwani wa Kata ya Berega, Mhe. Filemoni Maube alisema wanaishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja la Berega kwani hapo awali kipindi cha masika wananchi wa Kata hiyo walikuwa wanapata tabu katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi na iliwalazimu kusubiri maji yapungue ndipo waanze kupita.
”Tunaishukuru sana Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja ili kwa sababu sasa tuna uhakika wa kupita hapa katika vipindi vyote tofauti na hapo awali, wanafunzi wataweza kufika shuleni, wagonjwa watafika hosptalini pamoja na kusafirisha mazao yetu kwa urahisi”, alisema Mhe. Filemoni
Aidha, Bw. Gideon Mshala, Mkazi wa Kijiji cha Berega ameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ambalo limewasaidia wananchi wa Kata ya Berega, Kiegeya na maeneo jirani kuvuka kwa urahisi na kuzifikia huduma za kijamii tofauti na hapo awali ambapo daraja lilikuwa limekatika.
”Tunaishukuru sana Serikali kwa kukamilisha daraja hili, tulikuwa tunapata tabu katika kuzifikia huduma za kijamii pamoja na kusafirisha mazao yetu kama mbaazi, miwa, mahindi na viazi kwa kuwa wakazi wengi wa huku ni wakulima hivyo tulivyokosa huduma ya daraja tulipata tabu katika shughuli zetu za usafiri na usafirishaji”, alisema Gideon.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA unaendelea kutekeleza miradi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wanafika kusiko fikika.
Muonekano wa daraja la Berega lenye urefu wa mita 140, upana mita 11 katika barabara ya Berega – Dumbalume linalounganisha Wilaya ya Kilosa, Kiteto, Gairo na Kilindi likiwa limekamilika lililopo Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.