KATIKA kujenga kikosi bora cha ushindani, uongozi wa Coastal Union upo kwenye hatua za mwisho kunasa saini ya kiungo raia wa Uganda, Gift Abubakar Ali kutoka Proline FC.
Kiungo huyo ambaye amewahi kucheza KCCA ya Uganda na Uganda Police, yupo kwenye hatua za mwisho za kusaini mkataba na Coastal.
PAMBA Jiji ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa beki wa kulia wa Mbuni ya jijini Arusha, Yunus Lema.
Nyota huyo anayefananishwa Shomari Kapombe, inaelezwa ameivutia Pamba kwa umri mdogo na uwezo mkubwa aliokuwa nao, ni chachu ya kukiletea mafanikio kikosi hicho kilichodhamiria kuleta ushindani.
NAHODHA Msaidizi wa Alliance Girls, Elizabeth John (16) anahusishwa kujiunga na Ceasiaa Queens ya mkoani Iringa. Mchezaji huyo anayemudu kucheza nafasi ya kiungo, inaelezwa kama taratibu za kimkataba zitakwenda vizuri msimu ujao atakuwa sehemu ya kikosi hicho.
INAELEZWA kwamba Bunda Queens imevutiwa na kiwango cha winga Mkenya Nelly Kache ambaye amemaliza mkataba ndani ya Alliance Girls. Awali Simba Queens na Yanga Princess zilikuwa timu za kwanza kuanza mazungumzo na winga huyo kabla ya Bunda Queens kuingilia kati dili hilo.
YANGA Princess imeanza mazungumzo na winga wa JKT Queens, Alia Fikiri kwa ajili ya kuziba pengo la Precious Christopher aliyejiunga na watani zao, Simba Queens.Inaelezwa Yanga Princess imevutiwa na nyota huyo kutokana na kiwango alichoonyesha lich ya umri alionao.
KIUNGO Mshambuliaji wa Fountain Gate Princess, Amina Ramadhan ameziingiza vitani timu mbili za JKT Queens na Yanga Princess ambazo zinawania saini yake. Awali kiungo huyo alikuwa akihusishwa kujiunga na Yanga Princess ambapo kwa taarifa tulizonazo ni kuwa JKT Queens nayo imeingilia kati dili hilo.
GEITA Gold iliyoshuka daraja msimu uliopita imeanza mazungumzo na mshambuliaji, Athuman Masumbuko ‘Makambo’ kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi ya Championship. Nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar U-20 na Mashujaa, inaelezwa kama mambo yatakuwa sawa anaweza kujiunga nao.