Na Farida Ramadhani, WF – IKUNGI, SINGIDA.
Vijana
wametakiwa kuwasilisha malalamiko yao kuhusu huduma za fedha katika
mamlaka husika ili kupata suluhu haraka pamoja na kukabiliana na
changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Fedha ikiwemo utapeli,
udanganyifu na mikopo yenye riba kubwa (mikopo umiza/ kausha damu).
Mamlaka
wanazotakiwa kuwasilisha malalamiko hayo ni Benki Kuu ya Tanzania,
Mamlaka ya Dhamana ya Masoko na Mitaji, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima na
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wito huo umetolewa Ikungi mkoani Singida
na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini
kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, baada ya kutoa elimu ya
fedha katika Kongamano la Vijana wa Wilaya hiyo katika mkesha wa Mwenge
wa Uhuru.
Bi. Mjema alisema Serikali imeweka kanuni na miongozo
ili malalamiko hayo yaweze kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa
Sheria za Fedha.
“Waende Benki Kuu kama malalamiko yao yanahusu
masuala ya benki, kama yanahusu masuala ya dhamana ya masoko na mitaji
basi waende Mamlaka ya Dhamana ya Masoko na Mitaji, kama yanahusu bima
yapelekwe Mamlaka ya Usimamizi wa Bima na yale yote yanahusiana na mafao
ya uzeeni waende Ofisi ya Waziri Mkuu”, alifafanua Bi. Mjema.
Alisema
katika Kongamano hilo Wizara ya Fedha imetoa elimu ya fedha kwa vijana
kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, elimu ya mikopo, uwekaji wa akiba,
uwekezaji, maisha baada ya kustaafu, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha na
namna ambavyo Serikali imeweka miongozo mbalimbali ya kumlinda mtumiaji
wa huduma ndogo za fedha kupitia Kanuni za Kumlinda Mtumiaji.
“Tumewaelimisha
vijana kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika Sekta ya Fedha
ikiwemo kuwekeza katika Masoko ya Mitaji, mifuko ya uwekezaji wa pamoja,
upatikanaji wa mikopo katika benki na taasisi za fedha pamoja na huduma
ndogo za fedha”, alibainisha Bi. Mjema.
Alisema lengo la kutoa
elimu hiyo ni kuwawezesha wananchi hususan vijana kutambua fursa
mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya fedha ili waweze kujenga
uchumi wao, wa familia na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Naye
Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bw.
Peter Musa alisema wameona ni vema kuialika Wizara ya Fedha kutoa elimu
ya Fedha kwa kuwa kwa sasa masuala ya fedha yamekuwa changamoto hususan
kwa vijana.
Alisema pamoja na kuwa Wizara imekuwa ikifanya juhudi
kubwa za kusambaza elimu hiyo nchini lakini waliona mkusanyiko wa
Jukwaa la Vijana katika shughuli za Mwenge ni sehemu muafaka kwa ajili
ya kutoa elimu hiyo.
Kwa upande wa vijana walioshiri Kongamano
hilo, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa elimu hiyo muhimu kwa
maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Bw. Rajabu Kulandera miongoni
mwa washiriki ambaye alisema kutokuelewa vizuri sekta ya fedha kumekuwa
kukiwakosesha haki wananchi wengi hususan vijana ambao mara nyingi
wanajiona kuwa kundi lililosahaulika lakini baada ya elimu hiyo ameelewa
haki na wajibu wao kama watumiaji wa huduma za fedha , umuhimu wa
kuweka akiba, kutumia mifumo rasmi ya fedha pamoja na namna ya
kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo.
“Elimu
hii imetufumbua macho, pamoja na mambo mengine suala la mikopo ni kaa la
moto kwetu, lakini baada ya elimu hii tumeelewa umuhimu wa kusoma
mikataba kabla ya kukopa ili kujua kama mkopo ni kausha damu au ni wa
afya”, alisema Bw. Kulandera.
Aliiomba Serikali kupitia Wizara ya
Fedha kuendelea kutoa elimu muhimu kwa wananchi wa hali ya chini
hususani vijijini ili kuwanusuru na mateso wanayoyapata yanayotokana na
kutokujua mifumo rasmi pamoja na haki zao hali inayowafanya waangukie
katika kuchukua mikopo holela yenye masharti magumu.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa
Uhuru, Bw. Godfrey Mnzava akimsikiliza taarifa ya elimu iliyotolewa
katika Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bi.
Haika Massawe katika Kongamano la Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ikungi katika mkesha wa Mwenge wa Uhuru. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa
Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini kutoka Wizara ya Fedha,
Bi. Dionesia Mjema na Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro
ambao walitoa walitoa elimu fedha katika Kongamano hilo.
Kamishna Msaidizi wa Idara ya
Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini kutoka Wizara ya Fedha, Bi.
Dionesia Mjema, akitoa elimu ya fedha kwa vijana katika Kongamano la
Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika mkesha wa Mwenge wa
Uhuru.
Kamishna Msaidizi wa Idara ya
Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini kutoka Wizara ya Fedha, Bi.
Dionesia Mjema na Afisa Usimamizi wa Fedha, wa Wizara hiyo, Bi.
Elizabeth Mnzava wakichukua maswali na maoni mbalimbali yaliyokuwa
yakitolewa na washiriki wa Kongamano la Vijana wa Halmashauri ya Wilaya
ya Ikungi katika mkesha wa Mwenge wa Uhuru.
Sehemu ya washiriki wa
Kongamano la Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, wakifuatilia kwa
karibu mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika elimu ya fedha,
katika mkesha wa Mwenge wa Uhuru wilayani humo.
Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha,
Bw. Salim Kimaro akifafanua jambo wakati wa utoaji elimu ya fedha kwa
vijana katika Kongamano la Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
katika mkesha wa Mwenge wa Uhuru.
Mshiriki wa Kongamano la Vijana
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bw. Rajabu Kulandera akichangia
mada baada ya Wizara ya Fedha kutoa elimu ya fedha katika mkesha wa
Mwenge wa Uhuru wilayani hapo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Fedha)