SIMBA Queens msimu ujao haitaendelea na kipa wa timu hiyo, Zubeda Mgunda baada ya kumaliza mkataba mwishoni mwa msimu huu.
Kipa huyo alisajiliwa na Simba mwaka 2018 akidumu kikosini hapo kwa takribani misimu sita na kuiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) mara nne.
Inaelezwa sababu ya kuondolewa kikosini hapo ni kutokana na kushindwa kupata namba mbele ya kipa namba moja, Mkenya Carolyne Rufaa.
Ujio wa Rufaa Simba mwaka 2022 umekuwa ukimpa wakati mgumu wa kupata namba Mgunda ambaye msimu uliopita hakucheza mchezo hata mmoja wa Ligi.
Mmoja wa viongozi wa Simba (jina tunalo) ameiambia Mwanaspoti kuwa klabu hiyo itaachana na wachezaji sita ikiwemo kipa ili kupisha nafasi ya wachezaji wengine.
“Sio Mgunda tu wapo karibu sita kocha amebainisha kuwa hana mpango nao hivyo tumeachana naye na tumeamua tubaki na makipa wawili, Carolyne na Gelwa Yona,” amesema kiongozi huyo.
“Mgunda ni kipa mzuri nafikiri miaka ya 2021 watu walimuona uwezo wake lakini ameshindwa kuendeleza kiwango chake hivyo tutaachana naye.”