Hofu makaburi yakigeuzwa ‘gheto’ Mbeya

Mbeya. Hofu imezuka maeneo jirani na makaburi ya Sabasaba jijini Mbeya, baada ya watu wasiojulikana kuyageuza sehemu ya kulala huku wakijifunika nguo nyeupe mithili ya sanda.

Kwa mujibu wa wakazi wa maeneo hayo, si ajabu kukuta nazi zimevunjwa, vyungu na wakati mwingine watu kuogeshana hadharani katika njiapanda iliyopo karibu na makaburi hayo.

Mwananchi kwa takriban wiki tatu limeshuhudia uwepo wa vitu mbalimbali zikiwemo nguo na viatu karibu na makaburi hayo.

Kutokana na hofu wanayopata wananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema atamwelekeza Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), kutuma kikosi kazi kufanya doria kisha wampatie mrejesho.

Si mara ya kwanza mikasa kama hii kuripotiwa katika maeneo ya makaburi, kuwa waganga, watambikaji na wengine watafuta bahati huyatumia maeneo hayo, bila kusahau wahalifu.

Mwaka 2017, gazeti hili liliripoti kuhusu hali kama hiyo katika makaburi ya Mbuyuni, Tandika wilayani Temeke, ambako mwandishi alikuta familia ikilinda eneo lao lisigeuzwe kaburi kwa kukayaa mauzauza kama hayo.

Mbali na majirani hapo pia kwenye eneo la makaburi ya Kwa Kindale, Mtoni Mtongani nako kulikuwa na malalamiko kama hayo na kwingineko makaburi yakigeuzwa ‘gesti’ kufanyia vitendo vya ngono.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya wakazi wa maeneo ya karibu na makaburi hayo, walioeleza kuwa kwa sehemu kubwa watu hao ni wahalifu na wayatumia makaburi hayo kama sehemu ya kujificha.

Kutokana na mazingira hayo, wamesema ni vigumu kwa ndugu wa marehemu waliozikwa kwenye makaburi hayo kwenda kuyafanyia usafi.

“Tunashuhudia mambo ya ajabu licha ya watu kuweka hifadhi, wapo wengine wanakuja kufanya matambiko ya kishirikina kwa kufukia vichwa vya mbuzi na kuku kwenye mabakuri yaliyojengewa pembeni au ambayo hayajajengewa kabisa,” amesema mmoja wa wananchi kwa sharti la kutotajwa jina.

Mwananchi mwingine karibu na maeneo hayo, amesema watu hulala makaburini na wengine huvunja vyungu nyakati za usiku mnene.

“Ukiwa mtu wa wasiwasi huwezi kuvumilia mambo tunayoona, kama Polisi wanafanya doria muda huo ndio mzuri hawatakosa watu, watumie mbinu za kiintelejensia kwani wapo wanaojibanza huwezi kudhania kama kuna watu wamelala,” amesema.

Baadhi ya makaburi yaliyopo eneo ya Sabasaba jijini Mbeya. Picha na Hawa Mathias

Kinachodaiwa kusababisha watu hao kugeuza makaburi hayo malazi yao, ni kuwa wahusika hawakubaliki katika jamii, hivyo wameamua kuishi kwenye makaburi hayo.

“Wapo kama wawili ni sugu, wameishi ndani ya makaburi kwa zaidi ya miaka 25, niliwafukuza lakini wanaendelea kukaa humo kwa vificho, kuna wakati niliwategea niwakamate ili wachukuliwe hatua, waliponiona walikimbia na kuacha vitu vya thamani kama nguo ambazo huenda waliziiba mahali, nilizichoma moto,” amesema Joseph Mwambinje mmoja wa wakazi jirani na makaburi hayo.

Kwa upande wake, Kijana anayelala kwenye makaburi hayo, Amani Augustino (21) amesema analazimika kuishi eneo hilo kutokana na kukosa sehemu ya kulala.

Amesema anaishi maisha duni na hana ndugu wa kumsaidia.

Awali, anasema alikuwa analala kwenye vibanda vilivyojengwa Stendi ya Mbeya, lakini doria zinazofanywa na Polisi mara kwa mara zimemuhamisha na ameamua kuhamia makaburini hapo.

