Mawaziri wa mambo ya nje na wasaidizi wao kutoka nchi nane zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanakutana Zanzibar wakati huu wa changamoto nyingi za kisiasa, kijamii na kiuchumi duniani na kwenye kanda hiyo. Mkutano huo unafanyika wakati Kenya moja ya nchi wanachama imeshuhudia wimbi kubwa la maandamano ya vijana dhidi ya serikali.
Naibu Waziri Mkuu na waziri wa Afrika Mashariki wa Uganda, Rebecca Kadaga, na Waziri Kiongozi wa serikali ya Kenya Musalia Mudavadi ni miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ambao ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na marais wa nchi hizo kwa mawaziri hao wakutane kwa faragha kutafuta namna bora ya kuimarisha amani, usalama na kuharakisha muungano wa kisiasa baada ya mafanikio kuanza kuonekana katika forodha na Uhuru wa kibiashara.
Rais William Ruto wa Kenya aahidi mabadiliko baada ya maandamano
Wakizungumza kando na mkutano huo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Veronica Mueni Nduva amesema mkutano huo ni wa kuulizana na kuelezana ukweli.
“Mawasiliano yetu yatakuwa ni ya uwazi na tunayaweka mambo yote mezani ikiwemo vipi tunavyoweza kurekebisha mambo ambayo hayaendi vizuri na vipi tunaweza kuuboresha umoja ambao ni thabiti, mambo ambayo yameletwa katika mkutano wa mawaziri na mkutano wa marais wanaoziwakilisha jumuiya, lakini ubunifu wa mkutano huu ni tofauti ambao utakuwa wa uwazi na kuangaliana macho kwa macho ana kwa ana na kuulizana masuali magumu,” alisema Bi Nduva.
Wakitoa salaamu zao wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa siku tatu, mawaziri kutoka Burundi, Uganda, DRC, Somalia, na Kenya wamesema kuwa amani, usalama, na muungano wa kisiasa ni mambo yanayohitaji kuwekewa mikakati ili kufikia mafanikio.
Suala la vita vya Mashariki ya Kongo pia lipo katika ajaenda ya mazungumzo
Mkutano huo wa faragha utawapa nafasi mawaziri hao wa kuzungumza kwa uwazi zaidi kama anavyoeleza Waziri wa mambo ya nchi na ushirikiano wa Afrika Mashariki Tanzania, January Makamba.
“Kwa sababu masuala haya ni nyeti yanahitaji utulivu yanahitaji busara na yanahitaji hekima katika kutajadili na ndio maana tukaja kujificha huku Zanzibar ili tupate kuyajadili,” alisema Makamba.
Mbali ya masuala ya jumla, mkutano huo umeshuhudia pia mataifa yaliyotumbukia kwenye uhasama yakikaa mezani kujaribu kutafuta suluhu. Waziri wa mambo ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe alikutana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Kongo Gracia Yamba kuzungumzia mvutano kati ya Kongo na Rwanda. Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa kijamii wa X Ndihungirehe amesema mazungumzo na mwenzake wa Kongo yalifanyika katika hali ya nia njema na yalikuwa ya uwazi.
UN: Vikosi vya Rwanda vyasaidiana na M23 kupigana Kongo
Hata hivyo hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa juu ya kile kilichoafikiwa. Kongo na Rwanda zimo kwenye mvutano unaotanuka kutokana serikali ya Kinshasa kuutuhumu utawala mjini Kigali kuchochea machafuko mashariki mwa Kongo, Tuhuma ambazo Rwanda mara kadhaa imezikanusha. Mkutano huo ambao umewashirikisha mawaziri wote wan chi hizo unatarajiwa kumalizika leo jioni na kutoka na maazimio mahsusi ambayo yanatazamiwa kupelekwa kwa maraisi wote wa Afrika Mashariki.
Mwandishi: Salma Said DW Zanzibar