Serikali yaagiza mabasi kumaliza changamoto usafiri wa mwendokasi

Dar es Salaam. Ili kukabiliana na changamoto ya usafiri kutoka Mbezi hadi mjini kati, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Serikali imeagiza mabasi yaendayo haraka yatakayotoa huduma katika barabara hiyo.

Chalamila ameeleza hayo leo Jumatatu Julai 8, 2024  katika mkutano wa hadhara wa Katibu wa Itikadi, Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Liwiti, jijini Dar es Salaam.

Kauli ya Chalamila inakuja wiki kadhaa tangu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), itangaze mpango wa kutoa ruhusa kwa daladala 20 kuongeza nguvu ya huduma katika barabara hiyo.

Itakumbukwa baada ya usafiri wa mabasi hayo kuanza mwaka 2016, Serikali ilisitisha safari za daladala katika barabara hiyo kwenda mjini kati, badala yake huduma zilikuwa zikitolewa na mabasi yaendayo haraka.

Uchache wa mabasi hayo umesababisha msongamano wa abiria vituoni na wengine kulazimika kugeuza na magari, ili angalau wapate nafasi ya kusimama.

Katika maelezo yake, Chalamila amesema, “leo hii wananchi wanalalamika njia ya  Kimara mabasi machache, nitumie hadhara hii kuwaambia Serikali imeagiza mabasi kadhaa, ili kutatua changamoto hizo,” amesema Chalamila.

Mbali na hilo, Chalamila amemuondoa hofu mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli kuhusu changamoto za miundombinu, hasa katika jimbo hilo na Wilaya ya Ilala kwa ujumla. Amesema Serikali itajenga barabara za kilomita 250 kupitia mradi wa Uboreshaji wa Mkoa wa Dar es Salaam (DMDP).

Awali,  Kamoli amesema miundombinu inawaathiri wananchi wa jimbo hilo, akimuomba kuongeza nguvu kuhusu utekelezaji wa mradi DMDP, awamu ya pili utakaokuwa mkombozi wa kutibu tatizo hilo.

“Mheshimiwa mgeni rasmi (Makalla), licha ya Ilala kuongoza kwa mapato, ndiyo tunaongoza kwa kutokuwa na miundombinu hasa barabara katika jimbo la Segerea,  tunaomba ulibebe hili utusaidie,” amesema Kamoli.

Mbali na hilo, Kamoli amegusia suala la changamoto ya bomoabomoa ya  Mtaa wa Kipunguni, akisema licha ya kulifikisha kwenye mamlaka husika, bado halijapata ufumbuzi,  hivyo kumuomba Makalla jambo hilo lifikishe mwisho na wananchi wapate haki zao za kulipwa fidia.

Kutokana na hilo, Makalla amempigia simu Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliyekiri kulifahamu suala hilo na kuahidi kuanzia Agosti 2024, wataalamu wa wizara hiyo wataanza taratibu za malipo kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Ilala, Said Sidde amesema namna wananchi waliojitokeza katika mkutano, hakuna shaka chama hicho kitaibuka kidedea katika chaguzi zijazo kuanzia wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba 2024.

Related Posts