“Mimi nimetokea Mkoa wa Rukwa nilikuja kusaka maisha, awali nilikuwa nalala kituo cha mabasi ya mikoani, lakini baada ya kujenga uzio na kuimarisha ulinzi nimekuja kuweka hifadhi hapa, tupo wengi, wengine ni kweli wahalifu ambao hufika usiku wa manane na kutoka alfajiri sana,” amesimulia kijana huyo.

Kijana aliyejitambulisha kwa jina la Alex akionyesha sehemu ya ambayo watu hao uhifadhi mahitaji yao zikiwepo nguo na viatu kwenye moja ya kaburi. Picha na Hawa Mathias

Mkazi wa sabasaba anayejihusisha na shughuli za kukata majani ya mifugo, Alex Asajile amesema idadi kubwa ya waliofanya makaburi kuwa hifadhi yao ni wahalifu.

“Hawa jamaa sio watu wa kawaida kwa sababu sehemu ya makaburi sio rahisi mtu kwenda kulala pasipo hofu yoyote na kama sio wahalifu basi ni masuala ya imani za kishirikina,” amesema Asajile.

Amesema ili kurejesha amani kwa jamii, Jeshi la Polisi linapaswa kuingilia kati kwa kufanya doria za mara kwa mara na watakaobainika wahojiwe kwa kuwa si wenyeji wa maeneo hayo.

Sekela Joel, mkazi wa Forest amesema amewahi kunusurika kubakwa alfaji moja alipokuwa akienda Hospitali ya Rufaa Kanda kumuona mgonjwa.

“Nilipita eneo la jirani na makaburi hayo, lengo nipite sehemu kuna daraja linaunganisha na Kata ya Jakalanda na Barabara ya Mbalizi, ghafla nilikuta vijana wawili wameziba sura wakinifuata nyuma, nilipoona siwaelewi, nilitimua mbio ndio kunusurika lakini walifanikiwa kuvuta kikapu kilicho kuwa na mahitaji ya mgonjwa, huku wasema nina bahati wangenibaka,” anasimulia.

Happy Fredy, mmoja wa waliozika ndgu zao hapo, amesema mazingira ya eneo hilo kwa sasa si salama kwa sababu wanashindwa kuwahi alfajiri kusafisha makaburi ,kutokana na watu hao wanaolala eneo hilo.

“Kiuhalisia kama hujawahi kuona unaweza kukimbia, kwani ni mithiri ya mtu aliyehifadhiwa kwenye sanda na ukiwaita wanaitika kwa sauti nzito kwa madai wako nyumbani kwao, hawahitaji kelele,” anasema.

Happy ameiomba Serikali kuona umuhimu wa kujenga uzio katika makaburi ili kuzuia watu mbalimbali kulitumia eneo hilo kama maficho yao.

“Hapa sio kulala tu, hata imani za kishirikina zinafanywa sana na jamii yenye imani haba kwa kuzika kuku wazima ardhini ambao zaidi ya mara mbili nimeshuhudia,” amesema.

Akizungumza kwa masharti ya kutoandikwa jina, mmoja wa viongozi eneo hilo alisema matukio ya watu kulala yaliwahi kuripotiwa na hatua zilizochukuliwa ikiwemo kufanya doria na kuwabaini.

“Hayo yaliwahi kutokea tulifuatilia lakini tuliowabaini baada ya kuwahoji walikuwa hawana sababu za msingi, kimsingi suala hilo kama limejirudia tutalifanyia kazi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na matukio hayo hususan vijana kulala makaburini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema amelipokea suala hilo na atalifanyia kazi.

“Siwezi kujibu moja kwa moja kama nalielewa muda huu, nitamwagiza Mkuu wa Upelekezi Wilaya (OCD) kapange kikosi kazi kufanya doria kwenye maeneo ya makaburi ili kuwabaini watu hao,” amesema.

Kuzaga amewataka viongozi wa ngazi za kata na vijiji, kuhamasisha doria za polisi jamii na ulinzi shirikishi ili kukabiliana na matukio ya uhalifu katika maeneo yasiyo salama kwa jamii, hususan kwenye makaburi.

Related Posts