SAKILU: Kamba ndiyo itaamua hatima yangu Olimpiki

MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Jackline Sakilu ni miongoni mwa nyota ambao wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mashindano ya Olimpiki ambayo yatafanyika mwezi huu Paris Ufaransa.

Sakilu ambaye ni mwanariadha wa mbio za kilomita 42 anatokea katika timu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), akiwa ni miongoni mwa wanariadha wanne watakaokwenda kushiriki katika mashindano hayo.

Wengine ni Magdalena Shauri, Alphonce Simbu wote kutoka JWTZ na Gabriel Geay kutoka uraiani ambapo Sakilu alifuzu kupitia mbio za Shanghai Marathon za China, Novemba 26,2023 akitumia muda wa saa 2:26:50.

Muda ambao pia alikuja kuuboresha kupitia mbio za Chang’an Automobile Chongqing za huko China pia ambazo zilifanyika Machi 24, mwaka huu akitumia muda wa saa 2:21:27.

Bingwa huyo wa taifa wa nusu marathoni akiwa na rekodi ya muda wa 01:06:04 anakwenda kushiriki Olimpiki ya kwanza katika historia ya maisha akitazamiwa kukutana na ushindani mkali kutoka kwa wakimbiaji wa mataifa ya Kenya, Uganda na Ethiopia.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 37 ambapo anaelezea maandalizi na mikakati kuelekea Olimpiki.

Anasema maandalizi kwa upande wake yanaendelea vyema chini ya kocha wa timu ya taifa Antony Mwingereza ambaye pia ni kocha wa JWTZ ambapo kutokana na namna ambavyo anaendelea kujifua kila kitu kiko katika mstari kilichobaki ni kwenda kupambana.

Sakilu anaenda Paris akiwa na rekodi ya taifa ya nusu marathoni ambayo aliivunja Februari 24 mwaka huu katika mbio za Ras Al Khaimah za Falme za Kiarabu akishika nafasi ya tatu kwa muda wa mwaka jana kwa kutumia muda wa 01:06:04 na kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Magdalena Shauri kwa 01:06:37.

Anasema licha ya kwamba anaenda kukimbia mbio ndefu lakini rekodi hiyo inampa matumaini makubwa kwenda kufanya vizuri kwa sababu mbio zinaanzia chini hivyo ukiwa na muda mzuri huku chini hata huko juu inakupa mwanga mzuri.

“Ninaamini kabisa kutokana na hii rekodi yangu nitaenda kufanya vizuri na kurudi na medali”.

Olimpiki ya mwaka huu inasemekana itakuwa ngumu kwani mabingwa mbalimbali watakuwepo akiwemo mshindi wa mbio za Boston Marathon mara mbili mfululizo mwanadada Helen Obiri kutoka nchini Kenya lakini Jackilne yeye anasema.

“Kati ya hao wakali naamini na mimi ni mmoja wapo hivyo kamba ndio itaamua natambua Hellen Obiri ni mshindani lakini hata mimi ni mshindani pia wala simuogopi”

“Unajua kwenye mashindano lolote linaweza kutokea na kujiamini kwako ndio itakufanya uweze kushinda niseme tu kama uzima utakuwepo kama sasa kitaeleweka”.

Anasema licha ya kwamba wapo mastaa wengi ambao watampa ushindani mkubwa Olimpiki lakini nyota ambaye ana muhofia ni mwanadada Hellen Obiri kutoka Kenya kwani katika mbio ngumu yeye ndio anaziwezea lakini wengine ni wale wa mbio rahisi hivyo anaamini ushindani utakuwepo.

Anatumia jukwaa hili kuwaahidi Watanzania medali na kuweka rekodi ambayo haijavunjwa tangu 1980 ambapo ilipata medali mbili za shaba kupitia kwa Suleiman Nyambui aliyeshika nafasi ya pili katika mbio za mita 5000 na nyingine ikichukuliwa na Filbert Bayi katika mbio za mita 3000.

Sakilu anasema kitu ambacho hawezi kusahau kwenya maisha yake katika riadha ni kukatishwa tamaa na viongozi na ndicho ambacho kiliwahi kumvunja moyo na kumfanya kidogo aache mbio.

