Kijana Shadrack Yusuph Chaula (24) mkazi wa kijiji cha Ntokela kata ya Ndanto Tukuyu wilayani Rungwe, ameachiwa huru kutoka mikononi mwa jeshi la magereza baada ya ulipa faini ya Sh million tano kutokana na hatia aliyokutwa nayo ya udanganyifu wiki iliyopita. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Chaula amelipa fedha hizo baada ya kuchangwa na wanaharakati na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Tarehe 4 Julai mwaka huu na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, Shamla Shehagiro alimhukumu Chaula kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya Sh milioni tano baada ya kukiri kosa la kuandaa na kusambaza taarifa za uongo.
Baada ya hukumu hiyo, kijana huyo alienda gerezani kuanza kutumikia kifungo cha miaka miwili ndipo baadaye wanaharakati wakaanzisha mchango ili kupata fedha za kumtoa gerezani na kufanikiwa kupata zaidi ya Sh milioni sita.
Jopo la mawakili na watu mbalimbali wamefika katika viunga vya magereza ya Ruanda jijini Mbeya ambapo baada ya kushughulikia mambo kadhaa kijana Shadrack Chaula ameachiwa na kwenda kuendelea na maisha yake ya kawaida.
Baada ya kutoka gerezani Shadrack Chaula amewashukuru wananchi wote kwa kuungana naye na kumsaidia kuhakikisha anatoka gerezani.
Wakili wa kujitegemea Michael Mwangasa, amesema wameshirikiana kuona kijana huyo anaachiwa huru kwa kulipa faini tajwa na mahakama.
Naye Twaha Mwaipaya kwa niaba ya walioanzisha ukusanyaji fedha hizo, ameushukuru umma wa-Tanzania kwa kuungana kuhakikisha kijana huyo anaepuka adhabu ya jela.
Katika kesi hiyo, mawakili wa Serikali, Veronica Mtafya na Rosemary Mginyi waliieleza Mahakama kuwa tarehe 22 Juni 2024 katika eneo la Ntokela mshtakiwa alisambaza video zenye taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa Tik Tok, kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandaoni.
Chaula ambaye pia ni msanii wa uchoraji, video yake ilisimbaa mtandaoni tarehe 22 Juni 2024 akiwa anachoma moto picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, suala ambalo lilikemewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na kuagiza akamatwe.