Dar es Salaam. Wazalishaji wa sukari nchini (TSP) na Serikali wamekubaliana mambo sita kwa ajili ya kulinda sekta hiyo ikiwemo kupitia upya Sheria ya Sukari ya mwaka 2001.
Pia, wametaka kuimarishwa kwa mawasiliano kati yao na Serikali, kulindwa kwa sukari inayozalishwa nchini dhidi ya ile inayotoka nje ya nchi, sukari ya nakisi kuingizwa kwa wakati, kuwapo kwa utaratibu mzuri wa kuingiza sukari na sera zinazotabirika.
Wazalishaji hao wameyasema hayo leo Jumatatu Julai 8, 2024 jijini hapa walipokutana na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Keneth Bengesi, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geliad Teri.
Mkutano huo unafanyika ikiwa ni siku chache tangu wazalishaji hao kufanya mkutano na vyombo vya habari na kulalamika kutopewa nafasi ya kusikilizwa na Serikali juu ya sakata la sukari, huku wakikana kutumia uhaba wa bidhaa hiyo kujinufaisha.
Akizungumza kwa niaba ya pande zote Profesa Mkumbo amesema mapendekezo ya mapitio ya Sheria ya Sukari ya Mwaka 2001, Serikali imeyapokea na itayafanyia kazi.
“Hatuwezi kusema vipengele moja kwa moja, ila wao walikuwa wameomba, kuna haja ya kupitia upya sheria ya sukari ni ya muda mrefu ni ya miaka 20 iliyopita na hapa katikati kulikuwa na mambo mengi yametokea,” amesema Mkumbo.
Amesema wizara husika itaweka utaratibu utakawajumuisha wazalishaji hao ili kuweza kupitia kipengele kimoja baada ya kingine kuifanyia marekebisho sheria hiyo kwa kuwa wao ni wadau wa kwanza.
Naye msemaji wa Kampuni ya Bakhresa Group na Mkurugenzi wa Bagamoyo Sugar, Hussein Sufian amesema sheria hiyo ilitungwa wakati Serikali imeanza kufanya ubinafsishaji wa viwanda, hivyo kuna mambo mengi yametokea hapa katikati.
“Ni utaratibu wa kawaida kila baada ya muda fulani watu hubadilisha sheria zao ili ziendane na mazingira ya wakati huo, sheria tuliyonayo ni ya tangu mwaka 2001 ni zaidi ya miaka 23, hii ndiyo sababu iliyofanya sisi wazalishaji tuone haja ya kufanywa kwa mabadiliko katika sheria hiyo,” amesema Sufian.
Hata hivyo, Profesa Mkumbo amesema wazalishaji hao wamemkumbusha umuhimu wa kulinda sekta ya viwanda dhidi ya bidhaa zinazotoka nje.
Hivyo amewasisitizia kuwa Serikali itahakikishia inalinda viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazohitajika sana nchini, kwa lengo la kuhakikisha nchi inajitosheleza katika uzalishaji.
“Katika eneo la sukari tunakwenda vizuri, kwa sasa uzalishaji ni takribani tani 460,000 na matarajio kwa miaka miwili ijayo suala la nakisi ya sukari nchini litakuwa historia,” amesema Profesa Mkumbo.
Katika kulinda viwanda vya ndani pia wazungumzaji walitaka Sera na sheria za msingi zinazotabirika ili kulinda sekta hiyo huku Serikali ikiahidi kushughulikia suala hilo.
Kuhusu uagizaji wa sukari pia walitaka kuwapo kwa takwimu sahihi za nakisi ya sukari nchini kisha bodi na wazalishaji wakae na kukubaliana juu ya takwimu hizo.
Baada ya kukubaliana pia walitaka kuwapo kwa utaratibu mzuri wa namna ya kushughulikia nakisi kupitia waagizaji.
Kwa sasa Serikali imebadilisha utaratibu na imeupa Wakala wa Uhifadhi wa Chakula wa Taifa (NFRA) mamlaka ya kuagiza sukari ya nakisi ili kuondoa mkanganyiko uliokuwa ukitokea awali.