“Uvumilivu ni kitu muhimu sana, maneno yanaswemwa na utaswemwa sana sisi ni binadamu, wanariadha ambao wanachipukia inatakiwa wawe wavumilivu ili kufanikisha kile mabcho unakuwa umekilenga.”

Sakilu mwenye umri wa miaka 37, anasema umri kwake  ni namba wala sio kigezo cha kumfanya aamini kwamba hawezi kukimbia, bali ataendelea kukimbia mpaka  atakapochoka mwenyewe.

“Sasa hivi hata ukiangalia umri wangu na muda ambao nakimbia watu wengi wangekuwa wameshaacha na hata wengine ambao waliacha huko nyuma hawakufikia umri ambao ninao sasa,” anasema.

Mwanariadha huyo anasema ili Tanzania kuendelea kupiga hatua jambo kubwa inatakiwa wanariadha wenyewe kujitambua kwani katika mchezo huo kuna changamoto mbalimbali ambazo huwa wanakumbana navyo, ambapo kama hutakuwa makini lazima utajikuta uko palepale na hausogei na mafanikio kuyaona kwa wengine kutoka mataifa mengine.

“Kama unataka kufika juu lazima kwanza kwenye masikio yako weka pamba kabisa ziba alafu kingine ongeza bidii huku kwetu utapigwa majungu lakini ukisimama imara unatoboa tu.”

Anasema wanawake wana shauku ya kupata medali kwani tangu Tanzania ilipoanza kushiriki Olimpiki 1964 ni medali mbili pekee ndizo zimepatikana ambazo ni za shaba na zote zililetwa na wanaume -Filbert Bayi na Suleiman Nyambui.

“Tuna shauku sana ya kupata medali kwani ukiangalia kwa sasa wanaona wanaume ndio kila kitu na ukiangalia pia tunaongozwa na Rais mwanamke tutaenda kumwaminisha kwamba tunaweza,” anasema.

Sakilu anasema wanariadha wa Tanzania ambao wamekuwa wakiiwakilisha katika mashindano makubwa kuwa ni walewale kila siku inatokana na kujisahau.

“Wengi wamesahau misingi ya mbio kwa maana inatakiwa uanzie chini, viwanjani ili kuweza kujitengenezea shepu nzuri ya kuja kufanya vizuri katika mbio za barabarani,” anasema.

“Nilianza na mita 800 hadi 1500 na ndio imekuwa mwanzo wangu mzuri hadi kuwa staa wa nusu marathoni hapa nchini.

“Sasa unakuta mtu anakuja mjini yeye anachotaka cha kwanza aende marathoni na unajua marathoni Tanzania sasa hivi ndio zinaonekana zina pesa.

“Sasa mtu anakuja moja kwa moja anataka na yeye awe staa kama Simbu kwahiyo lazima aende marathoni kwahiyo hicho kinaua vipaji kwa sababu hauwezi kutoka chini ukaenda juu moja kwa moja”.

Anaongeza kuwa kule juu ndio pa kumalizia mbio kwani hauwezi kuwa na umri wa miaka 18,20 au 22 ujafanya vizuri chini lazima juu utashindwa kufurukuta.

“Yani mtu utakuwaje bora ikiwa kila mbio unataka ushiriki ,mbio zote zinakuwa za kwako lazima utapunguza kasi yako kikubwa tuangalie mbio za kukimbia.”

Anasema mazoezi yake huwa ni yaleyale ya siku zote ambayo amekuwa akiyafanza kwa bidii ili kufanikisha kila mbio ambazo amekuwa akishiriki, kwa maana ya kushinda ambapo kuna wakati anakwenda umbali mrefu zaidi na wakati kulingana na programu ya mwalimu.

“Kuna wakati pia naenda gym kujiweka fiti saidi lakini yote yanakuwa ni program ya mwalimu yeye ndo anajua hapa nimeenda spidi ndogo na hapa iko sawa lengo huwa sikuzote ni medali kwa maana ya kushinda.

“Mara zote huwa lazima mrejesho kwa mwalimu uwepo na nashukuru kocha wangu amekuwa ni msaada mkubwa sana kwangu katika kuboresha na kuongeza kiwango changu,” anasema.

Related Posts